Jela maisha kwa kulawiti mtoto wa miaka 12 Mufindi

Mufindi. Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, imemuhukumu kifungo cha maisha jela mkazi wa kijiji cha Ibatu Kata ya Igowole Tarafa ya Kasanga, Michael John Ngunda (27) baada ya kumtia hatiani  kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (12).

Hukumu hiyo imetolewa jana Machi 12, 2025 na Hakimu Mkazi Sekela Kyungu, katika kesi  ya jinai ya mwaka 2024 iliyokuwa ikimkabili Michael.

Akisoma hukumu hiyo Kyungu amesema ameridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka kuwa umeweza kuthibitisha shitaka dhidi mshtakiwa bila kuacha mashaka yoyote, kupitia mashahidi wanane na vielelezo viwili vilivyowasilishwa na kupokewa na Mahakama.

Polisi wakiwa wameimarisha usalama katika mahakama hiyo baada ya mtuhumiwa Michael akiwa tayari ameingia ndani ya gari hilo la Polisi. Picha na Mary Sanyiwa

“Kutokana na ushahidi  uliotolewa  Mahakama  imemtia hatiani mshtakiwa, Michael John Ngunda, kwa kosa moja la kulawiti ambalo ni kinyume na kifungu 154 (1)(a) cha Sheria ya Kanuni ya  Adhabu,  Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022, amesema Hakimu Kyungu.

Kabla ya Hakimu kutamka adhabu baada ya kumtia hatiani, Wakili wa Serikali Simon Masinga amesema upande wa mashitaka hauna kumbukumbu zozote za makosa ya jinai ya nyuma ya mshtakiwa, lakini akaiomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa Sheria.

“Naiomba Mahakama izingatie kifungu cha 154 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu katika  kutoa adhabu hiyo kwa sababu matukio hayo yamekuwa yakitokea kwenye jamii ili iwe fundisho kwake pamoja na jamii nzima.” amesema Masinga.

Mshtakiwa katika utetezi wake dhidi ya adhabu ameieleza tu Mahakama kuwa yeye hakufanya kosa hilo.

Hakimu Kyungu baada ya kusikiliza pande zote amesema kuwa Mahakama imezingatia utetezi wa pande zote lakini pia sheria katika kutoa adhabu

“Hivyo, mahakama hii baada ya kumtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa inamuhukumu adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela,” amesema Hakimu Kyungu na kuongeza kuwa haki ya rufaa iko wazi kwa upande wowote usioridhika.

Katika kumbukumbu za Mahakama katika hukumu hiyo, mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 19,2024 huko katika kijiji cha Ibatu Kata ya Igowole Tarafa ya Kasanga  wilayani hapa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu hizo, siku hiyo mshtakiwa  alimuingilia kinyume na maumbile  mtoto huyo wakati akielekea shuleni na rafiki zake.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka ambaye ni mtoto mwathirika aliieleza anamfahamu mshatakiwa kwa sura yake,  kwani aliwakimbiza  akiwa pamoja na rafiki yake.

Alieleza kuwa, Februari 19 muda wa asubuhi  akiwa anakwenda shuleni  na marafiki zake, mshtakiwa alitokea kwa nyuma  akiwa na mwenzake upande mwingine na kuongea kwa sauti kuwa kamata hao, ndipo yeye pamoja na rafiki zake  wakaanza kukimbia.

Kwa mujibu wa ushahidi wake huo, baada ya kukimbia na kuelekea uelekeo tofauti yeye alijikuta yupo peke yake ndipo mshtakiwa alimchota mtama  kisha akaanguka chini.

Baada ya kuanguka mshtakiwa alimkamata  na kumpeleka maeneo ya bondeni kisha alivua suruali yake  na kaptula yake aliyokuwa amevaa  na kumueleza kwamba ainame.

Mshtakiwa huyo alichukua chupa kidogo kilichokuwa na maji mfano wa kimiminika na kumpaka eneo la haja kubwa  mara mbili  baada ya hapo alitoa uume wake na kuingiza katika sehemu yake ya haja kubwa.

Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka, ilimuona mshtakiwa kuwa ana kesi ya kujibu, hivyo alipewa nafasi ya kujitetea.

Mshtakiwa katika utetezi wake alikana kutenda kosa hilo kama ilivyodaiwa na kwamba upande wa mashitaka ulitakiwa kuthibitisha shitaka lake bila kuacha shaka lolote lakini ulishindwa kufanya hivyo.

Gari la Polisi likiondoka katika eneo la Mahakama baada ya mtumuhiwa Michael kuhukumiwa kifungo Cha maisha katika mahakama ya Wilaya ya Mufindi. Mary Sanyiwa

Alisema kwamba siku ya tukio yeye alikuwa ameenda kwa mama yake  kumsaidia kuchambua mkaa   na kujaza kwenye mifuko ambayo ndio biashara yake.

Alisema kuwa katika kazi hiyo alikuwa yeye, dada yake,  baba yake pamoja na mama yake na  kwamba hakutoka kabisa nyumbani  na wala hamfahamu kabisa mwathirika.

Hata hivyo, akizungumzia utetezi huo wa mshtakiwa, katika hukumu hiyo amesema kuwa mshtakiwa alieleza mahakama tu kuwa siku hiyo ya tukio hakuwepo eneo la tukio bali alikuwa nyumbani.

Hata hivyo, Hakimu Kyungu amesema kuwa mshtakiwa alishindwa kuwaleta mashahidi wake (aliowataja kuwa alikuwa anafanya nao kazi siku hiyo) ili kuthibitisha alichokieleza mwanzo ili kuitetea hoja yake.

Kutokana na hukumu hiyo  baadhi ya wananchi mjini Mafinga, Atupele Chaula amesema kuwa matukio hayo yana athari kubwa katika jamii hususan kwa watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo.

“Matukio hayo sio mazuri yana athari kwa jamii hivyo wazazi wanatakiwa kufahamu mienendo ya watoto wao, ikiwamo wapo wapi, anafanya nini ili kupunguza kuendelea kutokea vitendo vya namna hiyo katika jamii,” amesema  Chaula

Related Posts