Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limewatahadharisha vijana na watu wanaojihusisha na kughushi vyeti vya kuhitimu mafunzo yanayotolewa na jeshi hilo, kuacha kufanya hivyo na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
JKT imekuwa ikitoa mafunzo kwa kundi la lazima (mujibu wa sheria), ambayo hutolewa kwa muda wa miezi mitatu na kundi la kujitolea ambapo vijana hufanya mafunzo kwa muda wa miaka miwili.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Machi 13, 2025 na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala la JKT, Kanali Juma Mrai alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Amesema hivi karibuni jeshi hilo limebaini uwepo wa baadhi ya vijana ambao sio waaminifu ili kujipatia ajira katika taasisi na kampuni ya inayohitaji watendaji waliopitia mafunzo ya JKT.
“JKT linapenda kuutaarifu umma wa Watanzania kuwa watakaobainika kughushi cheti cha JKT kwa matumizi yoyote yale hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” amesema.
Kanali Mrai amesema JKT lipo tayari kutoa ushirikiano kwa taasisi na kampuni yoyote inayohitaji uhakiki wa vyeti vya JKT kwa watumishi wao waliopitia mafunzo hayo.
Amewakumbusha Watanzania kuwa nafasi kujiunga na mafunzo hayo hutangazwa kila mwaka katika vyombo vya habari na mitandao ya jamii hapa nchini.
“Hivyo wananchi waepuke kutapeliwa kwa namna yoyote ile ikiwemo kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno katika simu zao, kupigwa simu na kutakiwa kutoa kiasi fulani cha fedha ili kupata nafasi hizo,” amesema.
Kanali Mrai amewaomba wananchi watakaopokea ujumbe wa namna hiyo kutoa taarifa haraka katika kambi yoyote ya jeshi au kituo chochote cha polisi kilicho karibu nao ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.