Tanga. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imetaka kuwe na mfumo wa kuziunganisha Mamlaka ya Bandari, barabara na reli kwa ajili ya kuwa na miradi endelevu itakayoleta tija jijini Tanga.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso wakati wa kufanya majumuisho baada ya kutembelea na kukagua miradi ya kiwanja cha ndege Tanga, reli na Bandari ya Tanga, leo Alhamisi Machi 13, 2025 ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya kamati hiyo mkoani humo.
Kakoso amesema mifumo itakapoziunganisha mamlaka hizo italeta tija na fursa za uchumi jijini humo.

Kakoso ambaye aliiongoza kamati hiyo kufanya ziara ya saa sita kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi saa 8:30 mchana katika miradi hiyo amemtaka pia Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya kuhakikisha kiwanja cha ndege cha Tanga kinajengwa kwa haraka huku akimsisitiza kuihakikisha mikataba wanayoingia.
“Naibu waziri wa ujenzi, kwenye eneo la mradi wa uwanja wa ndege unaosimamia na Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) hakikisheni mikataba mnayoingia, ili Serikali isiingie kwenye gharama zaidi,” amesisitiza na kufafanua hilo kwamba. “Tunaweza kuingia mkataba wa Sh95 bilioni lakini hadi mradi unakuja kukamilika unakuwa umetumia zaidi ya Sh100 bilioni,” amesema.
Awali, Naibu Waziri, Kasekenya alisema kiwanja hicho kitajengwa na mkandarasi ambaye taratibu za kumpata zipo kwenye hatua za mwisho na atasimamiwa na mhandisi mshauri, ambaye atafanya kazi ya mapitio ya usanifu na usimamizi wa mradi.
“Ujenzi huu ukikamilika utapandisha hadhi uwanja huu kutoka Daraja 2C kwenda 3C na kuwa na uwezo wa kupokea ndege za aina ya Bombandier Dash 8 – Q400,” amesema.
Kwa mujibu wa Kasekenya, tayari Serikali imelipa fidia ya Sh2.654 bilioni kwa waathiriwa wa mradi huo.
Pia ametaja faida zake utakapokamilika ni pamoja na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na mikoa jirani, kurahisisha shughuli za kibiashara, za kijamii, utakuza uchumi mkoani humo, kusaidia shughuli za utafiti wa uvuvi na kilimo na kukuza utalii wa mkoa na Taifa.

Hata hivyo, Kamati imeshauri pia jengo la abiria la uwanja huo ambalo lipo kwenye ramani liongezwe liwe na uwezo wa kubeba abiria 250 hadi 300 na si 150.
Akieleza historia ya kiwanja hicho, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema kilijengwa mwaka 1942 wakati wa ukoloni na kimeendelea kutumika hadi sasa.
“Kiwanja hiki kina barabara mbili, ya lami ina urefu wa mita 1,268 na upana mita 30 na nyasi mita 1,085,” amesema.
Amesema ukikamilika utakuwa na faida kubwa na kubainisha hivi sasa idadi ya abiria kutumia kiwanja hicho inaongezeka sanjari na idadi ya miruko.
“Mwaka 2020 idadi miruko ilikuwa 1,688 na abiria walioshuka 5,629 na walioondoka 5,333 mwaka 2024 idadi ya miruko iliongezeka hadi 2,678 abiria walioshuka 8,824 na walioondoka 9,537.
“Tunaamini kwa msukumo na ushauri wenu mradi huu ukikamilika utakuwa na faida kubwa na utakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na miradi mingine inayoendelea ya bandari, bomba la mafuta na reli,” amesema.
Mifumo ya reli, barabara na bandari
Kamati hiyo pia imeshauri mamlaka ya bandari ianze kuweka mifumo ya kuiunganisha na reli na barabara ili kuwe na miradi endelevu itakayozidi kufungua fursa mbalimbali za mkoa huo.
“Kitendo cha kufikiria kuanza kujenga barabara ya kutoka Tanga, kibrashi hadi Singida japo itakuwa inashirikisha wawekezaji ambayo itakuwa ya kulipia kutafungua fursa nyingi.
“Mamlaka ya Bandari mpange mkakati wa kushirikiana na Wakala wa Barabara (Tanroads) na Serikali,” amesema.
Upande wa Shirika la Reli, Kakoso amemuomba naibu waziri wa uchukuzi akieleza kwamba pesa zinazotolewa kwa ajili ya ukarabati wa reli ya Ruvu, Tanga inayokwenda hadi Kilimanjaro, Arusha ni ndogo akibainisha reli hiyo ni muhimu na itafungua uchumi mkubwa.
“Kipande cha reli cha Ruvu, Tanga, Kilimanjaro hadi Arusha kitafanyiwa ukarabati mkubwa na kiwango cha pesa kinachotolewa ni kidogo, naibu waziri liangalie ili ukileta ripoti ije imekamilika,” amesema.
Kamati hiyo pia iliishauri mamlaka ya bandari kuangalia uwekezaji kwenye ardhi akibainisha unaofanyika jijini Tanga baada ya miaka 10 ijayo utapandisha zaidi thamani ya ardhi.
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema mkoa huo unanufaika na miradi mbalimbali ambayo inakwenda kufungua fursa kwa wananchi wa Tanga na Tanzania.