Kifo cha mwanafunzi Polisi, mzazi watofautiana

Muleba. Polisi Mkoa wa Kagera wamesema chanzo cha kifo cha mwanafunzi aliyekuwa akisoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Tumusime, Janeth Mbegaya (7) hakijatokana na kubakwa wala kulawitiwa.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Brasius Chatanda amesema hayo jana Alhamisi, Machi 12, 2025 baada ya uchunguzi wa kitabibu uliyofanywa na madaktari wa Hospitali Teule ya Rubya iliyopo wilayani Muleba kwa kushirikiana na polisi.

Uchunguzi huo umebaini kuwa kifo cha mtoto huyo kimetokana  na kukosa damu, maji na utumbo wake ulikosa chakula kwa muda mrefu.

“Uchunguzi wetu wa awali umebaini huyu mwanafunzi amefariki kwa sababu hizo siyo kama inavyodhaniwa na wanajamii maana sisi baada ya kupata taarifa tumefanya uchunguzi wa tukio hilo,” amesema kamanda huyo.

“Awali ulikuwepo uvumi na minong’ono kuwa huenda kifo chake kimesababishwa kuingiliwa kimwili na kulawitiwa lakini si kweli, wataalamu kitu kingine walichokibaini kuna mtoto mwenzake walikuwa wanaitana mke wangu mume wangu.”

Kamanda huyo amesema uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea.

Wakati Polisi ikieleza hayo, mama mzazi wa marehemu ambaye ni mkazi wa Muleba, Zaifath Fadhili amesimulia tukio hilo akisema alipokea taarifa kwa mara ya kwanza kuhusu kuumwa kwa mwanaye Ijumaa ya Machi 6, 2025 kutoka kwa mkuu wa shule hiyo, akidai anaumwa sana na hajiwezi.

Amesema mwalimu huyo alimweleza wamempeleka kituo cha afya Kaigara na kugundulika kuwa na ugonjwa wa malaria na amepatiwa dawa tangu Alhamisi ya Machi 5, 2025.

Baada ya hapo mama huyo amesimulia huku akilia kuwa siku hiyohiyo ya Ijumaa akapokea taarifa tena kuwa mwanaye aliyekuwa akiishi bwenini shuleni hapo amekimbizwa Hospitali ya Teule ya Rubya iliyopo wilayani Muleba baada ya kumalizia dozi na kujihisi vibaya.

“Siku Jumamosi, Machi 7, 2025 nilifika hospitalini hapo nikakuta mwanangu hajielewi, nilipoongea na madaktari wakaniambia kwa sasa wanajaribu kutafuta mishipa ya damu ili wamuhudumie zaidi.”

Amesema wakamuambua wanapata shida kuipata mishipa ya damu, lakini jioni wakamwambia imepatikana kichwani na wakamuwekea chupa zaidi ya tatu.

“Mwanangu alikuwa hajitambui, pia alikuwa na tatizo la kupiga kelele na baadaye usiku wa kuamkia Jumapili saa nane alitulia na wakaanza kumpatia dawa za malaria kwa njia ya sindano, kesho yake daktari aliniuliza anakula nikajibu hapana wakaleta mipira ya kupitia chakula walipomuwekea chakula ilishindikana mipira ilianza kurudisha vitu vyeusi mpaka wakashangaa,” amesimulia.

Aidha amesema alitoka na kwenda kunyonyesha mtoto nyumbani siku ya Machi 10, 2025 aliporudi akauliza hali ya mwanaye madaktari wakamuambia mtoto amefariki dunia wakati anaingiziwa mipira ya chakula.

Amesema kilichomuumiza zaidi ni kifo cha mwanaye kilichotokea bila kuongea naye kujua kilichosababisha anafikia hali hiyo na alipouliza utaratibu wa kusafirisha maiti kwenda nyumbani, daktari aliyekuwa akimuhudumia mgonjwa huyo alimuambia hawezi kuruhusu kwa sababu katika uchunguzi wa awali kuna viashiria vinaonesha dalili alibakwa na kulawitiwa hivyo wasubiri uchunguzi zaidi.

Baada ya yote, mwili huo ulikabidhiwa jana kwa wazazi wa marehemu ambapo mazishi yake yalifanyika jana hiyohiyo wilayani Muleba.

Related Posts