Kiongozi wa CCM kata auawa na wasiojulikana

Ileje. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Chitete wilayani Ileje Mkoa wa Songwe, Halisoni Mwampashi (62) amefariki dunia baada ya kuuawa na watu wasiojulikana.

Tukio hilo limetokea saa tatu usiku wa jana Jumatano, Machi 12, 2025 katika Kijiji cha Ntembo wakati Mwampashi anatoka kwenye virabu vilivyopo kijijini hapo maarufu Gezaulole.

Mwananchi limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga ambaye amesema bado hajapokea taarifa hizo kwa kuwa yupo nje ya ofisi na atafuatilia tukio hilo ili atoe taarifa rasmi.

Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya wanasiasa, wafanyabiashara na wanaharakati kutekwa au kuuawa na watu wasiojulikana maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia tukio hilo leo Alhamisi Machi 13,  2025, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Joseph Mwashitete amesema alipokea taarifa za kifo cha Mwampashi kutoka kwa mmoja wa wananchi.

Amesema alipokwenda eneo la tukio, aliwakuta watu wamekusanyika wakiwamo wake zake wawili marehemu na mtoto wao wa kiume, Jose Mwampashi.

Mwashitete amesema alifika eneo la tukio na kuwakuta wake za marehemu nao wakidai walipokea taarifa kutoka kwa mtoto wao Jose Mwampashi ambaye alikuta mwili wa baba yake chini akiwa tayari amefariki dunia.

Amesema mtoto wa marehemu ambaye ni Jose alitoka kwake jirani na nyumbani kwao kwenda kula chakula cha usiku lakini cha kushangaza alikuta mwili wa baba yake ukiwa njiani.

“Nilifika eneo la tukio majira ya saa tatu usiku na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha kichwani, ndipo nikatoa taarifa kituo cha polisi Itumba ambao walifika eneo la tukio haraka kisha kuuchukua mwili na kuuhifadhi mochwari katika Hospitali ya Wilaya Ileje iliyopo Itumba,” amesema Mwashitete.

“Hakuna taarifa zozote tulizopokea zikionesha chanzo cha mauaji ya mzee, sisi kama wananchi wa Ntembo tutaendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili wahusika wabainike na kukamatwa,” amesema Mwashitete.

Katibu mwenezi wa CCM Kata ya Chitete, Daima Silwamba amesema kifo hicho kimewashtua kwa kuwa,  alikuwa kiongozi aliyekuwa anategemewa ndani ya chama hususani kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Silwamba ameliomba Jeshi la Polisi kufuatilia zaidi ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.

“Niombe wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwabaini wahusika wa mauaji hayo, kwani vitendo hivyo havifai kwenye jamii zetu,” amesema Silwamba.

 Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM, Wilaya ya Ileje, Maoni Mbuba amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kama wanaona kuna tofauti baina yao wafike kwa viongozi wao ili waweze kusuruhishwa.

Mbuba amesema chama kinaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo cha kuuawa kwa kiongozi huyo.

Amesema na pindi wahusika watakapobainika hatua kali zichukuliwe ili kukomesha tabia za kujichukulia sheria mkononi.

Tukio kama hilo la kiongozi wa CCM lilitokea Desemba 3, 2024 kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Tawi la Machinjioni, Kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya baada ya Michael Kalinga kukutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa.

Katibu wa CCM Wilaya Chunga, Charles Jockel alipozungumzia tukio hilo alisema alipokea taarifa hizo kutoka kwa uongozi wa CCM Kata ya Makongorosi.

“Haijulikani alikuwa anakwenda au kurudi Makongorosi maana mwili wake umekutwa eneo la kuelekea Kata ya Mkola,” alisema Jockel.

Tukio jingie ni lile lililotokea Novemba 13, 2024 la kupigwa risasi hadi kufariki dunia kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki.

Taarifa zilieleza kuwa, tukio hilo lilitokea Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, Wilaya ya Iringa alipokuwa akiishi. Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga na alikofariki dunia.

Novemba 10, 2024 Katibu wa CCM, Kata ya Itumba wilayani Ileje, Mkoa wa Songwe, Huruma Ally alidaiwa kuvamiwa na watu wasiojulikana na kuvunjwa miguu.

Related Posts