Dodoma. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma imependekeza jimbo la Dodoma Mjini kugawanywa na kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi jana Jumatano Machi 12, 2025, Ofisa uchaguzi wa Jiji la Dodoma, Albert Kasoga amesema mgawanyo wa jimbo hilo umezingatia mambo yote muhimu ili kutoathiri hali ya kiuchumi ya jimbo moja kutoka kwa lingine.
Amesema mgawanyo huo utatoa majimbo mawili ambayo ni Jimbo la Dodoma Mashariki litakalokuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,187.9, wapiga kura 412,000, kata 20, mitaa 99, shule za msingi 59, shule za sekondari 25, vituo vya afya vinne na zahanati 20.
Jimbo la Dodoma Magharibi litakalokuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,290.6, wapiga kura 385,000 kata 21, mitaa 123, shule za msingi 49, shule za sekondari 21, vituo vya afya vitano na zahanati 21.
Hata hivyo, kwenye mapendekezo hayo madiwani wamependekeza majimbo hayo yaitwe Jimbo la Mtumba (Dodoma Mashariki) na Jimbo la Dodoma Mjini (Dodoma Magharibi)
Ambapo kata zilizopo Jimbo la Dodoma Mjini (Dodoma Magharibi) ni Majengo, Madukani, Nkuhungu, Kizota, Kilimani, Mbabala, Uhuru, Kikuyu kusini, Kikuyu Kaskazini, Hazina, Mnadani, Mkonze, Matumbulu, Nala, Chamwino, Chang’ombe, Chigongwe, Mbalawala, Zuzu, Ntyuka na Mpunguzi.
Na kata ambazo zipo Jimbo la Mtumba (Dodoma Mashariki) ni Kiwanja Cha ndege,
Makutupora, Ngh’ong’ona, Tambukareli, Makole, Mtumba, Dodoma makulu, Chahwa, Msalato, Iyumbu, Nzuguni, Ipagala, Miyuji, Ihumwa, Kikombo, Chihanga, Viwandani, Hombolo Makulu, Hombolo Bwawani na Ipala
Madiwani wa Jiji la Dodoma wamesema mapendekezo yao yakipitishwa watafurahi kwa kuwa jimbo hilo ni kubwa na lina kata nyingi za kuhudumia. Kwa sasa jimbo hilo linaongozwa na Anthony Mavumbe ambaye pia ni Waziri wa Madini.
Wendo Kutusha ambaye ni diwani wa viti maalumu amesema Jimbo la Dodoma Mjini lina kata 41 ambazo ni nyingi kulinganisha na majimbo mengine Tanzania, ambapo yana jumla ya kata nane tu.
Amesema kama mapendekezo yao yatapitishwa wananchi watakuwa wamesogezewa huduma karibu, tofauti na sasa ambapo jimbo linatakiwa kuhudumia kata nyingi ambazo wakati mwingine hazifikiwi na huduma.
Kinachofanyika Dodoma ni sawa na maeneo mengine ambayo yanaendelea na utaratibu wa kupendekeza kugawanywa kwa majimbo.
Hatua hiyo inatokana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutangaza kuanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi.
Katika maandalizi hayo, INEC ilisema itaanza kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali Februari 27 hadi Machi 26, mwaka huu.
INEC ilitangaza utaratibu huo Februari 26, 2025 ambapo Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma alisema Tume hiyo itaanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi hadi Machi 26, 2025.
Kwa sasa, Tanzania ina jumla ya majimbo ya uchaguzi 264, Tanzania Bara yakiwa 214 na Zanzibar 50.