Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amempa miezi miwili (sawa na siku 60) mkandarasi wa jengo la Tamisemi kukamilisha ujenzi baada ya kuchelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa sita, litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wafanyakazi 600, ulianza Oktoba 2021 na ulitakiwa kukamilika mwaka 2023 huku gharama zikiwa Sh20.2 bilioni.
Mchengerwa ametoa agizo hilo leo, Alhamisi Machi 13, 2025, baada ya kutembelea ujenzi wa jengo hilo linalojengwa katika Mji wa Serikali wa Mtumba, jijini Dodoma.
“Mkandarasi aliyepewa ujenzi wa jengo hili amechelewesha ujenzi kwa kipindi cha mwaka mmoja. Baada ya kuzunguka, tumegundua maeneo mengi ujenzi umekamilik, na kwa mujibu wa mkandarasi, ujenzi umefikia asilimia 80,” amesema.
“Tumekubaliana jengo hili likamilike na watumishi wa ofisi ya Rais waanze kutumia mwezi wa sita (Juni), kwa hiyo tumewapa maelezo. Tutakapoondoka hapa, wakae wajipange, wafanye kazi usiku na mchana. Hakutakuwa na nyongeza ya muda, Katibu Mkuu,” amesema.
Mchengerwa amesema hakuna sababu ya jengo hilo kuchelewa kukamilika kwa sababu majengo mengine yaliyojengwa katika mji huo yameshakamilika na kuanza kutumika.
Amesema tayari mkandarasi huyo ameshalipwa asilimia 81 ya malipo yake.
“Nitazungumza na waziri wenu. Haiwezekani nyongeza ya mwaka mzima kama jengo lilitakiwa kukabidhiwa mwaka 2023 lakini hadi leo 2025 halijakabidhiwa. Ina maana huko kwenu kuna uzembe, nyinyi watendaji siyo wizarani,” amesema.
Amesema kama kwenye shirika hilo kuna kulegalega, sasa waongeze jitihada na wafanye kazi saa 24. Pia, amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Tamisemi kutembelea mara kwa mara ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati.
Naye Kaimu Meneja wa mradi kutoka Vikosi vya Ujenzi vilivyo chini ya Wizara ya Ujenzi, ambaye ni mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Deogratius Machupa, amesema wamepokea maelekezo na wanaahidi kuyatekeleza.
“Tunasema kuwa ifikapo Juni mosi 2025, jengo litakuwa limekamilika na tayari kwa matumizi,” amesema.
Jengo hilo ni miongoni mwa majengo yanayojengwa katika mji huo wa Serikali baada ya Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli, kutangaza kuwa Serikali inahamia jijini Dodoma Julai 25, 2016.
Awamu ya kwanza ya ujenzi huo, ambayo ilihusisha majengo ya wizara 23, ilianza Novemba 28, 2018, na kukamilika Machi 22, 2019, ambapo Sh39.387 bilioni zilitumika.
Awamu ya pili ilianza Desemba 2021, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliidhinisha Sh300 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya wizara na miundombinu mbalimbali katika mji huo.