Mechi zilizobaki Ligi Kuu Bara za jasho na damu

UKIWEKA kando mechi za viporo ikiwamo Dabi ya Kariakoo, asilimia kubwa ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zimeshuka dimbani mara 23, bado saba kuhitimisha msimu huu wa ligi hiyo. Hiyo inazifanya timu nyingi kuzipigia hesabu kali pointi saba zilizobaki ili kuangalia hatma yao.

Kesho Ijumaa, kuna mchezo mmoja wa kiporo, Simba itaikaribisha Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam. Simba kwa sasa imecheza mechi 21, ina viporo viwili dhidi ya Dodoma Jiji na Yanga na ndiyo timu iliyocheza mechi chache zaidi ya zingine. Dodoma Jiji na Yanga kila zina viporo pia ambapo zote zitakabiliana na Simba.

Wakati ligi hiyo ikitarajiwa kuendelea rasmi Aprili Mosi mwaka huu kwa kuchezwa raundi ya 24, kuna hesabu kali zinapigwa na timu shiriki, hasa zile ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini pia zinazozania ubingwa na nafasi nne za juu.

Hesabu hizo zimekaa kimkakati kwani mechi zilizosalia zinahitaji umakini mkubwa kuzicheza kutokana na ushindani uliopo tangu duru la pili lilipoanza.

Yanga na Simba zinakimbizana pale juu katika kuwania ubingwa, huku Azam na Singida Black Stars zinataka kubaki nne bora wakati Tabora United ikiifukuzia nafasi ya nne kwa kasi.

Kule chini, KenGold inapambana kujinasua kutoka mkiani ikiwa ndiyo timu iliyokaa hapo kwa muda mrefu kuanzia duru la kwanza hadi sasa. Ukiachana na KenGold, timu zinazoshika nafasi kuanzia ya sita kwa sasa roho mkononi muda wowote mambo yanaweza kubadilika na kujikuta sehemu mbaya zaidi kama zikishindwa kuchanga vizuri karata zake.

Kwa hesabu za haraka ukiiondoa Yanga inayoongoza msimamo wa ligi kwa pointi 58 ikifuatiwa na Simba, Azam, kisha Singida Black Stars, timu zinazofuatia zote bado hazina uhakika wa kusalia kwenye ligi kulingana na mechi zilizobaki.

Hiyo inatokana na kwamba, Tabora United iliyopo nafasi ya tano ikikusanya pointi 37, inaweza kufikiwa na KenGold ambayo hivi sasa inaburua mkia na pointi zake 16 kwani mechi saba zilizobaki zenye pointi 21, kimahesabu Tabora United ikipoteza zote na KenGold ikishinda zote basi itafikisha 37, ingawa isiwezakane kutokea hivyo kutokana na mwenendo wa Tabora United kuwa mzuri hadi kuifanya kuitishia Singida Black Stars.

Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, amenukuliwa akisema wanachokifanya kwa sasa ni kuikimbiza Azam na kuikimbia Tabora United, lengo ni kufikia malengo yao ya kumaliza nafasi nne za juu.

“Pointi nne zaidi yetu walizonazo Azam FC, tukichanga vizuri karata zetu tunaweza kufikia lakini hivyo hivyo kwao wakichanga vyema karata wana uwezo wa kutukimbia na kutuacha mbali zaidi, pia ipo hivyo kwa Tabora United ambayo imekuwa ikionyesha ubora kwenye michezo yao.

“Huu ni mzunguko wa lala salama tuna kikosi bora na kipana, ni wakati wa kuonyesha bila kujali mazingira yaliyopo na wachezaji wanatambua malengo ya Singida Black Stars tutapambana hadi tone la mwiosho ili kuhakikisha tunapata kile tunachokitaka.”

Kocha huyo raia wa Kenya, ameizungumzia ligi hasa kipindi hiki cha lala salama akisema: “Hakuna mchezo mwepesi, hata KenGold ambayo ni ya mwisho kwenye msimamo sio ya kuichukulia poa, ni timu ambayo inaingiza uwanjani wachezaji 11 kama sisi na wenye ubora na malengo.

“Ubora wa mchezaji mmoja mmoja na kikosi chetu kwa ujumla ni mzuri lakini hata wapinzani wetu pia wana kikosi kizuri, wanapambana kusaka nafasi ya kutwaa taji, wengine kucheza msimu ujao, huu ni mzunguko wa lala salama, ukidondosha pointi mwingine anasonga.”

Kwa Yanga na Simba ambazo zinaonekana zina nafasi kubwa ya kuwania ubingwa, hivi sasa zimepishana pointi nne, huku Yanga ipo juu ikiizidi Simba yenye mchezo mmoja mkononi. Endapo Simba ikishinda mechi ya kesho, itapunguza gepu na kuwa pointi moja.

Ikiwa hivyo, itaongeza ushindani zaidi ikizingatiwa kwamba Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kuwa ile mechi yao iliyoahirishwa Machi 8, itapangiwa tarehe nyingine ambapo mechi hiyo inaweza kutoa majibu ya nani atakaa juu.

Kwa sasa Yanga imebakiwa na mechi nane, kati ya hizo, tano itacheza jijini Dar es Salaam na tatu mkoani wakati Simba mechi mechi zake tisa zilizobaki, nane itacheza Dar es Salaam na moja pekee mkoani Mbeya dhidi ya KenGold.

Kucheza Dar mechi nane kwa Simba inaweza kuwa nafuu zaidi kwao kwani kati ya timu ilizobaki kucheza nazo, nane ilizifunga na kupoteza moja pekee dhidi ya Yanga.

Yanga ikikusanya pointi 12 kutoka sasa itafikisha 70 na Simba ikipata 16 itafikisha 70, hapo moja kwa moja itaifanya Azam kutokuwa na uwezo wa kumaliza hata nafasi ya pili kwani hivi sasa timu hiyo ina pointi 48 ikibakiwa na mechi saba ambapo ikishinda zote itamaliza ligi na 69. Kwa sasa tofauti ya Azam na Yanga ni pointi 10 huku ikiachwa pointi sita na Simba.

KenGlod yenye pointi 16, inahitaji miujiza kujinasua na janga la kushuka daraja katika mechi saba zilizobaki ambazo nne itakuwa nyumbani na tatu ugenini huku mechi hizo zikitarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na aina ya timu inazokwenda kukutana nazo.

Mchezo unaofuatia itakuwa nyumbani dhidi ya Azam, timu ambayo inapambana kumaliza nafasi za juu kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao huku hivi sasa uongozi wa klabu hiyo ukiwapa masharti nyota wake kuhakikisha kila mmoja atakayepewa nafasi ya kucheza anapaswa kupambana kweli kwani atakayezingua anaweza kuondolewa mwisho wa msimu.

Kutolewa kwao katika Kombe la FA na kuwa mbali katika mbio za ubingwa, ni sababu zilizowapa hasira mabosi wa Azam kiasi cha kupiga mkwara huo ambao unaweza kuwa hatari kwa wapinzani wao.

Baada ya hapo, itacheza na Tanzania Prisons, wapinzani wao wa jijini Mbeya ambao wanashika nafasi ya 15, moja kutoka waliyopo KenGold, lakini mchezo mwingine dhidi ya Pamba Jiji ambayo haijakaa sawa, nao utakuwa na ushindani mkubwa, hivyo kuna kazi ya ziada kwa Kocha Omary Kapilima na nyota wake wanapaswa kuifanya kuzipambania pointi 21 za mechi saba ili kuangalia namna ya kuepuka kurudi walipotoka. Zingine ni dhidi ya Dodoma Jiji, Coastal Union na Namungo.

Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya 15 na pointi 18 ikiizidi KenGold pointi mbili na kuachwa moja na aliye juu yake, Kagera Sugar, nayo ina mechi nne za kushikilia roho. Kwanza ni ile dhidi ya KenGold, pia dhidi ya Kagera Sugar, lakini Wajelajela hao watakabiliana na Yanga wanaousaka ubingwa wa ligi kwa mara ya nne mfululizo, pia itakabiliana na Singida Black Stars inayosaka nafasi ya kushiriki kimataifa. Mechi zingine ni dhidi ya KMC, JKT Tanzania na Coastal Union.

Kwa sasa msimamo ulivyo, KenGold na Tanzania Prisons, ndiyo timu zilizopo kwenye mstari wa kushuka daraja moja kwa moja kufuatia kushika nafasi ya 16 na 15, huku Kagera Sugar (14) na Pamba Jiji (13) zikiwa pale sehemu ya kucheza mechi za mtoano.

Ukiangalia tofauti ya pointi baina ya timu na timu, kuna gepu dogo sana kiasi cha kuifanya ligi hiyo inavyokwenda kila mechi ni ya kuitolea macho kwani ukifungwa au kutoka sare, aliyekuwa chini yako anaweza kukuacha muda wowote ukibaki unashangaa. Hiyo inatokana na kwamba kuanzia inayoshika nafasi ya 16 hadi ya sita, timu kwa timu zilivyo kwenye msimamo zimepishana pointi moja hadi tatu huku zote hadi sasa zikiwa hazina uhakika na maisha yao ya ushiriki kwenye ligi kwa msimu ujao.

Related Posts