Saba mbaroni kwa tuhuma ya kuwatesa walevi kwenye mahabusu feki

Kakamega. Watu saba wanaojiita ‘mabwana wa nidhamu’ wametiwa mbaroni kwa kosa la kuwakamata na kuwatesa walevi kinyume cha sheria huko nchini Kenya.

Tukio hilo limetokea katika mtaa wa Mabanda wa Makaburini kaunti ya Kakamega ambapo mbali ya kosa hilo pia washukiwa hao wanakosa la kuendesha mahabusu haramu.

Tukio hili linatokea ikiwa zimepita siku chache tangu Collins Leitich mkazi wa Kaunti ya Uasin Gishu Nchini Kenya, kukamatwa na Polisi kwa kosa la kuanzisha kituo cha polisi na kukiendesha kinyemela bila ya idhini ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).

Leitich alipaka kituo hicho rangi ya polisi ili kionekane ni halali. Ingawa mamlaka za eneo hilo zilishitukia ujanja wake kisha kutoa taarifa polisi Machi 8,2025.

Kwa mujibu wa Tuko ya nchini Kenya washukiwa hao saba wanadaiwa kuwakamata watu tisa waliokuwa wamelewa kisha kuwatesa kisa wamekunywa pombe.

Taarifa zinaeleza walevi hao walifungiwa katika chumba kichafu chenye kuta za udongo, wakalazimishwa kujisaidia haja ndogo kwenye ndoo na masharti waliyopewa ili kuachiwa, ilibidi watoe hongo ya KSh 300, (zaidi ya Sh6,000) la sivyo wavumilie adhabu ya kikatili kwa siku tatu.

Uchunguzi umebaini kuwa kituo hicho kilianzishwa kwa kisingizio cha kuwaadhibu wale wanaokunywa pombe kupita kiasi katika eneo hilo.

Lakini mambo yamekuwa kinyume kwani walevi hao wamekuwa wakipitia mateso makali ya kimwili na kisaikolojia kwa siku tatu kwa ambao hawakuweza kumudu hongo hiyo.

“Walinivuta, nilifungiwa ndani pamoja na watu wengine, na kuchapwa kwa siku tatu. Saa sita usiku mijeledi ilianza, walinipiga sana, mapaja yangu bado yanauma,” amesimulia mmoja ya wafungiwa.

 “Tulipobanwa, tulitumia ndoo bila kujali nani alikuwa akitazama, kwa sababu hatukuwa na chaguo. Jioni walikuwa wakileta ugali na mboga ya sukuma wiki,” mwingine amesimulia.

Wakazi wa eneo hilo wanasema kundi hilo ndilo linaendesha gereza haramu bila woga, na kukamata watu kiholela na kumnyamazisha yeyote aliyewahoji.

Msaidizi wa Chifu wa Mji wa Kakamega, Isaac Ayumba amethibitisha hilo, huku akisema watekelezaji sheria walichukua hatua haraka walipopokea taarifa kuhusu kufungwa kwao kinyume cha sheria.

“Nilienda kwanza kwa mzee wa kijiji cha mtaa huo kuulizia madai hayo. Tulithibitisha kuwepo kwa chumba cha mahabusu na kuhamia ili kuokoa waathirika,” amesema.

Kufuatia operesheni hiyo ya uokoaji, maofisa wa polisi na utawala wa serikali ya kitaifa wamewakamata washukiwa saba akiwemo mzee wa kijiji anayedaiwa kuongoza mahabusu.

Runinga ya Citizen iliripoti kuwa washukiwa walionaswa ni: Emmanuel Nyangweso, Derick Owino, Metrine Olenyo, Brian Obonyo, Johnson Shirava, Koffi Anan na Charles Kisamani. Washukiwa hao sasa wanakabiliwa na mashitaka mengi, ikiwa ni pamoja na kufunga kinyume cha sheria, kushambulia na kutoa vitisho.

Aidha mmoja wao pia amekutwa akiwa na bangi.

Related Posts