Sarafu mtandao bado ni pasua kichwa kwa mifumo ya kibenki

Benki Kuu mbalimbali duniani zimekuwa katika hatua za kutafuta suluhu na mbadala kuhusu matumizi ya sarafu mtandao (Cryptocurrency) katika uchumi. Hali kadhalika kwa Benki Kuu ya Tanzania BOT ambayo pia imekua katika hatua mbalimbali za kutafiti undani wa kadhia hiyo mpya katika mfumo wa fedha ambayo bado ni jambo linalotatiza katika nchi mbalimbali duniani.

Sarafu mtandao ni uvumbuzi mpya katika teknolojia ya fedha ambayo inaruhusu mabadilishano ya kifedha kama kufanya miamala ya kutuma, kupokea, au kuweza kufanya malipo kwa kutumia sarafu dhahania ya kimtandao kwa njia ya kidijitali (cryptos), sarafu hizo zilizo mtandaoni tu zinafanya kazi katika mfumo maalum wa teknolojia inayoitwa (blockchain). Sarafu mtandao maarufu ni Bitcoin, Litecoin, Ethereum na nyinginezo.

Matumizi ya sarafu hizo yanatatiza mifumo ya Benki Kuu, ambacho ndio chombo kilichopewa mamlaka ya udhibiti na usimamizi wa mwenendo wa mfumo wa kifedha katika nchi. Jambo hili linatokana na kuwa mfumo wa uendeshaji wa sarafu hizo una kinzana na misingi muhimu ya mfumo wa kawaida wa uchumi wa fedha unaotumika duniani (Fiat monetary system).

Kwanza, Benki Kuu ndio zimepewa mamlaka ya kutoa fedha (issuance), mfano mamlaka ya kutengeneza, kuchapisha, na kusambaza fedha katika mzunguko wa uchumi. Benki Kuu duniani zinapoteza uwezo wake huu katika mfumo wa sarafu mtandao kwa sababu ni mfumo unaojitegemea (decentralized), ambapo teknolojia ya blockchain yenyewe ndio inayoweza kutengeza sarafu hizo, na ndio inayodhibiti utengezaji wa sarafu za ziada.

Sambamba na hilo, mfumo wa fedha umejengeka katika msingi wa pili kuwa Benki Kuu ndio ina mamlaka ya udhibiti wa ugavi wa fedha, ikiwemo kuongeza au kupunguza kiasi cha fedha kilichopo katika mzunguko wa uchumi (Money supply) kwa kutumia sera mbalimbali za kifedha, Jambo hili linaweza kufanyika muda wowote kulingana na malengo ya kiuchumi na ustawi yanayokusudiwa katika wakati husika.

Katika sarafu mtandao Benki Kuu haitakuwa na uwezo wa kufanya hivyo kwa sababu teknolojia ya blockchain ndio inayoamua kiasi gani cha fedha mtandao cryptos kiwe katika mzunguko, na ndio inayodhibiti usambazaji wa sarafu hizo baina ya watumiaji wake.

Katika hatua nyengine, msingi muhimu wa tatu mfumo wa fedha unaotumika duniani umezipatia Benki Kuu mamlaka ya kuweza kudhibiti viwango vya thamani ya fedha moja dhidi ya nyengine na kiwango cha mfumuko wa bei katika uchumi (exchange rate, inflation rate). Kwa mfano Kupitia hatua mbalimbali za kisera kupunguza mikopo ya kibenki inayoingia katika mzunguko ili kudhibiti kiasi cha fedha kinachoingia katika uchumi na kupunguza kasi ya mfumuko wa bei.

Lakini ikiwa katika sarafu mtandao Benki Kuu haitaweza kufanya hivyo, teknolojia inayoendesha sarafu hizo ndio huamua bei kulingana na nguvu ya soko na ndio itapanga kiwango cha bei ya sarafu hizo, na thamani ya sarafu hiyo dhidi ya fedha za kawaida.

Lakini pia sarafu mtandao zipo katika mfumo ambao inatoa ugumu wa kuweza kuratibiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za usimamizi wa kifedha za nchi husika kama inavyotakiwa katika mfumo wa fedha wa kawaida. Teknolojia ya blockchain inayoratibu sarafu hizo inaficha anuani za watumiaji, pia miamala inaweza kufanyika moja kwa moja baina ya watumiaji bila kuhitaji muhusika wa kati.

Mfumo huo, unapoka mamlaka za Benki Kuu kama msimamizi wa usalama wa mfumo wa fedha kwa kuzuia uwezo wa kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mwenendo wa watumiaji, na pia inatoa mwanya kwa baadhi ya watumiaji wasio nia nzuri kufanya vitendo vya uhujumu uchumi kama utakatishaji fedha na ukwepaji kodi usiokuwa halali.

Hivyo, sarafu za kimtandao ni kama mfumo mwingine wa kifedha unaojitegemea na unakinzana na misingi muhimu ya uendeshaji wa mfumo wa fedha wa kidunia.

Related Posts