Simba kuipeleka robo fainali ya CAF Amaan

SIMBA imepata matumaini ya kuendelea kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry baada ya serikali kubainisha umefanyiwa marekebisho yaliyotakiwa na kulitaka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuukagua tena ili waufungulie, ila imedokezwa kama itashindikana mchezo huo utapelekwa Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitangaza kuufungia uwanja huo, huku Shirikisho la Soka nchini (TFF) likitakiwa kutuma jina la uwanja mbadala utakaotumiwa na Simba katika mchezo huo na Al Masry uliopangwa kuchezwa Aprili 9, ikipewa hadi kesho Ijumaa iwe imeshafahamika uwanja mpya.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson  Msigwa, alisema jana: “Ni kweli leo (jana) wameamka na hiyo taarifa kuwa CAF wameufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sababu za dosari katika eneo la kuchezea. Ukaguzi wa CAF ulifanyika kama wiki mbili zilizopita na ulifanyika baada ya mechi ya Simba na Azam na kumbukeni tulishautangaza kuufunga kupisha ukarabati.

“Lakini hizi mechi zinakuwa na mashabiki wengi na mambo mengi ya kiusalama. TFF ikaomba iutumie uwanja, (CAF) siku wamekuja pale uwanja ulikuwa umekatwa nyasi hadi chini kabisa. Kwa hiyo wachezaji walipokuwa wanacheza na unajua hizi mechi zina presha kidogo ukachimbika chimbika kidogo,” alisema Msigwa aliye pia Msemaji Mkuu wa Serikali.

Aliongeza wakati wa mechi ya Simba na Azam iliyopigwa Februari 24 na kumalizika kwa sare ya 2-2, wakaguzi wa CAF walikuwapo na waliwaeleza wahakikishe wanarekebisha na wakataka kuona mashine za kurekebishia sehemu ya kuchezea (pitch).

Hata hivyo, alisema hawakuweza kuwaonyesha kwa kuwa mashine hizo zilikuwa njiani zinatoka kwa mtengenezaji kutoka China na ziliingia nchini baada ya siku tano tangu walipotaka kuziona na kutumika kufanya ukarabati wa uwanja huo.

“Hata Dabi (Yanga vs Simba) kama ingefanyika (Machi 8, 2025) uwanja uko tayari. Baada ya tangazo lao la asubuhi tumewasiliana na TFF tukawaambia waambieni waje wakague leo (jana) uwanja. Uko tayari.”

Alipotafutwa Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, alisema: “Kama tulivyotoa taarifa ya kufungiwa kwa uwanja hata hilo suala la Simba itatumia uwanja gani litawekwa wazi muda ukifika.”

Awali, Msigwa alisema: “Huwezi kukagua wiki mbili zilizopita halafu unakuja kuufunga uwanja baada ya wiki tatu, leo uwanja uko tayari mashine zimekuja, umeshakarabatiwa na uko tayari.

“Kwa sisi kuendelea kuutumia uwanja wakati unakarabatiwa unatuongezea gharama. Huu uwanja ulitakiwa kukamilika Agosti (2024) yaani hadi leo uwe haujakamilika! Waje kuangalia uwanja umeshakarabatiwa na lile tangazo walitakiwa kutuambia kabla ya kulitoa.”

Katika hatua nyingine, taarifa zinabainisha, baada ya Kwa Mkapa kufungiwa, Simba chaguo lake la kwanza ni kuutumia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja kwa ajili ya mchezo huo huku chaguo la pili ikiwa ni Uwanja wa Amahoro wa Kigali nchini Rwanda.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu mchakato huo wa kutafuta uwanja mwingine, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu alisema:

“Taarifa imetolewa na TFF, lakini sisi Simba hatuna uhalali wa kuzungumzia, wenye mamlaka ni Shirikisho, naweza kusema hivi kumbe si hivyo nikapotosha. Mwenyekiti sijaruhusiwa kuongelea hilo, TFF ndio wana mamlaka ya kuchagua uwanja gani hivyo wao wanajua na wanafahamu, ukiwauliza wanajua kila kitu.”

Related Posts