Unguja. Wakati kukiwa na malalamiko ya kuendesha shughuli, biashara na ujenzi usiofuata taratibu, imebainika baadhi ya taasisi za Serikali kusababisha tatizo hilo na kuibua migongano huku kila upande ukijiangalia badala ya kuangalia masilahi ya umma na Serikali.
Kadhalika, imebainika nyumba za biashara hususani hoteli hazina mikataba ya ukodishwaji wa ardhi jambo ambalo linatajwa kuikosesha mapato Serikali kupitia taasisi zinazohusika.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya.
Dk Sada amesema licha ya Serikali kuhitaji kodi lakini haipaswi kuvunja sheria inazojiwekea yenyewe kwani kuna baadhi ya maeneo hata biashara zinazofanyika ni tofauti na usajili wake.
“Haya maeneo yapo mengi sana hapa Zanzibar, taasisi ama kampuni zinapewa vibali kwa jambo moja lakini zinaendesha jambo lingine huku taasisi za Serikali zinazotoa vibali watendaji wake wakikaa ofisi bila kufuatilia kujua nini kinaendelea,” amesema Dk Saada
Waziri huyo amelazimika kutoa kauli hiyo leo Alhamisi Machi 13, 2025 baada ya kufanya ziara maalumu akiwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na taasisi nyingine za ardhi, usajili wa biashara na kodi kutembelea hoteli kukagua mikataba ya ukodishwaji ardhi na ulipaji kodi, ambapo wamebaini biashara nyingi kutokuwa na mikataba hiyo.
Wakiwa katika ziara hiyo, wamekuta ujenzi ukiendelea katika eneo la Matrekta Mbweni linalomilikiwa na kampuni ya Duma Investment Co Ltd.
Ambapo Dk Saada ameeleza kuwa baada ya ukaguzi wamebaini kuendesha biashara za baa, muziki na kumbi za starehe katika eneo lisiloruhusiwa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar kutokana na kuwa katikati ya makazi ya watu.
Pamoja na kuwa katika eneo ambalo amesema haliruhusiwi kuendesha shughuli hizo, bado wanaendelea na upanuzi wa jengo na kusogolea hifadhi ya barabara wakiwa na kibali kilichotolewa na Kamati ya Usimamizi na Udhibiti Ujenzi (DCU). Alipotafutwa Mwenyekiti wa DCU, Muchi Ameir bila kukataa wala kukubali kama wametoa kibali, amemtaka mwandishi amtumie vibali vya eneo hilo vinavyoonyesha walivitoa wao.
DCU ilianzishwa na Serikali mwaka 2015 kwa ajili ya kusimamia shughuli zote za ujenzi Zanzibar.
DCU inajumuisha wakurugenzi wote wa serikali za mitaa Unguja na Pemba, Mamlaka ya usimamizi mazingira (ZEMA) Mamlaka ya Mji mkongwe (STCDA), Idara ya Mipango miji na Jumuia ya wafanyabiashara (ZNCCIA).
“Hapa biashara hii ipo kimakosa ni katikati ya makazi ya watu hivyo ni kinyume, lakini anaendelea na ujenzi, changamoto iliyopo taasisi za Serikali hatuzungumzi lugha moja kuona kama sheria zinafuatwa,” amesema.
Waziri Saada amesema wamebaini biashara anayofanya na kodi anayolipa haviendani, kwani amesajili biashara moja ila anaendesha nyingi ndani ya eneo moja.
Amesema watachukua hatua stahiki kwa sheria na taratibu ambazo wamejiwekea biashara hiyo haistahili kuwa katika mazingira yale.
“Sisi wenyewe taasisi za Serikali hatuna mfumo mmoja wa kuzungumza kuona kwamba hili ni jambo linapaswa liwepo au lisiwepo na hii sio mara ya kwanza, ukisema na ukaona hakuna anayechukua hatua kwa hiyo kila mmoja anafanya kazi kivyake,” amesema.
“BPRA (Wakala wa Usajili na Biashara wa Mali Zanzibar) na wao hawafuatilii wapo ofisini, ni taasisi nyingi tunahusika na hizi biashara zipo maeneo mengi, tunahitaji kujiangalia, unajiandikisha kwa jambo moja lakini unafanya mambo lukuki na sisi Serikali hatufuatilii, hili halikubalikia,” amesema.
Wakati Dk Saada akisema hivyo, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amekuwa akisisitiza taasisi za Serikali ambazo zinafanya kazi zinazoendana kuwa na mfumo mmoja wa uendeshaji wa shughuli zake, badala ya kila mmoja kufanya kazi kivyake.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa BPRA, Khamis Juma Khamis akizungumza kuhusu usajili wa kampuni ya Duma Investiment Co Ltd amesema waliisajili mwaka 2020 na biashara zote zinazoendeshwa ndani za baa, muziki ziliorodheshwa wakati wa usajili.
“Kwenye mkataba wao vitu walivyovitaja ni miongoni mwa tulivyoona hapa, lakini swali linabakia kuwa sisi tumesajili, sisi tunaposajili huwa tunatazama kuwa eneo lao la biashara ni wapi kwa maana ya na si mara zote sehemu unayotamka kuwa ya usajili ikawa ndio sehemu ya operesheni ya biashara,”
Amesema “zinatofautiana kampuni, wengine wanaweza wakasema wanasajili ofisi yao ikiwa hapa Mbweni lakini shughuli zake za kibiashara akawa anazifanyia Nungwi.
Amesema wamebaini watu wengi wanafanya biashara lakini usajili wao haupo vizuri.
Alichokisema Waziri wa Ardhi
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali amesema wamegundua kuna biashara nyingi zinaendeshwa hazina mikataba ya ardhi.
“Tumegundua wapo wanasajili lakini mikataba haipelekwi Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA),” amesema
Amesema wameandaa kanuni ambayo ina kifungu kimoja cha penati ambayo kama hujasajiliwa na unafanya biashara ukigundulika unalipa asilimia 25 ya mkataba kwa mwaka mzima.
Amesema walikuwa wanashindwa kumkamata mtu au kumchukulia hatua kwa sababu hawakuwa na mamlaka hiyo kwani yapo chini ya BPRA.
Kwa mujibu wa sheria ya umiliki ardhi ya mwaka 1992 lazima uwe na mkataba wa ukodishwaji ardhi (Lease Agreement) ambao unamtaka muhusika alipe kodi ya ardhi na kwa mwaka kutegemea na ukubwa wa eneo la biashara.
Amesema wamebaini kuna kubananga kwa kiasi kikubwa, wapo wanaosajili kampuni lakini hawalipi kodi, wanaolipa kodi ya biashara bila mkataba wa ardhi, “kwa hiyo tunataka kila mmoja alipe kodi kama inavyotakiwa.”
Naye Msimamizi wa biashara hizo, Laurent Charles amesema kila kinachoendeshwa katika eneo hilo kimefuata taratibu zote na wanavibali husika. Hata hivyo amesema bosi wake ndiye anaweza kuzungumzia zaidi kuhusu taratibu hizo ambaye kwa sasa hayupo kisiwani hapo.
Hata hiyo, katika hoteli ya Dhow Palace Mawaziri hao hawakupata nyaraka yoyote kwa kile kilichoelezwa na meneja wa hoteli hiyo, Nawab Abdul kwamba nyaraka zinatunzwa na mmiliki yupo safarini.