Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeeleza mikakati inayochukua kukabiliana na ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa katika vituo vya afya na upimaji wasafiri wanaoingia kwenye visiwa hivyo.
Machi 10,2025 Wizara ya Afya Tanzania Bara ilithibitisha uwapo wa wagonjwa wawili wenye maambukizi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo, jana Machi 13, 2025 Waziri wa Afya, Jenister Mhagama alitoa taarifa kuhusu kumalizika kwa ugonjwa wa Marburg huku akitoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Mpox.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kutokwa na vipele sehemu mbalimbali za mwili, homa kali, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo.
Katika taarifa kwa umma, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui Machi 13, 2025 amesema licha ya kuwa hakuna mgonjwa yeyote ambaye ameripotiwa kisiwani hapo, Serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huo usiingie kisiwani humo.
“Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa katika vituo vya afya, upimaji wa wasafiri wanaoingia na kutoka kupitia maeneo makuu ya nchi uwanja wa ndege na bandarini,” amesema.
Pia, wanaimarisha utoaji wa elimu ya afya na kuhamasisha jamii ili kuwawezesha kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo na magonjwa mengine ya mlipuko.
Pamoja na hatua hizo zinazochukuliwa, wizara inatoa wito na kuwasisitiza wananchi kuchukua na kutekeleza hatua za kujikinga.
Hatua hizo ni pamoja na kuwahi kituo cha afya kwa uchunguzi na matibabu wanapoona dalili za ugonjwa huo au kupiga simu nambari 190 bila malipo.
Pia, waepuke kugusuana kwa kupeana mikono, kubusiana, kukumbatiana au kujamiiana na mtu mwenye dalili hizo.
Pia, wanatakiwa kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za homa ya nyani na kuepuka kumhudumia mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa huo.
Imewakumbusha wafanyakazi wa afya kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa wakati wote wanapohudumia wagonjwa wenye vipele na homa na kunawa mikono mara wa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Wakati huo huo, Serikali imewataka wananchi kujitahadharisha na magonjwa ya mlipuko katika msimu wa mvua, ambazo zimetabiriwa kunyesha kuanzia Machi hadi Mei,2025.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani na chini ya wastani.
Hata hivyo, Waziri Mazrui amesema mvua hizo zinaweza kuleta athari kubwa za kiafya kutokana na kujitokeza kwa magonjwa ya mripuko kama kipindipindu, hivyo kuwataka wananchi kudumisha usafi wa mazingira ili kupunguza hatari ya magonjwa hayo.
Itakumbukwa miaka ya karibuni mvua za masikia zilisababisha athari kubwa za kiafya kwa kujitokeza magonjwa ya kipindipindu na homa za matumbo
“Hii inatokana na maji kutuama na usafi duni wa mazingira katika maeneo yetu,” amesema
Nao baadhi ya wananchi wamesema bado wanahitaji kupata elimu zaidi na kudhibiti ugonjwa huo usiingie katika visiwa hivyo.
“Huu ugonjwa huku kwetu bado haujaingia lakini ni vyema zikaongezwa nguvu katika kudhibiti badala ya kusubiri ushambulie kisha ndio harakati ziwe nyingi,” amesema Thuwaiba Ali Ahmed mkazi wa Malindi Unguja.