Tanzania ilivyojipanga 2G, 3G zikielekea ukomo

Kufutwa kwa teknolojia ya mitandao ya 2G na 3G ni miongoni mwa mwambo yanayozungumzwa sasa na wataalamu wa teknolojia za mawasiliano hususani katika mataifa yaliyoendelea.

Hata hivyo, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania habari hiyo haizungumzwi sana kutokana na utegemezi mkubwa wa teknolojia hiyo, gharama kati ya watoa huduma na watumiaji, pamoja na usambazaji usio sawa wa teknolojia za kisasa hususani vijijini.

Kwa muda mrefu mitandao ya 2G na 3G umekuwa ukitajwa kama uti wa mgongo wa mawasiliano ya simu kwa watu wengi, ikitoa huduma muhimu kama simu za sauti na miamala ya pesa kwa njia ya simu, hivyo watoa huduma wanalazimika kuwekeza katika upanuzi wa mitandao ya kisasa huku wakidumisha na hata kupanua mitandao yao ya zamani ili kuhakikisha kila mtu anapata huduma za mawasiliano.

Baadhi ya mataifa tayari yameweka ukomo wa mwisho wa matumizi ya teknolojia hiyo ya zamani, wapo wanaosema mwisho ni mwaka 2025 na wengine wanasema 2033, kila mtu kulingana na soko lake.

Wengi wanazingatia kustaafisha mitandao yao ya 2G na/au 3G ili kutumia upya masafa yao yaliyopo na kuyachanganya na masafa mengine ili kuboresha huduma za 4G na 5G ili kutoa huduma za kisasa zaidi.

Lakini kwa mataifa ya Afrika bado hayana haraka jambo hilo, makala yaliyochapishwa na Shirikisho la kampuni za simu (GSMA) hivi karibuni yalielezea kuwa kasi hiyo ndogo inatatiza watu kupata huduma za intaneti ya kasi lakini kuna sababu.

Mathalani mpaka sasa mitandao ya 3G bado ndiyo inayotumika zaidi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini 4G inatarajiwa kuupiku ifikapo mwaka 2027. GSMA linakadiria kuwa matumizi ya 3G yatashuka hadi kufikia asilimia 50 mwaka huu, huku matumizi ya 2G yakishuka hadi chini ya asilimia 10.

Matumizi ya 4G yanatarajiwa kuongezeka mara mbili ifikapo 2030 na kufikia karibu nusu ya jumla, hivyo kuipita 3G mwishoni mwa 2027. Ingawa matumizi ya 5G yatakuwa ya polepole yanatarajiwa kushika kasi na kufikia asilimia 17 ifikapo 2030.

Mabadiliko haya yatasababisha ongezeko la matumizi ya data ya simu kwa kila mtumiaji mara nne ifikapo 2028, hata hivyo yote hayo yatategemea uboreshaji wa mitandao unaoendelea na upatikanaji wa vifaa kwa bei nafuu utachochea ongezeko hili.

Nchini Tanzania takwimu za Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti Tanzania hadi Desemba 2024 ilikuwa watu milioni 48 na kati ya hao milioni 47.8 wanatumia internet ya simu ikiongezeka kutoka mwaka 2020 watumiaji wa milioni 26.07.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa wanaotumia mtandao wa 2G kwa simu wapo milioni 22.26 huku wanaotumia 3G na kuendelea wakiwa ni milioni 25.6, wastani wa matumizi ya intaneti kwa mwezi kwa kila mtu ni GB 4.49 na kasi ya kupakia ni Mb10.8 kwa sekunde huku ya kupakua ikiwa ni Mb14.9 kwa sekunde.

Asilimia ya watu waliofikiwa na huduma za 2G hadi Desemba 2024 ilikuwa ni 97.2, 3G asilimia 91, 4G asilimia 88 na 5G asilimia 20 tu huku eneo la nchi lililofikiwa likiwa ni asilimia 75.1 kwa 2G, asilimia 73.8 kwa 3G, asilimia 71 kwa 4G na asilimia 2.5 kwa 5G.

Mkurugenzi wa biashara wa kampuni ya simu inayoongoza kwa wateja wengi nchini (Vodacom) Brigita Shirima anasema kuna namna tatu za kufaidi/kuunganishwa na huduma ya 4G ambazo ni kuwa na kifaa chenye uwezo huo, kuwa na mnara unaotoa huduma ya 4G na kuwa na laini inayoweza kuhimili na wao wanaweka juhudi katika vyote.

“Sisi tumekuwa mstari wa mbele kuongeza uwezo wa minara yetu kutoa huduma ya 4G katika maeneo mbalimbali hili linaenda sambamba na ujenzi wa minara mipya yenye uwezo wa 4G. Katika hili, zaidi ya minara 3500 yenye uwezo wa 4G na 5G,” anasema Shirima Mkurugenzi hiyo wa ambaye kampuni yake inaongoza soko kwa utoaji wa huduma za inteneti kwa asilimia 34.

Anasema mbali na hayo wamekuwa wakihamasisha wateja kuongeza uwezo vifaa na laini zao za simu ili kuweza kutumia huduma hiyo na pindi mtu anapotaka kuhuisha laini yake hupewa bure na zaidi hupewa ofa ya kifurushi.

“Pia tunatoa mikopo ya simu janja zenye uwezo wa 4G huku tukishirikiana na wadau mbalimbali kama wauzaji rasmi wa simu hizo na benki, lengo ni kuwezesha umiliki wa simu janja kwa gharama nafuu kwa Watanzania tunafanya hivyo kupitia programu ya ‘Miliki Simu Lipa Mdogo Mdogo,” anasema.

Shirima anasema kupitia programu hizo zaidi ya wateja wao milioni nane wanatumia simu janja ikidhihirisha matokeo chanya ya mikakati yao mbalimbali ya kuwezesha wateja wa kampuni hiyo kufurahia huduma za kidijitali kupitia simu zao za mkononi.

Kadhalika Shirima anasema Serikali inafanya jitihada kubwa ili kuwezesha mabadiliko ya watanzania kutumia teknologia za 4G akitolea mfano utoaji wa ruzuku ya uwekezaji kwenye minara ya mawasiliano yenye uwezo wa 4G katika maeneo ya vijijini kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF).

Pia anasema Serikali kupitia mkakati wake wa Digital Tanzania inachochea upatikanaji wa huduma za intaneti zenye ubora wa hali ya juu kwa serikali na wananchi ikiwa ni pamoja na kuboresha uwezo wake katika kutoa huduma za umma za kidijitali.

Hata hivyo Shirima anasema kuna haja ya Serikali ifikirie upya kuhusu kodi ya ongezeko la thamani (VAT) inayotozwa kwenye simu janja kama hatua ya kimkakati ya kufanya vifaa hivi muhimu vya kidijitali kuwa nafuu zaidi.

“Kupunguza gharama za simu janja kutaongeza kasi ya upatikanaji na matumizi yake, hasa miongoni mwa Watanzania ambao kwa sasa wengi wao hawawezi kumudu. Hatua hii itachangia kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza ajenda ya kidijitali ya taifa, kuimarisha ujumuishi wa kidijitali, na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” anasema Shirima.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya habari Mohammed Abdulla yeye anasema Serikali ya Tanzania haina mpango wa kusitisha mtandao wa 2G isipokuwa ina mipango na sera thabiti na zote zinazungumzia kuongeza matumizi ya 4G na 5G na uzuri watoa huduma za simu tayari wameanza kuchukua za kuhakikisha wanaongeza matumizi na usambazaji wa teknolojia hiyo ya kisasa.

“Ukiangalia hapa nchini teknolojia ya 2G inatumika zaidi vijijini, maeneo mengi ya mjini hivi sasa inatumeka 4G na 5G. Ukisema uzime 2G na 3G wengi wataondoka kwenye huduma sisi tunaamini teknolojia hiyo itaondoka yenyewe,” anasema Abdulla wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya.

Anasema pamoja na kuwa Serikali imeuza masafa ya 5G na baadhi ya maeneo tayari inapatikana lakini kuna kundi kubwa la watu wanatumia vitochi (simu ambazo zilizo nyingi zinatumia 2G na 3G) ndiyo maana suala la kusitisha matumizi ya teknolojia hizo za zamani haziwezi kuwa sehemu ya sera ya Serikali.

“Itakuwa kama ilivyotokea kwenye televisheni, mwanzoni tulikuwa tunatumia analogi baadaye tukahamia dijitali, watu walikuwa wakihama wenyewe kidogokidogo kuacha kutumia antena na sasa wanatumia ving’amuzi,” anasema.

Anaongeza kuwa matumizi ya 2G na 3G yanaendelea kuwa muhimu kwa kuwa si wananchi wote wana uwezo wa kuwa na vifaa vya 4G na kuendelea na sasa msisitizo wa Serikali ni kuongeza miundombinu ya kisasa na kuhakikisha watu wanapata vifaa vya kisasa.

“Tunaangazia namna ya kuwa na uzalishaji wa ndani, tunataka simu ziunganishwe hapa, tayari tuna kiwanda kimoja jijini Arusha tunataka tuwe navyo hata vinne hilo litapunguza hata bei ya vifaa hivyo. Tunatoa motisha ili kuvutia uwekezaji wa namna hiyo,” anasema na kuongeza kuwa simu za kisasa zenye uwezo wa kati zinaweza kuuzwa kwa hata Sh40,000.

Abdulla anasema watoa huduma za simu wana uwezo wa kuongeza matumizi ya 4G kwa kuwa wanaweza kuwa na vifaa vya kisasa na kwa bei rafiki pamoja na utaratibu wa kulipa kidogokidogo hivyo hata wenye kipato kidogo wataweza kumudu.

Kwa upande wake Mhadhiri wa uhandisi wa mawasiliano wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Khadija Mkocha yeye anasema ili kuwa na ujumuishi katika huduma za intaneti yenye kasi ni lazima watumiaji wa 2G na 3G sasa waone umuhimu wa kuhama kuliko kusalia walipo.

“Teknolojia ya 2G ilitangulia miaka mingi iliyopita lakini mpaka sasa watu wanaitumia, mtu anaona inamtosha, kuna haja ya kuwa na ubunifu huduma au suluhu ya kumfanya kila mtu aone kuwa anahitaji intaneti yenye kasi,” anasema.

Dk Mkocha anasema kwa sasa anaona suala la kuistaafisha teknolojia ya 2G na 3G kwa Tanzania bado ni jambo la siku nyingi zijazo lakini anaamini kuwa kukiwa na ubunifu wa kimapinduzi linaweza kufanyika hata kesho kwani kila mtu atahamia kwenye mtandao wa kasi.

“Lakini kwa mwenendo wa sasa bado sana kwani intaneti ya kasi (4G na zaidi) inatumika zaidi maeneo ya mijini tu kwa kuwa ndiko kuna soko hata ikija 6G na 7G itaendelea kuwa hivyo muhimu ni mtu kuona thamani ya kutoka huko aliko na apate uzoefu a thamani mpya,” anasema Mkocha.

Related Posts