
“Kama wadau wa sekta ya usafiri majini, tunapaswa kushirikiana kwa kuwa suala hili ni mtambuka, hivyo, taasisi za serikali ambazo zina vifaa na wataalamu hatuna budi kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa mafanikio ya kukabiliana na changamoto kama hizi yanategemea mshikamano na ushirikiano wa wadau wote katika bahari na maziwa,” amesema Wakili Mutaki.
Ameongeza kuwa zoezi hilo lina umuhimu mkubwa hasa kwa Mkoa wa Tanga, ambao unazidi kushuhudia ukuaji wa miradi ya kimkakati kama upanuzi wa Bandari ya Tanga na uwekezaji katika bohari za mafuta.
“Serikali inatekeleza miradi mikubwa chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kama upanuzi wa bandari na miundombinu ya mafuta inayojengwa. Hali hii inahitaji maandalizi makini ili kukabiliana na dharura zozote zinazoweza kujitokeza,” amesititiza Wakili Mutaki.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Bw. Clever Mwaikambo, ambaye ni mtaalamu wa uhifadhi wa bahari na maeneo tengefu, amesema kuwa Tanga imechaguliwa kwa sababu ya shughuli nyingi za kiuchumi zinazoendelea, hususan zinazohusiana na sekta ya mafuta.
“Kwa kuzingatia miradi kama ujenzi wa bomba la mafuta la EACOP kutoka Uganda na uwekezaji mwingine unaohusiana na mafuta, kuna uwezekano wa umwagikaji wa mafuta na kuathiri mazingira. Hivyo, ni muhimu kuwa na timu yenye ujuzi wa hali ya juu katika kukabiliana na changamoto hizi,” amesema Bw. Mwaikambo.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za umwagikaji wa mafuta baharini, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa maalum na mbinu za udhibiti wa uharibifu wa mazingira.