Tiba ya figo zilizofeli | Mwananchi

Figo ni kiungo muhimu sana mwilini. Mungu ametupa figo mbili moja kulia na nyingine kushoto, ziko tumboni chini ya mbavu. Figo huanza kazi tangu mtoto akiwa tumboni mwa mama yake.

Kazi ya figo ni kuchuja damu, kuondoa taka mwili, kudhibiti uwiano wa madini na maji mwilini. Figo pia husaidia mchakato wa kutengemeza damu na kuimarisha mifupa. Kazi zake ni muhimu na siku zikishindwa kufanya kazi ndio utaelewa mambo yalivyo.

Katika kazi yangu ya udaktari ninaona wagonjwa wanaoumwa na magonjwa ya figo na pengine kupelekea kufeli kwa figo.

Nitayataja kidogo, mtoto akiwa tumboni mwa mama figo zinaweza kushindwa kufanya kazi na kupelekea mtoto tumboni kufariki.

Watoto wadogo huugua ugonjwa wa figo pia, kama vile nephrotic syndrome ambao ni ugonjwa wa wa chujio za figo kushindwa kazi. Na upo mwingine wa saratani ya figo kwa watoto, ujulikanao kama Wilm’s tumor.

Vijana pia huugua figo pia kama vile polycytic kidney disease. Na watu wazima huugua ugonjwa wa figo kufeli, kidney failure.

Ugonjwa huu unaanza taratibu na unapokomaa ndio dalili zake huonekana. Yaani ukiziona dalili, jua ugonjwa umefika mbali stage 4 au 5.

Ugonjwa huu husababishwa na matumizi ya holela na yasiyodhibitiwa ya dawa hasa za maumivu na antibiotic kama vile Diclofenac, Asprin, Gentamycin, Diclopar na nyingine za aina hizo.

Sababu nyingine ni pamoja na ugonjwa wa kisukari uliokithiri na kutokudhibitiwa, ugonjwa wa kuziba njia ya mkojo kama mawe ya kwenye figo, ureta.

Mwili kutokuwa na maji ya kutosha, husababisha figo kufeli, yaani ni sawa na kuendesha gari bila maji kwenye rejeta, injini hinoki.

Vitu vingine vinavyopelekea magonjwa ya figo ni shinikizo la damu, matumizi ya pombe na kadhalika.

Dalili za ugonjwa huu hazijitokezi haraka maana figo hupambana nazo hadi dakika ya mwisho, ndipo hutoa dalili kama vile kuvimba miguu na uso, kupungua kwa kiasi cha mkojo na pengine kutokukojoa kabisa, upungufu wa damu, kuharisha na pengine kupoteza fahamu au kuharisha na kutapika damu. Dalili ni nyingi na kila mgonjwa anaweza kuwa na dalili zake mahususi.

Hata hivyo, ugonjwa huu hutibika na huzuilika. Tunapoadhimisha siku kama ya leo, Siku ya Figo Duniani, tunatumia fursa hii kuwakumbusha wananchi kuchukua hatua kujikinga na magonjwa ya figo.

Hospitalini figo huchunguzwa kwa kupima kiwango cha mkojo kwa siku, kiwango cha protini kwenye mkojo, uwepo wa chembechembe nyekundu za damu kwenye mkojo, pia hupima kiwango cha urea na createnine kwenye damu.

Vipimo vingine ni pamoja na mwonekano wa figo kwenye ultrasound, kiwango cha kasi ya uchujuaji wa creatine (creatinine clearance ratio) na mwisho ni kwa kuchukua sampuli kwenye figo (kidney biopsy).

Ikithibitika una ugonjwa wa kushindwa kwa figo (kidney failure) matibabu huanzishwa haraka. Matibabu hayo ni pamoja na kuchuja damu kila wiki kwa mashine maalumu (hemodialysis) kwa watoto hufanya peritoneal dialysis.

Kulingana na kiwango cha kufeli na aina yake, uchujaji wa damu unaweza kuwa endelevu pengine mara mbili au tatu kwa wiki kwa kipindi chote cha uhai wa mgonjwa kilichosalia.

Kwa maneno mengine, kushindwa kwa figo kunahitaji mbadala wa figo, yaani Renal Replacement Therapy.

Uchujaji damu kwa mashine ya dialysis ni gharama sana, kwa wiki moja hapa Tanzania humgharimu mgonjwa Sh500, 000 (gharama za moja kwa moja hospitali).

Ili kuchuja damu ni lazima mgonjwa awekewe mpira maalumu wa kuvuta damu inayoenda kuchujwa na mwingine kurudisha damu mwilini iliyokwisha chujwa (central catheter).

Mpira huu huwekwa kwenye mshipa mkubwa shingoni, au chini ya mfupa wa bega(collar bone) au kwenye mshipa mkubwa wa paja.

Hii njia huwa ni ya muda, Mpira huu huuzwa kwa gharama ya Sh250, 000 hadi Sh300, 000. Na hubadilishwa mara kwa mara. Wengine hulazimika kutumia kifaa kiitwacho palmcath ambacho hupandikizwa kwanye mshipa mkubwa na kuchimbiwa ndani ya mwili.

Ndiyo njia ya kudumu ya kuchukua na kurudisha damu mwilini. Wakati wa uchujaji hufanyika upasuaji ya kuungamisha mishipa ya artery na vein ya mikononi maarufu kwa jina la AV fistula. Upasuaji wake ni gharama na pengine husubiri mpaka mshipa upanuke vya kutosha(fistula maturation).

Hii ni njia tu ya kusaidia kuendelea kuishi hapa duniani.

Njia thabiti makini na ya kudumu ya tiba za figo zilizofeli ni kupandikiziwa figo nyingine. Upandikizaji wa figo duniani ulianza miaka ya 1960, hapa nchini Tanzania ulifanyika mwaka 2017.

Njia hii huhitaji mgonjwa kuwa na mtu atakayempatia figo (kidney donor). Wagonjwa waliopandikizwa figo hurejea kwenye hali ya kawaida kama awali na huishi miaka mingi, tofauti na wale wanaosafisha figo kwa uchujaji wa mashine.

Sifa za mchangiaji wa figo ni lazima awe anafanana kwa karibu na anayepokea (matching)

Upandikizaji wa figo hufanywa kwa kutumia figo ya mtu mzima anayeishi (livedonor) au aliyefarik i(cadaveric donor), watafiti wamejaribu kupandikiza figo ya nguruwe na nyani, na wako wanaotumia teknolojia ya 3D printing kudesign machine ndogo ya figo, itakayopandikizwa mwilini kuchuja damu na pia wengine wanajaribu teknolojia za stem cell therapy.

Upandikizwaji wa figo (live kidney transplant) ni operesheni inayofanyika kwa takribani saa nane. Mtoa figo huanza kufanyiwa upasuaji na kwa utaalamu figo yake huchukuliwa. Operesheni ya anayepokea huanza saa mbili baada ya operesheni ya anayetoa figo kuanza.

Mishipa ya damu huunganishwa kwanza na kisha mrija wa mkojo huunganishwa kwenye kibofu cha mgonjwa. Mara baada ya upasuaji huo, wagonjwa wote – aliyetoa na aliyepandikizwa figo huwekwa chini ya uangalizi maalumu (ICU).

Mgonjwa aliyepandikizwa figo huchunguzwa ufanyaji kazi wa figo iliyopandikizwa.

Hapa Hospitali ya Benjanim Mkapa ninapofanya kazi tangu mwaka 2018 hadi sasa, timu ya wataalamu wa upandikizaji figo chini ya uongozi wa Profesa Masumbuko Mwashambwa wamepandikiza wagonjwa 50 figo kwa mafanikio makubwa.

Hospitali zinazofanya upandikizaji wa figo hapa nchini mbali na Hospitali Benjamin Mkapa hapa Dodoma ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Mlongazila. Jiihada zinaendelea kuziwezesha Hospitali za Bugando Mwanza na KCMC Moshi kuanza kutoa huduma hizi.

Ukipandikizwa figo basi mambo yanakuwa yamerejea na mgonjwa anakuwa amepona kabisa.

Tunaendelea kuchagiza jitihada za Serikali, viongozi wa hospitali zetu, wataalamu wetu na wadau wengine wa maendeleo ya tiba za figo ndani na nje ya nchi, ili wagonjwa wetu wapate huduma hizi za upandikizaji wa figo.

Kwa sasa huhitaji kusafiri nje ya Tanzania kupandikiza figo, labda kuwe na sababu binafsi za kufanya hivyo.

Wito wangu ni kwa jamii kuitikia mwito wa kuchangia wengine figo, baada ya Serikali kutunga sera na sheria ya uchagiaji na upandikizaji wa viungo utakaoanzisha Benki ya Viungo nchini (Organ Bank).

Pili, tukeze kwenye tafiti za magonjwa yakiwemo ya figo kwa kujenga maabara za utafiti na uchunguzi wa viungo.

Tatu tutoe elimu ya upandikizaji kwa  wananchi na kusomesha wataalamu zaidi.

Nne tuwezeshe wananchi kumudu gharama za upandikizaji

Mwisho, lakini so kwa umuhimu, tuhakikishe tunadhibiti magonjwa yanayopelekea figo kushindwa kazi kwani kinga ni bora kuliko tiba.

Na wale watakaokufa kwa sababu nyingine yeyote ile, basi wasiende kaburini na viungo vyao kwani wengine wanavihitaji mno hapa duniani.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘gundua ugonjwa mapema na anza tiba mara moja.’

Mwandishi ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya Upasuaji Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma Tanzania na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania.  Kwa maoni na ushauri andika kwa: [email protected]

Related Posts