Na Farida Mangube, Morogoro
Wakulima nchini wametakiwa kuzingatia kilimo hai na endelevu kwa lengo la kulinda afya za watu na mazingira, pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na matumizi ya kilimo kisicho salama.
Kauli hiyo imetolewa na Prof. Samwel Kabote, Rasi wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii na Insia wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakati akifungua warsha ya siku mbili inayofanyika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro, Machi 13 -14, 2025.
Warsha hiyo inalenga kujadili mbinu za kutangaza na kuendeleza kilimo hai kwa wakulima, kwa kushirikiana na vijana kutoka taasisi za elimu na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Kabote alisema SUA, kupitia Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE), itaendelea kufanya tafiti na kutoa elimu ya ugani kwa wakulima ili kuwawezesha kulima kwa tija na kujua jinsi ya kupata masoko ya bidhaa zao.
Aidha, Prof. Kabote alibainisha kuwa changamoto kubwa inayokwamisha maendeleo ya kilimo hai ni ukosefu wa sera madhubuti, lakini wanataaluma wanaendelea kuishawishi serikali kutumia matokeo ya tafiti ili kuimarisha uelewa wa kilimo hicho kwa misingi ya kisera.
Kwa upande wake, Dkt. Adolf Makauki kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambaye ni mwenyekiti wa maandalizi ya warsha hiyo, alisema mwitikio wa wakulima kuelekea kilimo hai bado ni mdogo, lakini kuna matumaini ya ukuaji wake kadri elimu inavyoendelea kutolewa.
“Mimi naona tunarudi kwenye maisha yetu ya zamani, maana kilimo hiki ndicho kilichokuwepo kabla ya matumizi ya kemikali. Tukitangaza zaidi kilimo hai, wakulima wataelewa na kuanza kushiriki kwa wingi, kwani hakuna mtu anayependa kuugua magonjwa kama kisukari,” alisema Dkt. Makauki.
Naye Dkt. Lilian Sechambo, Mhadhiri wa Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani, SUA, alisema kilimo hai ni msingi wa ustawi wa jamii yoyote kwa sababu hakitumii kemikali hatarishi, na hivyo kusaidia kulinda afya na mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Warsha hiyo inatarajia kufanya ziara kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro yanayotekeleza kilimo hai ili kuona changamoto zilizopo na kubuni mikakati ya kuboresha sekta hiyo kwa manufaa ya taifa.