Dar es Salaam. Raia wa Ghana, Valentine Kofi (45) na Watanzania watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kuingilia mfumo wa benki na kuiba Sh2bilioni, mali ya benki ya Banc ABC.
Mbali na Kofi ambaye ni mkazi ya Mikocheni washtakiwa wengine ni Patrick Tarimo(34) mkazi wa Kibaha, Aisha Kagashe(40) mkazi wa Sinza na Idan Msuya(46) mkazi wa Mikocheni.
Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi, Machi 13, 2025 na kusomewa kesi ya Uhujumu uchumi.
Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru aliwasomea mashtaka yao, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Kabla ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa hao kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya Uhujumu Uchumi.
Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Septemba Mosi, 2021 na Oktoba 25, 2021 ndani ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi tisa za Afrika ambazo ni Ghana, Ivory Coast, Uganda, Zambia, Senegal, Cameroon, Ufaransa, Mali na Bukinafaso.
Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishw mahakamani, kuongoza genge hilo kwa kuingilia mfumo wa benki ya African Banking Corporation of Tanzania Limited( Banc ABC).kwa lengo la kuiba Sh2,095,170,000 mali ya benki hiyo.
Shtaka la pili ni kuingilia mfumo wa benki, ambapo washtakiwa hao na wengine ambao hawajafikishwa mahakamani siku na maeneo halo, waliingilia mfumo wa kompyuta wa benki hiyo na kudukua akaunti 160 za visa za malipo ya awali zilizopo katika benki hiyo na kupelekea benki hiyo ya Banc ABC ipate deni la Sh 3,543,555,243.
Shtaka la tatu ni wizi, tukio wanalodaiwa kulitenda Okotoba 24 na Oktoba 25, 2021 katika maeneo hayo, ambapo washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, waliiba Sh2,095,170,000 kupitia kadi ya visa ya malipo ya awali kutoka katika benki hiyo yenye namba ya utambukisho 486054 mali ya benki hiyo.
Shtaka la nne ni kutakatisha fedha, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Oktoba 24, 2021 na Februari 18, 2025 katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi hizo, washtakiwa kwa pamoja na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani hapo, walijipatia Sh2bilioni mali ya benki ya Banc ABC, wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la wizi.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kwamba wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 27, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.