Bukoba. Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefunga shughuli za uvuvi katika Ziwa Ikimba mkoani Kagera kwa kipindi cha miezi sita.
Hatua hiyo inalenga kupisha upandikizaji vifaranga vya samaki tani milioni 1.5 ili kuongeza uzalishaji kutoka tani milioni moja hadi kufikia tani milioni 13 za samaki kwa mwaka.
Ziwa hilo ni miongoni mwa maziwa 15 madogo mkoani Kagera, lililopo Bukoba Vijijini. Lina ukubwa wa kilomita za mraba 38.09 likiwa halina mwambao.
Ziwa hilo linakopatikana samaki aina ya furu, sato, kamongo na kambale, na linakabiliwa na changamoto za uvuvi haramu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji, akizungumza na wananchi, wakiwamo wavuvi jana Machi 12, 2025 kwenye mwalo wa ziwa hilo wa Buterankuzi akiwa ziarani, amesema uamuzi wa kusimamisha shughuli za uvuvi ni kutokana na mfululizo mbaya wa kila mwaka wa uzalishaji wa samaki.
“Tunasimamisha shughuli za uvuvi kutokana na mfululizo mbaya na upatikanaji hafifu wa samaki katika ziwa hili ambao hauwezeshi wananchi na Serikali kupata samaki kwa wingi. Hivyo, tumeamua kuongeza uzalishaji; ndiyo maana leo tumepanda vifaranga tani milioni 1.5 ili kuongeza wingi wa samaki kutoka tani milioni moja hadi tani milioni 13 baada ya miezi sita,” amesema.

Dk Kijaji ameelekeza wataalamu wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba kufanya tathmini kama ndani ya Ziwa Ikimba kunaweza kufanyika ufugaji wa aina hiyo ili wananchi wanufaike zaidi.
Mvuvi katika ziwa hilo, Antony Mussa, amesema upatikanaji wa samaki ni mdogo, hivyo kukosa hata wa kitoweo cha nyumbani.
Ameiomba Serikali, kama imeamua kupandikiza vifaranga vya samaki, iweke ulinzi mkali ili kuzuia uvuvi haramu.
Amesema hilo likifanyika, watakuwa na msimu mzuri baada ya kipindi kilichopangwa, hivyo kujiongezea kipato.
“Nilikuwa sipati samaki wa kutosha. Awali changamoto ya uvuvi haramu wa kutumia nyavu na dawa ulitawala. Ulikuwa unafyeka hadi vifaranga. Tunaiomba Serikali iweke ulinzi vifaranga vilivyopandikizwa viweze kukua tupate samaki wa kutosha,” amesema.
Mkazi wa Kata ya Kaibanja ambaye ni mvuv ziwani hapo, Deodatus Shemo, amesema wamekuwa wakigharimia ununuzi wa vifaa na mitego ya samaki kama nyavu na mitumbwi, lakini kuna wakati anapata Sh10,000 kwa siku na muda mwingine anakosa samaki wa matumizi ya nyumbani.
Diwani wa Kaibanja, Jackson Rwankomezi, amesema kusimamishwa kwa shughuli za uvuvi kupisha upandikizaji vifaranga kutaongeza upatikanaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Bukoba Vijijini.
Amesema uvuvi haramu umesababisha makusanyo ya mapato ya ndani kwa mwaka yanayotokana na samaki kuwa Sh5 milioni kwa mwaka fedha, ambazo ni kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa ziwa.