Ahoua, Kibu wafunika, Simba ikiifyatua Dodoma jiji

TUSIZOEANE. Ni kama onyo kali vile ilichofanya Simba jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji kwa kuweka rekodi ya kibabe huku wakipunguza utofauti wa pointi kati yao na Yanga ambao wanakimbizana nao kwenye vita ya ubingwa.

Simba iliyofikisha pointi 57, moja pungufu na ilizonazo Yanga yenye 58 kileleni zote zikicheza mechi 22 kila moja, na ushindi huo imeifanya iwe timu ya kwanza msimu huu kuibuka na ushindi mkubwa zaidi wa mabao 6-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.

Kwa mara ya kwanza msimu huu, ameshuhudiwa Kibu Denis kwenye mchezo huo akifunga mabao mabao mawili katika dakika ya 55 na 66 na kutoa asisti mbili hivyo ameondoa gundu la kucheza zaidi ya michezo 10 bila ya bao.

Mbali na Kibu, Charles Jean Ahoua naye alikuwa shujaa katika mchezo huo kwa kufunga mabao mawili katika dakika ya 22  na 45+8  kutoa asisti mbili kama ilivyokuwa kwa Kibu.

Mabao mengine ya Simba kwenye mchezo huo yamefungwa na Elie Mpanzu dakika ya 17 na Elie Mpanzu dakika ya 48.

Mabao mawili yaliyofungwa na Charles Jean Ahoua yamemfanya kiungo huyo mshambuliaji kuwazidi kete nyota wa Yanga, Prince Dube na Clement Mzize kwenye vita ya ufungaji bora Ligi Kuu Bara.

Awali Ahoua, Mzize na Dube walikuwa wanalingana kwa mabao kabla ya MVP huyo wa msimu uliopita Ivory Coast kufanya yake dhidi ya walima dhabibu hao.

Kwa mabao hayo, Ahoua ndiye mchezaji mwenye mchango mkubwa zaidi kwenye kiklsi cha Simba mbali na kuwa na mabao 12 anaasisti nane (sita kabla ya jana)  hivyo amehusika katika mabao 20.

Mpango wa kushambulia kwa mipira mirefu huku wakijenga mashambulizi yao kuanzia nyuma haukuonekana kufanya kazi ipasavyo kwa Dodoma Jiji.

Mara nyingi kila ambapo walikuwa.wakijaribu kutoka eneo lao, washambuliaji wa Simba walitengeneza presha kubwa ambayo iliwafanya kufanya makosa.

Hata mipira mirefu ambayo walipanga kuitumia kwa Lusajo ambaye alisimama mwenyewe kwenye eneo la mwisho mabeki wa Simba walifika na kuondosha hatari hizo.

Angalau katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Dodoma ilionekana kuwa nguvu  katika eneo lake la kiungo licha ya kuzidiwa, kipindi cha pili walionekana dhaifu.

Licha ya kuingia dirisha dogo la usajili, Elie Mpanzu ameonyesha kuwa anaweza kuisaidia Simba kurejesha heshima yao iliyopotenda ndani ya misimu mitatu iliyopita.

Mpanzu ambaye alipiga mashuti matatu ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza huku moja likiwa bao, aliwapa wakati mgumu mabeki wa Dodoma Jiji hasa Mhilu ambaye alikuwa akicheza upande wa kulia.

Uwezo wa kuulinda mpira na kuipangua ngome ya Dodoma Jiji ni miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakiipa faida Simba kwenye safu yao ya ushambuliaji huku akisaidiana na Mohammed Hussein na kuna wakati alikuwa akibadilisha nafasi ya Charles Jean Ahoua aliyekuwa akicheza namba 10.

Bao na asisti ambayo Mpanzu ametoa dhidi ya Dodoma Jiji, vimemfanya kuhusika katika mabao sita, amefunga matatu na asisti tatu.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids ni kama ameamua kuwaganyia mechi washambuliaji wake wa kati, Leonel Ateba na Steven Mukwala wote wenye mabao 17 kwa pamoja kwenye ligi kila mmoja akifunga manane na mwingine tisa.

Tangu mchezo dhidi ya Coastal Union ambao ulichezwa Arusha na kushuhudiwa  Mukwala akifunga mabao matatu, Msauzi huyo amemua kutoa nafasi sawa kwa washambuliaji hao, awali Ateba mwenye mabao manane  alionekana kupata nafasi zaidi kwa kuanza katika  michezo mfululizo ikiwemo mitatu ya mwisho  ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kabla ya mchezo wa leo, baada ya Mukwala kufunga hat trick dhidi ya Coastal, Ateba alipewa TMA kwenye raundi ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho na kupachika bao moja kwenye ushindi wa mabao 3-1 ambao wekundu hao wa Msimbazi waliupata.

Katika mchezo wa leo, Fadlu, aliamua kuanza na Mukwala ambaye ndani ya dakika 45 za  kipindi cha kwanza alipiga mashuti mawili ambayo hata hivyo hayakulenga lango kabla ya kufunga bao lake la tisa msimu huu katika ligi  kwa kisigino.

SIMBA: Ally, Duchu, Hussein (C), Chamou,  Hamza, Kagoma,  Kibu, Ngoma, Mukwala, Ahoua  na  Mpanzu.

DODOMA JIJI: Ngeleka,  Augustino,  Apollo,  Hoza,  Milandu,  Mwana,  Mhilu,  Mukrimu,  Lusajo, Obata na  P. Peter.

Related Posts