YUKO wapi Manula? Kuna nini kinaendelea? Ni maswali yanayosumbua kwa sasa vichwani mwa mashabiki wa soka baada ya kipa huyo tegemeo wa timu ya Taifa kutoonekana uwanjani kwa muda mrefu.
Baada ya kuwepo kwa tetesi za kipa Moussa Camara kuumia katika mechi dhidi ya Azam, wengi waliamini ilikuwa nafasi ya Manula kurudi langoni.
Hata hivyo, katika pambano dhidi ya Coastal Union, kipa huyo hakukaa hata benchi. Kikosi cha kwanza alianza Ally Salim, huku benchi akiwamo Hussein Abel.
Juzi kati tena ikicheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TMA Stars, Manula hata benchi hakuwepo na kuzuia hisia upya juu ya mustakabali wa Manula.
Huko mitandaoni baadhi yanauliza, Manula yu wapi? Kutoonekana tangu alipotoka kupona majeraha yake, kumeibua hisia mbaya kwa mabosi wa Msimbazi, WANAMKOMOA!

Kipa huyo aliyejiunga na Simba msimu wa 2017-2018 akitokea Azam, amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa, Ayoub Lakred kutokea FAR Rabat ya Morocco kabla ya kipa huyo kuondoka hivi karibuni.
Ujio wa Camara kutoka AC Horoya ya Guinea msimu huu ukaongeza balaa zaidi kwa kipa huyo mzawa.
Baada ya kuumia kwa Ayoub wakati kikosi hicho kikiwa katika maandalizi ya msimu ‘Pre Season’, wengi walitegemea kumwona Manula akidaka japo imekuwa ni tofauti, kwani Camara ameingia moja kwa moja katika mfumo wa Kocha Fadlu Davids.
Tangu Camara alipojiunga na Simba msimu huu, ameidakia michezo yote ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku akikosa mmoja tu wa Ligi Kuu Bara kati ya 21, akiwa hajaruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15, ‘Clean Sheets’.
Mchezo pekee ambao Camara aliukosa ni wa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union, Machi 1, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Salim, huku Manula akikosekana hata benchi.

Kukosekana kwa nyota huyo ni ishara tosha maisha yake Simba yanaenda ukingoni, kwani mchezo wa mwisho kuonekana Ligi Kuu ni wa kichapo cha mabao 2-1, dhidi ya Tanzania Prisons, Machi 6, 2024.
Hii ikiwa na maana ni mwaka mmoja sasa Manula hajakaa langoni mwa Simba katika Ligi Kuu iliyopo ukingoni.
Hata hivyo, kipa huyo alicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa ya kikosi hicho dhidi Al Hilal ya Sudan iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, siku ya Agosti 31, 2024. Baada ya hapo amekuwa akionekana akipiga tizi tu na wachezaji wenzake, lakini bila kutumika na hakuna taarifa zozote juu ya kutohitajika kwa mchezaji huyo Simba, kwani hata dirisha dogo zilipoenea tetesi anajiandaa kurudi Azam, zilikufa.
Mabosi wa Simba kupitia Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally aliwahi kunukuliwa mara baada ya kusahulika kwa Manula katika utambulisho wa wachezaji siku ya tamasha la Simba Day, kipa huyo ni mali yao na kilichotokea ni bahati mbaya tu.
Hata hivyo, kipa huyo hajaonekana Ligi Kuu na hata katika mechi za Kombe la Shirikisho na kwa zile za Kombe la Shirikisho Afrika mara ya mwisho alionekana benchi Simba dhidi ya Constantine ya Algeria, Januari 19, mwaka huu.

Ingawa haiwekwi wazi, lakini zipo taarifa zisizo rasmi zinaeleza misimamo mikali aliyokuwa nayo kipa huyo, iliwahi kuwachefua mabosi wa klabu na kwa sasa picha haziendi kwa pande hizo mbili, ila kinachofanya waendelee kuwa pamoja ni mkataba uliopo.
Inaelezwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku mwenyewe akiwa amekubali yaishe ilimradi mkataba umalizike aondoke salama Msimbazi bila tatizo, ikidaiwa kutoaminika kwake kulianzia katika Dabi ya Novemba 5, 2023 na Yanga ilishinda 5-1.
Licha ya aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba na aliyewahi kuwa kaimu kocha wa timu hiyo, Dani Cadena kufichua, Manula alilazimishwa kuchezeshwa akiwa hajapona sawasawa, lakini dhahama ilimuangukia na balaa lilizidi aliporuhusu mabao mawili walipolala 2-1 mbele ya Tanzania Prisons.
Hata hivyo, sio Simba wala menejimenti ya Manula imewahi kuweka wazi sintofahamu inayoendelea baina yao, zaidi ya kipa huyo kutoonekana uwanjani na kuzua maswali mengi, juu ya kipi kimempata, je anakomolewa na mabosi wake ama kitu gani kilichopo nyuma ya kutoonekana kwake uwanjani.
Hoja ni hata kama Camara ana ubora kuliko Manula, ni vipi sasa Camara akiwa majeruhi, Manula asianzishwe kikosini na badala yake kipa namba tatu na nne ndio wanaotumika katika mechi za hivi karibuni?

Kabla ya kutoweka uwanjani, Manula alionyesha uwezo mkubwa hadi kuitwa ‘Tanzania One’ na sio bahati mbaya kwani tangu ajiunge na Simba ametwaa mataji mengi yakiwemo ya Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Manula alijiunga na Simba mwaka 2017 akitokea Azam aliyoitumikia kuanzia mwaka 2012, alipojiunga nayo akitokea Mkamba Rangers na alionyesha kiwango bora kilichompa zaidi umaarufu na kuwavutia mabosi wa Msimbazi waliomsajili.
Msimu wa mwisho akiwa na Azam, aliingia katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za mchezaji bora msimu wa 2016-2017, kipindi hicho ikiitwa VPL kabla ya Vodacom kujitoa kwenye udhamini, akidaka michezo 28, kati ya 30, sawa na dakika 2520.
Katika michezo hiyo 28, Manula aliiongoza Azam kutoruhusu nyavu zake kuguswa mechi 15, huku akiruhusu 13, ikiwa pia ni rekodi nzuri msimu huo, kwani hakuna kipa yeyote aliyefanya hivyo, akiendelea kuonyesha kiwango kizuri langoni mwake.
Msimu wa 2015-2016, Manula alitwaa tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Bara, kipindi hicho ikiitwa VPL, kabla haijaitwa TPL na aliwania na kipa mwenzake, Beno Kakolanya anayeichezea Namungo kwa sasa, japo alikuwa Tanzania Prisons.
Msimu wa 2016-2017, alitwaa tuzo ya Ligi Kuu na kuendeleza rekodi akiwa na Simba msimu wa kwanza tu wa 2017-2018, akimbwaga tena Beno Kakolanya aliyekuwa anaichezea Yanga wakati huo, baada ya kukosa michezo miwili tu msimu huo.
Mataji mengine aliyochukua na Simba mbali na Ligi Kuu ni Kombe la FA mara mbili msimu wa 2019-2020 na 2020-2021, Kombe la Mapinduzi 2022, la Muungano 2024, huku akiifikisha pia robo fainali sita za michuano ya CAF kati ya saba tangu mwaka 2018.
Kwa upande wa Camara, kabla ya kujiunga na Simba alichukua tuzo ya kipa bora mara mbili katika Ligi Kuu ya Guinea akiwa na kikosi cha Horoya, huku akikiwezesha pia kutwaa mataji manne ya Ligi, FA akichukua mara tatu na Super Cup mara mbili.
Hivi karibuni, Manula aliitwa katika timu ya taifa, Taifa Stars na kuwa mmoja ya walioisaidia kufuzu fainali za Afcon 2025 wakati Stars ikiifunga Guinea kwa bao 1-0 Novemba mwaka jana licha ya kwamba hakuwa anatumika Simba.
Pia amekuwa akitumika kama kipa namba moja katika mechi zilizoivusha Stars kwenda fainali za CHAN 2025 na hata mechi za kuwania fainali za Kombe la Dunia za 2026, kuonyesha kuwa bado ni tegemeo la taifa.
Hilo la kuwa na nafasi katika kikosi cha Stars, lakini hapewi nafasi ndani ya Simba, limeibua sintofahamu kwa mashabiki waliotaka kuona safari hii kikosi kitakachokabiliana na Morocco Machi 26 katika mechi ya kuwania fainali za Kombe la Dunia, ataitwa au atapotezewa?

PAWASA, KIBADENI WATIA NENO
Nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kinachohitajika kwa Manula ni kuendelea kuonyesha ukomavu wa kiakili na kimwili.
“Moja ya nafasi ngumu kwa kocha kuibadilisha ni ya kipa kwa sababu mwenzako akicheza na kuonyesha uwezo mkubwa ni ngumu tena kuingia moja kwa moja hasa ukiwa umetokea majeruhi, anachopaswa kukifanya ni kujituma mazoezini ili apangwe tena.”
Pawasa alisema mbali na kipa huyo kutakiwa kujituma ila anahitajika pia msaada wa kisaikolojia ili kumjengea morali ya kuamini bado nafasi ya kucheza anayo, licha ya ushindani wa Camara ambaye amekuwa chaguo la kwanza kikosini kwa sasa.
“Kipa anaweza kucheza kwa muda mrefu kuliko mchezaji yeyote na ndiye anayeusoma mchezo, Juma Kaseja amecheza kwa kipindi kirefu sana kwa sababu sio eneo ambalo benchi la ufundi linabadilisha mara kwa mara, labda itokea changamoto nyingine.”
Kwa upande wa kocha na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Abdallah ‘King’ Kibadeni, alisema Manula ni kipa tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, hivyo kutocheza kwake sio ishara nzuri hasa wakati tunajiandaa na michuano ya AFCON.
“Mimi nafikiria kama kuna misuguano iliyopo baina yake na uongozi wakae chini wayamalize, sioni afya kwa kinachoendelea kwani tumemshuhudia hivi karibuni akiichezea timu ya taifa, ila katika klabu hata benchi hayupo jambo ambalo silielewi.”
Hivi karibuni akiwa na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa inasaka tiketi ya kushiriki michuano ya kufuzu fainali za CHAN, Manula alinukuliwa akiweka wazi ataendeleza kupambana na suala la yeye kucheza hilo litabaki kwa benchi la ufundi.
“Ni kweli usipopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kuna muda unapoteza hali ya kujiamini, lakini niseme wazi nitapambana mazoezini kwa ajili ya timu kiujumla, ushindani ni mkubwa ila nitaonyesha uwezo kadri iwezekanavyo,” alinukuliwa Manula.
“Swala la kucheza ni swala la nafasi ikifika muda utapewa nafasi ya kucheza uoneshe ulichonacho, nimepata nafasi wameona japo kwa sababu sijacheza muda mrefu siwezi kuwa yule kama mwanzo kwa vile kuna vitu ambavyo unapoteza ukiwa unakosa nafasi ya kucheza mechi,” aliongeza Aishi Manula alipohojiwa mara baada ya mechi mojawapo ya kimataifa iliyoidakia Stars mwishoni mwa mwaka jana.