Arusha. Mahakama ya Rufani iliyoketi Iringa, imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa, aliyokuwa amehukumiwa Marko Kivamba, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua baba yake mzazi, Matei Kivamba na mama yake wa kambo, Rozarina Nyingo.
Tukio hilo lilitokea Machi 1, 2017 katika Kijiji cha Igomtwa wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa.
Miongoni mwa ushahidi uliomtia hatiani ni pamoja na kukiri kumuua baba yake na mama yake wa kambo kwa kuwakata na panga kutokana na mgogoro wa ardhi, kwa madai kuwa baba yake alimzuia kulima shamba lake kutokana na ushauri mbaya alioutoa mama yake wa kambo.
Hukumu hiyo imetolewa Machi 13, 2025 na jopo la Majaji watatu ambao ni Rehema Kerefu, Leila Mgonya na Lameck Mlacha na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.
Rufaa hiyo namba 18 ya mwaka 2022 inatokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Iringa Novemba 29, 2021.
Jaji Kerefu amesema baada ya kutafakari kwa makini sababu za kukata rufaa, mawasilisho yaliyotolewa na mawakili wa pande zote mbili na kuchunguza rekodi ya rufaa iliyo mbele yao, wanaona upande wa mashitaka ulithibitisha kesi yake bila kuacha shaka yoyote.
Amesema kwa kuwa hiyo ni rufaa ya kwanza wana wajibu wa kutathimini upya ushahidi wote ulio kwenye kumbukumbu kwa kuusoma pamoja na kuufanyia uchunguzi wa kina ili kufikia hitimisho.
Jaji Kerefu amesema katika rufaa hiyo hakuna shaka kuwa kesi ya upande wa mashitaka iliegemea zaidi ushahidi wa kimazingira, kwani hakukuwa na mtu aliyeshuhudia mrufani akitenda kosa hilo.
Amesema kuwa ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu unaonyesha jaji alimtia hatiani mrufani kwa sababu ya maungamo aliyotoa mbele ya shahidi wa tano na sita, aina ya silaha iliyotumika, kiasi cha nguvu alichotumia kuwadhuru marehemu pamoja na mwenendo wake baada ya tukio.
Nyingine ni maungamo yake mwenyewe ambapo alisimulia kwa uwazi jinsi alivyowaua wazazi wake hao, wanaona inafaa kutoa tena sehemu husika katika taarifa yake ya ziada ya mahakama inayopatikana katika ukurasa wa 135 wa rekodi ya rufaa.
“…Niliondoka kwenda nyumbani kwa mama mzazi ilikuwa saa tano usiku nikakaa kwenye nyumba nyingine. Nikachukua tochi, nilimaliza kula na kunywa ulanzi kidogo, nikabadilisha mavazi, nikachukua panga na kisu, nikaondoka bila kuaga. Nilifika kwa mama mdogo (Rozarina) nikaingia na kukuta mlango haujafungwa walikuwa wanaota moto,”imesema sehemu ya ungamo hilo
“Niliingia bila kuwasha tochi nikaingia na kuona mtu akiwa amelala nikaingia chumbani na kuwasha tochi na kumulika na kumwona baba akiwa amelala. Nilianza kumkatakata shingoni na kichwani, nilipotoka nikasikia mtu anapiga kelele nikamfuata na kumpiga panga la kichwa, usoni huku akilalamika kuwa niwasamehe.
“ Ndipo nikamwambia wewe ndiye uliyesababisha yote haya. Nilipohakikisha nimemmaliza, niliosha panga na kurudi kwa baba na kumwona naye tayari, nikaona katoto kadogo kamezubaa ndipo nikaondoka zangu na kwenda kutoa taarifa kwa mama yangu kuwa nimewaua wote wawili yaani baba na mama mdogo. Nilimweleza afunge mlango…Ndipo nikiwa Kijiji kingine nikaja kukamatwa (Ugesa) na ilikuwa usiku…” imeongeza.
Jaji Kerefu amesema masuala yote hayo yanatoa ushahidi mwingi wa ushiriki wa mrufani katika kutenda kosa hilo, huku akinukuu kesi mbalimbali na kueleza ni maoni yao kuwa yaliyomo katika maelezo ya mrufani ni ushahidi bora zaidi, unaeleza juu ya kile kilichotokea katika usiku wa tukio.
Amesema katika hali hiyo wameridhika Jaji wa Mahakama Kuu alizingatia vya kutosha utetezi wa mrufani hivyo kutupilia mbali sababu hiyo ya rufaa.
Jaji Kerefu amesema kwa kuangalia jumla ushahidi huo hawana shaka kwamba kesi ya upande wa mashitaka dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka yoyote, hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosa mashiko.
Katika kesi ya msingi, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi saba na vielelezo vinne ikiwemo maelezo ya ungamo ya mrufani.
Ilielezwa kuwa siku ya tukio kati ya saa tano hadi saa nane usiku, Matei akiwa na mke wake mdogo (Rozarina) walikuwa wamelala kwenye nyumba yao, ghafla kukasikika kelele zilipigwa na Rozarina akiomba msaada na kusema ‘Marko Kivamba unaniua.
Watoto wa mke mdogo huyo waliokuwa nyumba ya jirani walitoka nje kwenda nyumbani kwa wazazi wao, ambapo walikuta baba yao amekatwa na kitu chenye ncha kali na kwenda kutoa taarifa kwa balozi wa nyumba 10, Zawadi Nyigo (shahidi wa kwanza).
Zawadi alisema siku ya tuko alifuatwa na watoto wa marehemu waliomjulisha kuwa wazazi wao wameuawa na kutoa taarifa kwa kamati ya usalama ya kijiji, ambao waliongozana hadi kwenye nyumba hiyo.
Alisema kuwa walipofika walikuta mwili wa Matei ukiwa juu ya kitanda ukivuja damu akiwa na majeraha kichwani, sehemu nyingine za mwili huku mwili wa Rozarina ukikutwa kwenye shamba la nyumba hiyo akiwa na majeraha kichwani, mikononi na miguuni.
Alieleza watoto wa marehemu waliwajulisha kuwa wazazi wao wameuawa na mrufani ambaye alikamatwa katika Kijiji cha Ugesa, kilomita sita kutoka kijiji tukio lilipotokea.
Akihojiwa na shahidi wa tano, Marko alikiri kuwaua marehemu kwa kuwakata na panga kutokana na mgogoro wa ardhi, kisha akapelekwa Kituo cha Polisi Mafinga.
Uchunguzi wa miili ya marehemu ulionyesha chanzo cha vifo hivyo ni mshtuko uliosababishwa na majeraha makubwa ya kukatwa kichwani na kusababisha damu nyingi kutoka.
Shahidi wa tatu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mafinga Mjini, Felista Kessy, alieleza Mahakama kuwa mrufani alikiri kuwaua wazazi hao kutokana na mgogoro wa ardhi baina yao.
Katika utetezi wake, mrufani alijitenga na tuhuma zinazotolewa dhidi yake na kudai kuwa alikamatwa Februari 28, 2017 na kuwa mgambo waliomkamata saa tano usiku wakimjulisha sheria za kijiji haziruhusu watu kutembea usiku.
Alidai asubuhi ya siku iliyofuata alipelekwa Kijiji cha Igomtwa na kuwaambia hajui lolote kuhusu mauaji hayo.
Katika rufaa hiyo, mrufani huyo alikuwa na sababu sita ikiwemo ushahidi wa shahidi wa saba haukuwa wa kuaminika kwani hakushuhudia akitenda kosa hilo, Jaji alikosea kumtia hatiani kulingana na ushahidi wa shahidi wa kwanza, nyingine ni ushahidi wake wa utetezi haukuzingatiwa.
Wakili Cosmas Kishamawe, akimwakilisha mrufani huyo aliieleza mahakama kuwa wanaachana na sababu nyingine na kubaki na ya mwisho (ushahidi wa utetezi wa mrufani kutozingatiwa).
Ili kuhalalisha hoja yake hiyo, aliielekeza Mahakama kwenye ukurasa wa 103 na 104 wa kumbukumbu ya rufaa hiyo na kusema kuwa, katika utetezi wake, pamoja na mambo mengine, mrufani alieleza kuwa alikamatwa kwa sababu ya kutembea usiku wakati akienda kumsaidia rafiki yake shambani.
Wakili huyo alidai mrufani huyo alieleza mahakama kuwa hajui lolote kuhusu tukio hilo la mauaji ila shahidi huo ulipuuzwa. Jaji angeuzingatia utetezi wa mteja wake, angefikia uamuzi tofauti.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Magreth Mahundi, aliieleza Mahakama kuwa hoja hiyo ya utetezi kutozingatiwa haiungwi mkono na kumbukumbu kwani katika ukurasa wa 209 wa kumbukumbu za rufaa Jaji aliyesikiliza alizingatia vya kutosha utetezi wa mrufani.
Wakili huyo aliieleza mahakama kuwa Jaji aliukataa utetezi huo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kudhoofisha kesi ya mashitaka kwani ilikuwa ni kukana tu.
Wakili huyo aliielekeza Mahakama ukurasa wa 30 wa rekodi ya rufaa ambapo wakati wa usikilizwaji wa awali mrufani alikiri yeye ni mtoto wa Kivamba na Rosarina ni mama yake wa kambo.
“Lakini wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ukurasa wa 103 hadi 104 alieleza kuwa waliofariki walikuwa ni ndugu zao tu na alikuwa hajui chochote. Naisihi mahakama ione rufaa ya mrufani kuwa haifai na muitupilie mbali kabisa,”alisema wakili huyo