Balozi aeleza kilichowakuta Othman, Lissu Angola

Dar es Salaam. Wakati ACT-Wazalendo ikihoji ukimya wa Serikali kuhusu viongozi wake wakuu kuzuiliwa kuingia nchini Angola, Balozi wa Tanzania nchini Angola, Luteni Jenerali Mathew Mkingule ameeleza kilichotokea.

Jana Machi 13, 2025 Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu walizuiwa kuingia nchini Angola katika Uwanja wa Ndege wa Luanda walipokwenda kushiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD).

Kwenye msafara wake Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliambatana Waziri kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Nasra Nassor Omar na maofisa wengine wa chama hicho, ambao wamerejea nchini usiku wa kuamkia leo Ijumaa Machi 13,2025.

Leo kupitia taarifa ya umma iliyotolewa na Katibu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa ACT Wazalendo, Mwanaisha Mndeme imeeleza kusikitishwa na ukimya wa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

“Ni jambo linaloshangaza na kusikitisha kwa Serikali ya Tanzania kushindwa kutoa kauli yoyote dhidi ya kitendo hiki kinachokiuka taratibu za kidiplomasia, ari ya mshikamano wa Afrika na undugu wa kihistoria baina ya Tanzania na Angola.

“Tunaitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itoke hadharani na kufafanua kilichotokea Angola na msimamo wa Serikali juu ya hilo ikizingatiwa miongoni mwa viongozi waandamizi waliokumbwa na kadhia hiyo yumo pia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,” amesema Mndeme.

Wakati taarifa ya ACT Wazalendo ikieleza hayo, Balozi Mkingule amelieleza Mwananchi kuhusu kinachoendelea sasa baada ya viongozi hao kuzuiwa, bila kutaja hasa sababu ya hatua hizo.

Amesema baadhi viongozi kutoka Tanzania waliruhusiwa jana jioni, Alhamisi Machi 13, 2025 kutoka Uwanja wa Ndege wa Luanda na kupewa hoteli yenye hadhi ya nyota tano kwa kila kiongozi, kwa gharama ya Serikali ya Angola.

“Wanategemewa leo kuondoka kurejea Tanzania,” amesema Balozi Mkingule.

Alipoulizwa sababu za viongozi hao kuzuiwa, Balozi Mkingule amejibu kwa ufupi: “Mimi sijui, kwa sababu mimi nipo kama balozi, nitazungumza baadaye.

“Sasa hivi ninatayarisha usafiri wa mheshimiwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar (Othman) kurudi Tanzania.

Hadi sasa Serikali ya Angola hazijazungumzia suala hilo.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar imetoa taarifa kwa umma ikilaani kitendo cha kuzuiwa kwa Othman kwa takriban saa nane katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro wa Luanda, huku naye akichapisha taarifa kuhusu suala hilo kwenye ukurasa wake wa X.

“Mimi pamoja na viongozi wengine mashuhuri wakiwemo marais wastaafu kutoka Botswana na Colombia, Waziri Mkuu mstaafu wa Lesotho na baadhi ya wakuu wa vyama vya siasa kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika tulizuiwa.

“Saa nne usiku tuliachiliwa huru na kupelekwa katika hoteli tulizopangiwa huku tukiwa na uchovu,” amesema Othman katika taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Othman wakati hayo yanakitokea, alikuwa ameambatana na Balozi Mkingule, anayewakilisha Tanzania nchini Angola.

“Kitendo hiki cha aibu kidiplomasia kilichotekelezwa na mamlaka za Angola, hakikuwa na sababu hata kidogo, na kimetia doa dhana ya Umoja wa Afrika, tena katika wakati ambao Rais wa Angola ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

“Hiki ni kitendo kinachopaswa kulaaniwa vikali na Waafrika wote na watu wengine duniani, wanaothamini na kutukuza misingi ya udugu iliyowekwa na viongozi waasisi waliopigania Uhuru wa Bara hili,” amesema Othman.

Hata hivyo, Othman amesema pamoja na kukerwa na kuchukizwa na waliyotendwa, hana kinyongo na raia wema wa Taifa la Angola, ambao Tanzania imekuwa nao na uhusiano mwema na madhubuti wa kihistoria kwa muda mrefu.

“Baada ya kuzingatia tukio la jana, nimeamua kutoshiriki katika mkutano muhimu nilioalikwa, wa Jukwaa la Demokrasia Afrika, na badala yake ninarejea Tanzania.

“Nahitaji muda wa kufanya tafakuri ya kina na kutathmini kile kilichotendwa dhidi yetu, ambacho kilikuwa ni shambulio dhidi ya diplomasia na demokrasia ndani ya Afrika,” amesema Othman.

Related Posts