Che Malone ashtua Simba | Mwanaspoti

SIMBA inashuka uwanjani leo kumalizana na Dodoma Jiji katika mchezo wa kiporo cha Ligi Kuu Bara, lakini ndani ya kambi ya Wekundu wa Msimbazi, kuna taarifa inayoshtua juu ya beki wa kati Che Malone Fondoh.

Beki huyo aliyeumia katika mchezo dhidi ya Azam FC uliopigwa Februari 26 na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 huku akitumika kwa dakika 20 za kwanza, tangu hapo hajaonekana uwanjani.

Taarifa za ndani kutoka Simba ni kwamba mabosi wa wekundu hao wameshtuliwa kwamba kuna uwezekano mkubwa Che Malone kwa msimu huu safari yake ya kucheza imeisha mapema kutokana na majeraha aliyonayo.

Ingawa jopo la madaktari wakubwa wanapambana kulinusuru hilo, lakini tayari benchi la ufundi na hata viongozi wa juu wameshajulishwa kwamba wajiandae kisaikolojia kwani lolote linaweza kutokea.

Inaelezwa kwamba madaktari wameshauri kuwa, beki huyo afanyiwe matibabu ya taratibu kwa kuwa ameumia sehemu ngumu ya goti lake ambapo kama yatafanyika makosa inaweza kumsumbua baadaye.

“Che Malone ameumia sana. Awali, ilionekana kama tatizo dogo, lakini hali sio nzuri sana Kuna uwezekano mkubwa tukamkosa zaidi na hata msimu akawa ameumalizia hapa,” alisema bosi huyo wa juu wa Simba na kuongeza;

“Tumeshauriwa tusiharakishe tukaja kumpa shida zaidi kwahiyo hapa tunaumiza vichwa namna gani tutamalizia msimu bila yeye.”

Awali, kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids alinukuliwa mara baada ya pambano lililopigwa jijini Arusha ambapo Simba ilishinda mabao 3-0 likiwa pambano la kwanza kwa Che Malone kukosekana sambamba na kipa, Moussa Camara alisema alitarajiwa kutumika katika Dabi ya Kariakoo.

Hata hivyo, dabi hiyo iliahirishwa na juzi Simba ilicheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TMA Stars na kushinda 3-0, wawili hao hawakucheza kuthibitisha kuwa hali zao hazipo vizuri na jana kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola alikiri hawatatumika dhidi ya Dodoma Jiji.

Kinachoiumiza kichwa Simba ni namna ya kucheza mecji zao za robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri na michezo mingine iliyosalia katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) ikiwa miongoni mwa zilizotinga 16 Bora na itavaana na Bigman ya Championship.

Awali, taarifa kutoka kwa kocha Fadlu zilisema Che Malone alikuwa ametafutiwa daktari maalumu ili kumsaidia apone haraka, lakini kwa hali ilivyo ni kwamba benchi linajiandaa kuendelea na mechi zao bila beki hiyo Mcameroon aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka CotonSport ya Cameroon.

Tangu Che Malone aumie Simba imekuwa ikimtumia na Abdulrazak Hamza na Karaboue.

Related Posts