Chuo Cha Furahika Chatoa Fursa Kwa Vijana Kujifunza Ujuzi wa Kitaalamu Bila Malipo

Mkuu wa Chuo cha Furahika, Dkt. David Msuya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 14, 2025 kuhusiana na kuwakaribisha wanafunzi wapya katika chuo hicho.

CHUO cha Ufundi Furahika kimetangaza nafasi za masomo bure kwa vijana kwa mwaka wa masomo 2025/26, kikiwa na lengo la kuwajengea ujuzi wa kujitegemea na kuboresha maisha yao ya baadaye. Fursa hii inawapa vijana waliomaliza Darasa la Saba na Kidato cha Nne njia mbadala ya kujikwamua kiuchumi kupitia elimu ya ufundi stadi.

Mkuu wa Chuo hicho , Dkt. David Msuya, amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutoa elimu jumuishi na yenye tija kwa jamii. 

Ameeleza kuwa wanafunzi watajifunza bure, huku wakihitajika kulipia tu gharama ya mitihani na vifaa vya kujifunzia kwa kiasi cha shilingi 50,000.

“Elimu ya ufundi ni njia ya uhakika kwa vijana kupata ajira au kujiajiri. Tunaendelea kupokea wanafunzi, na wale waliopo mikoani wanaweza kujisajili kupitia tovuti yetu,” amesema Dkt. Msuya.

Chuo hicho, kilichopo Buguruni Malapa, Dar es Salaam, kinatoa kozi mbalimbali kama Ualimu wa Awali, Uhazili, Huduma za Usafirishaji wa Abiria, Programu za Kompyuta, Utawala wa Biashara, pamoja na Uhasibu na Fedha. Masomo haya yanawawezesha wahitimu kupata ujuzi wa kitaalamu unaohitajika sokoni, hivyo kupunguza tatizo la ajira na kuongeza fursa za maendeleo kwa vijana.

Wazazi pia wamehimizwa kuchangamkia fursa hii kwa kuwapeleka watoto wao kujiunga na masomo. Bi Madaraka Omary, mmoja wa wazazi waliounga mkono mpango huo, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha sekta ya elimu na kusaidia vijana kupata maarifa bila vikwazo vya kifedha.

Kwa mujibu wa uongozi wa chuo, bado kuna nafasi za usajili kwa wanafunzi wapya, na mafunzo haya yanatoa msingi mzuri kwa maendeleo ya kitaaluma na kijamii kwa vijana wa Tanzania.

Related Posts