GOODNESS GRAYSON ATOA SHUKRANI UONGOZI HOSPITALI YA WILAYA YA SAME KWA HUDUMA BORA

Na Ashrack Miraji Michuzi Tv  

Goodness Grayson Ketto ameonesha shukrani zake kwa huduma bora alizozipata wakati alipojifungua mtoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Same.

Katika mahojiano maalum na mwandishi wetu, Grayson alielezea jinsi huduma za afya kutoka kwa wauguzi na madaktari zilivyokuwa muhimu kwa usalama wake na wa mtoto wake. Alisema kuwa hospitali hiyo imetoa huduma bora na ilimsaidia kumtunza yeye na mtoto wake katika hali ngumu.

“Nilikuwa na wasiwasi mwingi kwa sababu mtoto wangu alikuwa njiti, lakini wauguzi walikuwa makini sana. Hali yangu imeimarika, na mtoto wangu sasa anaendelea vizuri,” alisema Goodness kwa furaha.

Alitoa pia shukrani kwa uongozi wa hospitali chini ya Mganga Mkuu, Dkt. Alexander, kwa kuhakikisha rasilimali muhimu zilikuwepo wakati wa kujifungua kwake na kumsaidia kupokea huduma bora.

“Shukrani nyingi kwa uongozi wa hospitali hii, walifanya kila iwezekanavyo ili tuwe na afya bora,” aliongeza.

Pia, Goodness alielezea shukrani zake kwa serikali kwa kuimarisha huduma za afya katika hospitali za serikali na kuhakikisha mama na watoto wanapata matibabu bora, hususan kwa wanaozaliwa katika hali ngumu kama ya mtoto njiti.

“Bila msaada wa serikali na hospitali hii, hali yangu ingekuwa ngumu zaidi. Shukrani nyingi kwa wote waliohusika,” alisema Goodness na kuongeza kuwa mtoto wake sasa ana umri wa miezi saba na ameendelea kuwa na afya njema.

Goodness alitoa wito kwa wazazi wenzake kuacha kukimbilia hospitali za gharama kubwa, akisisitiza kuwa hospitali za serikali zimeboreshwa sana na zinatoa huduma bora kuliko hospitali binafsi.

“Hospitali ya Wilaya ya Same imeboreshwa sana, huduma zao ni bora ukilinganisha na miaka ya 2000,” alisema na kuongeza kuwa, “Mhe. Rais anajitahidi sana kujenga na kuboresha hospitali hizi kwa sababu yeye ni mzazi na anajua changamoto tunazokutana nazo kina mama hasa wakati wa kujifungua. Naomba azidi kutuletea vifaa vya kutosha na madawa katika hospitali yetu ya Wilaya ya Same, kwani hiyo ni hospitali tegemezi.”

Huduma nzuri alizopata Goodness zimeongeza matumaini kwa familia yake, huku ikionyesha mabadiliko makubwa katika sekta ya afya, hasa kwa wanawake na watoto wa Wilaya ya Same.


Related Posts