KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA UTEKELEZAJI MRADI WA UMWAGILIAJI NYIDA, SHINYANGA

-Ni mradi wa Umwagiliaji unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC)

NIRC Shinyanga

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo na Mifugo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi inayofanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Nyida mkoani Shinyanga.

Kamati hiyo imesema kinachofanywa na Tume kinaendana na thamani ya fedha inayowekezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miradi ya umwagiliaji nchini.

Akizungumza katika ziara fupi ya kukagua miradi hiyo mkoani Shinyanga, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deodatus Mwanyoka, amesema kamati
inaridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba thamani ya fedha inaonekana.

“Hata kwa macho ukiangalia ujenzi wa ofisi, bwawa na miundombinu mingine inaridhisha na Sh8 bilioni zilizoanza kufanyiwa uwekezaji zinaoneka.”

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa anaamini malipo yaliyobaki kiasi cha Sh5. 6 bilioni ili kukamilisha mradi huo unaotarajia kugharimu Sh13. 6 bilioni yatafanyika kwa wakati.

“Tuwaahidi ndugu zetu Tume, sisi hatutasita kuwasemea ili mradi huu ukamilike na wananchi waone matunda yake,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, fedha zilizowekezwa katika mradi huo zimetumika ipasavyo na kamati imeridhika kabisa na utekelezaji wake.

Hata hivyo, Mwanyoka alisema pamoja na kuridhika nakazi hiyo, Kamati inaagiza mambo mawili muhimu ikiwamo Tume kuhakikisha inakamilisha kwa wakati miradi yake ikiwamo wa Nyida ili ianze kutumika.

Vile vile, Tume imsimamie mkandarasi ipasavyo na Wizara ihakikishe fedha zinapatikana kwa wakati ili ajenda ya Rais Samia na Serikali ya kubadilisha kilimo cha Umwagiliaji iweze kuwa na tija kwa wakulima.

“ Kazi iliyofanyika hapa ni kubwa tumetembelea miradi mingi, Tume mnafanya kazi na tunatoa angalizo muda wa mradi ni mchache.
Mvua mwaka jana zilikuwa nyingi, mwaka huu hakuna hivyo mategemeo ya wananchi ni makubwa,” alisisitiza.

Awali Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Annamlingi Macha, alisema mkoa unaiipongeza Wizara na NIRC kwa kazi kubwa iliyofanyika katika miradi ya miradi ya Umwagiliaji.

“Mara kwa mara nimetembelea mradi huu na ule wa kwetu kule Chekereni Kilimanjaro. Tume inafanya mambo makubwa chini ya Rais Samia na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametuahidi watafanya uwekezaji hapa kwa kujenga mashine na ghala hivyo wakulima wa mpunga mtauza mchele na kunufaika zaidi kiuchumi,” alisema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Umwagiliaji na Ushirika Wizara ya Kilimo Mhandisi Dkt Stephen Nindi, amesema wanatambua kuwa Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan ina hamu ya kuona maendeleo ya wananchi wa Nyida ili kubadilisha uchumi hivyo mradi huo utakamilika kwa wakati.

“Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya Tume lengo la Serikali ni kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa. Tutafanya kazi kwa juhudi na kuleta mabadiliko ya haraka katika sekta ya kilimo tumepokea maagizo ya kamati na miongozo yake na itatekelezwa kwa maslahi mapana ya kilimo cha Umwagiliaji nchini.

“ Rais Dkt. Samia, amefanya kazi yake na ametekeleza nanyi kamati mmekuja kujiridhisha kuona fedha zilizotengwa zimefanyiwa kazi ipasavyo,’ aliongeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa (NIRC), Raymond Mndolwa, alisema Tume itahakikisha inakamilisha mradi huo ipasavyo kwani vyanzo vyake vya maji ni vya uhakika kutoka Mto Manonga na Ziwa Victoria.

Mndolwa alisema tayari Tume imenunua mashine kubwa mbili zitakazochimba mita 1,500 chini kujaza maji katika mabwawa.

Aliongeza kuwa ujenzi wa bwawa hilo umezingatia mahitaji yaliyopo ikiwamo kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo na masuala ya mazingira kwa watu wa jirani kutofanya shughuli za kibinadamu eneo la mradi.

“Tutaweka ulinzi eneo la mradi hadi katika bwawa, lengo likiwa ni kuona fedha za Serikali zilizotumika zinakuwa endelevu kwa muda mrefu kwa mradi huo kunufaisha wakulima na Taifa kwa ujumla.

“Mradi huu utanufaisha wananchi wa Nyida na Lyamalagwa ambako ulinzi utakaokuwepo utaanzia katika bwawa kwa kuzingatia kuwa litakuwa na ufugaji wa samaki na ni mradi endelevu utakaoleta mabadiliko chanya katika sekta ya Kilimo,” alisema.

Akifafanua kuhusi mrasi huo, Mhandisi wa Mkoa Ebeneza Kombe, alisema mradi huo wa kimkakati unaghariku zaidi ya Sh13. 6 bilioni na unatekelezaji wake umeanza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili, 2024.

Alisema mradi huo ukikamilika utanufaisha eneo la Umwagiliaji la hekta 800 kwa Nyida na hekta 1,500 kwa Lyamalagwa na zaidi ya wakulima 4,5000 kutoka Nyida na Lyamalagwa watanuafaika.

Related Posts