Kichocheo ukuaji uchumi Tanzania chatajwa

Arusha. Uwajibikaji na uwazi katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia Tanzania, unatajwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali kuhusu namna rasilimali zinavyowanufaisha.

Pia, Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili rasilimali hizo ziweze kuinua uchumi kuanzia wa mtu binafsi hadi Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema hayo leo Alhamisi Machi 13, 2025 alipomwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko katika kikao cha 62 cha Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Uhamasishaji wa Uwazi katika Sekta ya Uziduaji (Eiti) uliofanyika jijini Arusha.

Amesema wananchi wanahitaji kujua rasilimali zilizopo nchini zinawanufaisha vipi, ndiyo maana Tanzania imekuwa ikiweka wazi mapato yatokanayo na sekta hizo ikiwa ni njia mojawapo ya kuonyesha uwajibikaji.

“Tanzania ni Taifa lenye utajiri wa rasilimali asili ikiwemo madini na gesi asilia, rasilimali hizi zina uwezo wa kukuza maendeleo ya uchumi na kuboresha maisha ya wananchi, ndiyo maana tunasisitiza uwazi na uwajibikaji tukijua ndiyo msingi wa uhusiano mkubwa kati ya Serikali na wananchi.

“Watanzania wana haki ya kujua jinsi mapato yatokanayo na rasilimali zetu yanavyotumika na yanavyowanufaisha, ndiyo maana tunaendelea kuongeza uwazi katika masuala haya,” amesema.

Bashungwa amesema Tanzania mwaka 2015 ilitunga Sheria namba 13 ya Teiti ili kukidhi vigezo vya kimataifa vya Eiti.

Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Ludovick Utouh, amesema kikao hicho kimekutanisha wajumbe wa bodi kutoka nchi 57 duniani ambazo ni wanachama wa Eiti.

“Kikao hiki ni muhimu kwani kimekutanisha wajumbe kutoka nchi wanachama na tangu Tanzania ijiunge na Eiti mwaka 2009 hii ni mara ya kwanza kwa taasisi hiyo ya kimataifa kufanya kikao chake hapa nchini.

“Hadi sasa Tanzania imechapisha na kutoa ripoti 14 zinazolinganisha malipo yaliyofanywa na kampuni za madini, mafuta na gesi asili na mapato yaliyopokewa na Serikali. Tunatarajia kutoa ripoti ya 15 kabla ya Juni mwaka huu. Ukiangalia ripoti zilizopita utaona kila mwaka mchango wa sekta hizi unaongezeka,” amesema Utouh, aliyewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema uimarishaji wa diplomasia umeendelea kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa.

Amesema Tanzania ni wadau wa kuhakikisha eneo la uwazi na uwajibikaji kwenye sekta ya uziduaji inapewa kipaumbele kikubwa.

Mavunde amesema imekuwa miongoni mwa nchi wanachama wa Eiti ambao wanafanya vizuri, ndiyo maana imeweza kuvutia kufanyika mkutano huo.

Amesema wananchi wengi wamekuwa na hamu ya kujua namna Taifa linavyonufaika na rasilimali zake na kupitia utaratibu wa uwazi ambao unawekwa kwenye taarifa za mapato unasaidia wananchi kufahamu jinsi Taifa linavyonufaika na rasilimali hizo.

“Tulishatoa ripoti ya 14 ya uwazi na uwajibikaji ambayo imeonyesha Tanzania inaendelea kufanya vizuri hasa katika kuiweka wazi mikataba iliyoingiwa kwenye sekta ya madini na nishati, na kuweza kutambua wamiliki wa kampuni mbalimbali ambazo zinafanya kazi kwenye sekta ya uziduaji hapa nchini,” amesema.

“Tafsiri yake katika eneo hili hivi sasa kama nchi tumejizatiti kuhakikisha tunaweka taarifa zote wazi ili wananchi wafahamu kinachoendelea katika sekta ya uziduaji na sisi kama wizara, tutaendelea kuhakikisha taarifa zote zinawekwa kwa uwazi ili wananchi wafahamu kinachopatikana kupitia rasilimali ambazo tumejaliwa,” amesema.

Serikali ilivuna Sh1.877 trilioni kutoka kampuni 44 zilizohusishwa katika sekta ya madini, mafuta na gesi, huku tofauti ya malipo na mapato ikiwa ni Sh402.41 milioni kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya 14 ya Teiti, Waziri Mavunde amesema kampuni 26 kati ya hizo ni za madini, saba ni za gesi asilia na mafuta na 11 zinazotoa huduma katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia.

Related Posts