Kitakachofuata baada ya SADC kuondoa vikosi DRC

Dar es Salaam. Uamuzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuondoa vikosi vyake vya kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), unatajwa kuwa mbinu ya kushinikiza njia mbadala ya kuisaka amani nchini humo.

Kwa upande mwingine, uamuzi huo unaelezwa ni dalili ya vikosi hivyo vinavyojulikana SAMIDRC kusalimu amri, baada ya kuzidiwa nguvu na waasi wa M23 waliovamia na kuidhibiti miji ya Goma na Bukavu nchini DRC.

SADC ilitangaza uamuzi huo jana Machi 13, 2025 kupitia Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa katika mkutano wa wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo kuhusu mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC.

Katika taarifa ya pamoja jumuiya hiyo imesema vikosi vya SAMIDRC vitaanza kuondoka DRC kwa awamu.

“Lazima tuharakishe utekelezaji wa uamuzi uliofikiwa wakati wa mkutano wa pamoja wa SADC-EAC ikiwa ni pamoja na utekelezwaji wa michakato ya amani ya Rwanda na Nairobi. Zaidi ya hayo, mazungumzo ni msingi muhimu wa kuwahakikishia watu wa DRC amani ya kudumu.

“Wakati ujumbe wetu ukiwa katika hatua ya kujiondoa, tunaomba ushirikiano kuwezesha hatua hiyo na ya kuhamisha vifaa vyetu,” alisema Mnangagwa.

SADC ikifikia uamuzi huo, tayari Afrika Kusini ilishapoteza wanajeshi 14 ambao ni sehemu ya kikosi hicho, Tanzania wawili, Malawi wawili na wengine wawili kutoka vikosi vingine vya Umoja wa Mataifa.

SAMIDRC ilianza kutuma vikosi DRC tangu Desemba, 2023 kuisaidia Serikali ya DRC, ambayo pia ni mwanachama wa SADC kurejesha amani na usalama.

Afrika Kusini ndiyo iliyotuma idadi kubwa ya wanajeshi katika kikosi hicho wanaokadiriwa kufikia 1,000. Baadaye kukawa na shinikizo la kutaka wanajeshi hao waondolewe, huku Malawi Februari mwaka huu, ilianza kujiandaa na mchakato wa kujiondoa DRC.

Kutokana na uamuzi huo wa SADC, swali linabaki nini kitafuata baada ya SAMIDRC kuondoka DRC?

Nini kimechochea uamuzi huo?

Ingawa taarifa ya pamoja ya SADC haikuweka wazi sababu, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sabatho Nyamsenda anaona mambo yanayoendelea katika mgogoro huo ndiyo yaliyochochea uamuzi uliofikiwa.

Amesema katika mgogoro huo kumeibuka majibizano kati ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame na wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Pia kumetokea vifo vya wanajeshi wa Afrika Kusini, Malawi na Tanzania.

Mgogoro huo kwa mujibu wa Dk Nyamsenda, umeibua tishio la kuendelea na kuwa wa kikanda kwa sababu kuna nchi ndani ya ukanda wa maziwa makuu zinaunga mkono kila upande zinaoona upo sahihi.

“Katika mazingira hayo, upo uwezekano nchi hizo zinazounga mkono pande tofauti, zikaingia vitani na hatimaye mgogoro ukatanuka zaidi,” amesema.

Amesema inaonyesha bado SADC inadhani njia ya diplomasia na mazungumzo katika kutafuta amani inapaswa kuendelea.

“Ukiunganisha yote hayo unapata picha kuwa mgogoro una wadau wengi zikiwamo nchi za ndani na nje ya Afrika. Kuna hatari ya mgogoro kuendelea. Ni mgogoro ambao ni zaidi ya mapigano,” amesema.

Ni nini kitafuta baada ya uamuzi huo? Dk Nyamsenda amesema anadhani SADC itaongeza nguvu kuingia kwenye utatuzi wa kidiplomasia na njia za amani.

“Kama pande zinazogombana zitakubaliana na njia za kidiplomasia, kuna uwezekano wa matokeo chanya kupatikana,” amesema.

Kwa upande mwingine, amesema kilichofanywa na jumuiya hiyo, inaweza kuwa dalili ya kushindwa dhidi ya waasi wa M23 baada ya kuzidiwa nguvu na kuona wanajeshi wa vikosi vya SAMIDRC wanaendelea kupoteza maisha.

“Kama uhalisia ni huo maana yake hatima ya amani ya DRC ipo mikononi mwa masharti ya waasi wa M23. Ikiwa hivyo, DRC italazimika kukubaliana na matakwa ya waasi ili irudishe amani,” amesema.

Kwa mtazamo wa kidiplomasia, Balozi Christopher Liundi amesema uamuzi wa SADC unaweza kuwa na tija katika kumaliza mapigano yaliyodumu kwa takribani miongo mitatu nchini DRC.

Amesema kuondolewa kwa vikosi kunatoa nafasi kwa njia nyingine za kuisaka suluhu kuchukua nafasi, yakiwemo mazungumzo.

“Hivi karibuni kuna jitihada za waasi na DRC kukutana katika meza ya mazungumzo, ni muhimu wakati juhudi za mazungumzo zinaendelea, kusiwe na nguvu za kijeshi zinazoendelea,” amesema.

Balozi Liundi amesema uamuzi wa kuondoa vikosi unaweza kuwa shinikizo la kutaka pande zinazogombana zikae mezani kumaliza tofauti zao, hivyo ni jambo la busara.

“Ukipeleka vikosi hata kama vya kulinda amani, maana yake unaruhusu silaha ziendelee kurindima, ukisitisha hilo, watu watatafuta njia mbadala,” amesema.

Amesema viongozi wa pande zote kati ya waasi na Serikali ya DRC wakubali kukutana na kuridhia kujadiliana.

“Mazungumzo yao yatakuwa na tija iwapo pande zote zitakubali kukutana na kujadiliana,” amesema.

Related Posts