Majalada 524 yachunguzwa na GCLA ikiwemo ya uhalali wa wazazi

Dodoma. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imesema majalada 524 yasiyohusiana na masuala ya jinai ikiwemo ya kutaka uhalali wa wazazi wa mtoto yamechunguzwa ndani ya kipindi cha miaka minne.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai wa mamlaka hiyo, Fidelis Bugoye ameyasema hayo leo Machi 14, 2025  wakati wa kuelezea mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita na mwelekeo wa mamlaka hiyo.

Amesema kuna ongezeko la watu wanaotaka huduma za vinasaba kwenye mamlaka hiyo kwa ajili ya uamuzi, hali inayotokana na uelewa wa huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.

“Zipo changamoto nyingi ambazo zinahitaji taarifa za vinasaba na hata zisizo za jinai na kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana jumla ya majalada 524 yamechunguzwa yakiwa yanahusiana na masuala yasiyo ya  jinai ambayo pengine ni kutaka uhalali wa wazazi yamefikiwa,”amesema.

 Amesema kwa mujibu wa sheria wamekuwa wakipokea maombi kutoka mamlaka ombezi zikiwa ni ustawi wa jamii, mawakili na mahakama kutaka kujua uhalali wa watoto kwa uzazi.

Amesema wakishamaliza uchunguzi taarifa hizo za siri hupelekwa kwa mamlaka ombezi ambao huzitoa kwa wakati unaofaa.

 Naye Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko amesema katika kipindi cha miaka minne uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kwa sampuli na vielelezo umeongezeka kutoka sampuli 155,817 mwaka 2021/2022 hadi kufikia sampuli 188,362 kwa mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 21.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha huu wa 2024/2025, kuanzia Julai hadi Desemba 2024, sampuli 108,851 zilifanyiwa uchunguzi sawa na asilimia 104.50 ya lengo la kuchunguza sampuli 104,161,”amesema.

Dk Mafumiko amesema katika kipindi hicho mamlaka ilipokea na kuhudhuria wito wa mahakama 6,986 kutoka mahakama mbalimbali nchini kwa ajili ya kutoa ushahidi wa kitaalamu.

“Utoaji wa ushahidi huo umechangia katika mnyororo wa haki jinai kwa kutoa maamuzi ya haki kwa muhusika na kwa wakati, hivyo kuchangia kuleta, amani na utulivu wa nchi,”amesema.

Aidha, amesema kumekuwa na ongezeko la vibali vya uingizaji wa kemikali kutoka vibali 40,270 kwa mwaka 2020/2021 hadi vibali 158,820 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 294 ya vibali vilivyotolewa.

“Ongezeko hili la vibali limetokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita, wadau kuongeza uelewa wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia shughuli za kemikali kwa kujengea uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama, inayotumika katika uombaji wa usajili na vibali,”amesema.

Related Posts