KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, ametangaza kikosi cha mastaa 24 kitakachoingia kambini kesho Jumamosi, huku nahodha Mbwana Samatta na kipa Aishi Manula wakitemwa kwa sababu tofauti, huku akiwapotezea mastaa watatu wa Singida BS waliobadili uraia.
Stars inajiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco utakaopigwa Machi 26 na Samatta ametemwa kwa sababu ya kuwa majeruhi wakati Manula aliyekuwa katika kikosi kilichofuzu fainali za CHAN na AFCON 2025 hajajumuishwa katika kikosi hicho.
Stars itacheza mchezo huo ugenini imejumuisha wachezaji wanaocheza ndani na nje ya nchi, wakiwemo kutoka ligi za England, Denmark, Australia, Iraq, Uturuki, na Morocco.
Miongoni mwa nyota walioitwa ni Simon Msuva (Al-Talaba SC, Iraq), Kelvin John (Aalborg BK, Denmark), na Selemani Mwalimu (Wydad Casablanca, Morocco).
Kocha Morocco, alitangaza kikosi hicho mapema leo na kusisitiza maandalizi yatafanyika kwa umakini ili kuhakikisha kuwa timu inakuwa na ubora wa kushindana na Morocco itakayokuwa nyumbani kwani ni moja ya timu bora barani Afrika na duniani kwa ujumla.
“Tunataka nafasi ya kwenda Kombe la Dunia na hii ni ndoto ya kila mtu. Tumezingatia tuna wachezaji gani kwa kipindi hiki sasa hawa ni wachezaji ambao tumeona wanaweza kutusaidia kwenye mchezo huo,” alisema Morocco ambaye alipoulizwa juu ya nafsi ya mastaa watatu wa Singida BS, Emmanuel Keyekeh (27), Arthur Bada (22) na Damaro Camara (21) kwenye kikosi chake, Morocco alisema; “Kuhusu wachezaji hao siwezi kuzungumza chochote maana sina uhakika juu ya kubadilisha kwao uraia na hizo taarifa nazisikia tu mitandaoni na magazetini.”
Kukosekana kwa nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kwa sasa huko Ugiriki akiwa na PAOK, kocha huyo alisema ni kutokana na majeraha huku akidai hii ni fursa kwa wachezaji wengine.
“Kukosa kwa Samatta kama timu inatakiwa tuwe na plan B (mbinu mbadala) kwenye mpira naamini tuna vijana ambao wanaweza kucheza kwa viwango,” alisema.
Mchezo huu ni moja ya hatua muhimu kwa Tanzania katika safari ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, ambapo mashabiki wanatarajia kuona kikosi hicho kikitoa ushindani kwa miamba hiyo ya Afrika na kupata matokeo mazuri.
Orodha kamili ya kikosi cha Stars ipo hivi; Makipa ni Yakoub Suleiman (JKT Tanzania), Ally Salim (Simba SC) na Hussein Masaranga (Singida BS)
Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba SC), Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Mohamed Hussein (Simba SC), Pascal Msindo (Azam FC), Mirajy Abdallah (Coastal Union) Ibrahim Abdulla (Yanga), Dickson Job (Yanga), Abdulrazack Mohamed (Simba SC), Ibrahim Ame (Mashujaa FC), Haji Mnoga (Salford City, Uingereza).
Viungo, Novatus Miroshi (Göztepe FC, Uturuki), Mudathir Yahya (Yanga), Yusuph Kagoma (Simba SC), Feisal Salum (Azam FC).
Washambuliaji: Charles M’Mombwa (Newcastle United Jets, Australia), Kibu Denis (Simba SC), Simon Msuva (Al-Talaba SC, Iraq), Clement Mzize (Yanga), Iddy Selemani (Azam FC), Selemani Mwalimu (Wydad Casablanca, Morocco) na Kelvin John (Aalborg BK, Denmark).
Timu P W D L F A P
1. Morocco 3 3 0 0 10 1 9
2. Niger 3 2 0 1 5 2 6
3. Tanzania3 2 0 1 2 2 6
4. Zambia 4 1 0 3 6 7 3
5. Congo 3 0 0 3 2 13 0
6. Eritrea 0 0 0 0 0 0 0