Mchange ahojiwa na Takukuru kwa tuhuma za ‘kujipitisha Kigamboni’

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wilaya ya Kigamboni, imemuhoji mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Habibu Mchange kwa tuhuma za kutaka kutoa rushwa kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho wa kata ya Tungi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtoa taarifa Mchange ni miongoni mwa wanaotaka kutia nia ya kugombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Kigamboni katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kitendo ambacho ni kinyume na sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 na kanuni za CCM kwa kufanya kampeni kabla ya dirisha kufunguliwa na kuahidi kutoa zawadi ambazo haziko kwenye ilani ya chama hicho.

Hata hivyo, viongozi mbalimbali wa CCM wamekuwa wakitoa kauli za onyo na kuwatahadharisha wale wanaotaka kuwania nafasi hizo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kusubiri muda ufike.

Miongoni mwa viongozi hao ni Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi kwa nyakati tofauti waliowaonya wale walioanza kampeni mapema kwamba, watawachukuliwa hatua.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 14, 2025 Mkuu wa Takukuru mkoa wa Temeke, Joseph Makungu amesema Machi 13 mwaka huu walipokea taarifa fiche kutoka kwa msiri kuwa Mchange ameandaa baadhi ya viongozi wa CCM kata ya Tungi ili awagawie fedha.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Temeke, Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za taasisi hizo katika wilaya ya Kigamboni.

Amesema baada ya kupokelewa taarifa ilifanyiwa uchunguzi wa awali kwa kuzingatia sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007 iliyofanyiwa marejeo ya mwaka 2022 na wachunguzi walifika katika ofisi ya CCM kata ya Tungi saa saba mchana.

“Maofisa walifuatilia na kubaini baadhi ya viongozi wa CCM walikubaliana kukutana saa nane kamili mchana ila baadaye muda ulibadilishwa na kuwa saa tisa alasiri kwa sababu walikuwa wanamsubiria Habibu Mchange,” amesema Makungu.

Amesema saa tisa Alasiri baadhi ya viongozi wa CCM kata ya Tungi waliingia ukumbini na baada ya muda mfupi gari aina ya kluger iliwasili kwenye maegesho ya magari ya ofisi hiyo ya CCM na baadaye iligundulika ndiyo iliyokuwa imembeba Mchange.

Makungu amesema kitendo hicho ni kinyume na sheria kwa kuwa si mtekelezaji wa ilani ya chama kwa kuwa si kiongozi, si mbunge, si mwakilishi na wala si diwani katika chama hicho kwa sasa kama kanuni ya 69 (6) kuhusu uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola inayosema:

 “Ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake kutoa misaada wakati wa uchaguzi unapokaribia ambayo ni dhahiri ina lengo la kuwavutia wapiga kura isipokuwa Rais, mbunge, mwakilishi na diwani ambao wako madarakani.” amesema Makungu.

Aidha baadhi ya viongozi wa CCM kata ya Tungi waliokutwa katika ukumbi huo hawakutaka kutoa ushirikiano kwa maofisa wa Takukuru, hivyo waliondoka nao kuelekea kwenye ofisi zao za wilaya kwa ajili ya mahojiano zaidi.

“Katika mahojiano wote walieleza kuwa kikao kile hakikuwa halali na kiliitishwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Tungi, Sebastian Kapela Mabula ambapo uchunguzi wa tuhuma hizi unaendelea,” amesema.

Amesema Takukuru inafuatilia kwa karibu wote wanaodaiwa kufanya kampeni mapema kwa kutoa rushwa kwa wapiga kura kwa jimbo la Kigamboni na Tanzania kwa ujumla.

Pia, amesema kumekuwa na  taarifa za Takukuru kuwafungia viongozi wa CCM wakiwa kwenye kikao cha kupanga uhamasishaji wa uandikishaji daftari la wapigakura, akisema  si za kweli bali maofisa ndiyo waliofingiwa na wanachama hao na kuwaachia baada ya kufika mwenezi wa chama hicho.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM  Wilaya ya Kigamboni, Stanley Mkandawile amesema viongozi wa kata waliita viongozi wa matawi ili kukutana na mtia nia Mchange ambapo awali alianzia kata za Pembamnazi.

“Kilichokea jana kuna mtia nia wa ubunge alitaka kutoa rushwa kwa wanachama na kusingizia kuwa walikuwa na kikao cha maandalizi ya uandikishwaji wa daftari la wapigakura ambayo wao walikuwa na kikao leo, lakini viongozi hao walifanya mkutano huo kinyume na sheria na bila kuwataarifu uongozi wa wilaya,” amesema Mkandawile.

Amesema hatua wanayoichukua ni kuwaita viongozi wa kata ya Tungi na kuwafikisha kwenye kamati ya maadili kwa kile walichokuwa wanakifanya,  kwani kikao chao hakikuwa cha halali wala kutambulika na chama.

Related Posts