MSD kujenga maghala mapya mikoa mitano

Dodoma. Bohari ya Dawa (MSD) inatarajia kuanza ujenzi wa maghala mapya katika mikoa ya Geita, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Mwanza na Ruvuma ili kuimarisha uwezo na kutatua changamoto za utunzaji wa bidhaa za afya.

Ujenzi huo umepangwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa ghala la kisasa la kuhifadhia bidhaa za afya linalojengwa na Bohari ya Dawa (MSD) katika eneo la Kizota, jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya MSD, Rosemary Silaa, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ghala la kisasa la kuhifadhia bidhaa za afya linalojengwa na MSD jijini hapa.

Silaa amesema MSD itaendelea na ujenzi wa maghala mapya kwa lengo la kutatua changamoto za utunzaji wa bidhaa za afya, ambapo baada ya ujenzi huu wa Dodoma na Mtwara MSD itaanza ujenzi wa maghala mapya mkoani Geita, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Mwanza na Ruvuma.

MSD kwa sasa ina uwezo wa kutunza bidhaa hizo kwenye mita za mraba 56,000 huku ikiwa na uhitaji wa mita za mraba 100,000 kukidhi mahitaji yake.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka ameipongeza MSD kwa kazi kubwa inayoifanya ya ujenzi wa ghala kubwa la kisasa ambalo litakwenda kutatua changamoto za utunzaji wa bidhaa za afya kwa kiasi kikubwa.

“Kazi mnayoifanya inaonekana, leo tumeona uwekezaji mkubwa wa ghala hili kubwa na la kisasa ambalo lina ubora wa kimataifa, serikali imewekeza hapa zaidi ya Sh23.7 bilioni kujenga ghala hili lenye mita za mraba 7,200 sisi kama kamati tunategemea kuona changamoto za utunzaji wa bidhaa za afya zinapungua,” amesema.

 Aidha, pamoja na kupongeza ujenzi wa maghala Kaboyoka amepongeza namna MSD inavyosambaza mashine za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, ambazo zimesaidia kupunguza gharama za huduma hiyo kwa wananchi.

“Siku hizi magonjwa ya figo yamekuwa mengi hadi watoto wadogo wanapata ugonjwa huo tunaishukuru MSD kwa kupunguza gharama ya huduma hii baada ya kuanza kusambaza mashine za kusafisha damu, sasa hivi tunaona huduma hiyo imepungua gharama kwa kiasi kikubwa,” amesema Kaboyoka.

Related Posts