Nini hatma ya masharti magumu ya Rais Putin kwa Ukraine

Rais wa Russia, Vladimir Putin, ameeleza kuwa anakubaliana na wazo la kusitisha mapigano nchini Ukraine, lakini ameweka masharti magumu kwa ajili ya amani ya kudumu. 

Hii inakuja baada ya Ukraine kukubali mpango wa kusitisha mapigano wa siku 30 kufuatia mazungumzo na Marekani. 

Hata hivyo, masharti aliyoweka Putin yameleta utata mkubwa, huku Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, akiyataja kama “mbinu za ujanja” na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuimarisha vikwazo dhidi ya Russia.

Kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Moscow leo, Putin ameeleza kuwa wazo la kusitisha mapigano ni sahihi lakini kuna maswali yanayopaswa kujibiwa na kujadiliwa kwa kina. Amesisitiza kuwa usitishaji mapigano lazima ulete amani ya kudumu na kushughulikia mizizi ya mzozo huu.

“Tunapaswa kujadiliana na washirika wetu wa Marekani ili kuhakikisha kuwa mapatano haya yanakuwa na msingi madhubuti. Huenda nitafanya mazungumzo na (Rais wa Marekani) Donald Trump,” amesema Putin.

Rais wa Russia, Vladimir Putin (kushoto) na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy.

Moja ya vipengele vya masharti aliyoweka ni kuhusu eneo la Kursk, ambalo Russia inadai kuwa lilivamiwa na vikosi vya Ukraine Agosti, 2024. Putin alidai kuwa Russia imedhibiti kikamilifu eneo hilo na askari wa Ukraine walioko huko wamezingirwa. “Kwa sasa wanaweza kuchagua moja ya mambo mawili tu: kujisalimisha au kufa,” ameongeza Putin kwa msisitizo.

Ukraine, Marekani zapingana na msimamo wa Russia

Rais Zelensky ameeleza kuwa kauli za Putin ni mbinu za kuchelewesha mpango wa amani. Katika hotuba yake ya kila usiku kwa taifa, Zelensky alisema: “Putin hajakataa moja kwa moja usitishaji mapigano, lakini kwa vitendo vyake, anajiandaa kukataa mpango huu.” 

Aliongeza kuwa Putin anajaribu kuchelewesha mchakato ili kupata muda zaidi wa kuimarisha jeshi lake.

Rais wa Marekani, Donald Trump (kulia) wakati wa mazungumzo na Rais wa Ukraine, Volorymyr Zelensky Februari 28, 2025 White House.

Huku hayo yakiendelea, Marekani imetangaza vikwazo vipya dhidi ya sekta ya mafuta, gesi na benki za Russia. Hatua hii imechukuliwa kama jaribio la kuiwekea Russia shinikizo zaidi kuafiki mpango wa amani bila masharti magumu.

Mazungumzo ya kidiplomasia na majibu yake 

Putin anatarajiwa kufanya mazungumzo na mjumbe maalumu wa Rais Trump, Steve Witkoff, ambaye alisafiri kwenda Moscow kwa mazungumzo hayo. 

Hata hivyo, haijulikani wazi ikiwa mkutano huo ulifanyika kama ilivyopangwa, kwani vyanzo vya habari vya Serikali ya Russia viliripoti kuwa ndege iliyodhaniwa kumleta Witkoff iliondoka Moscow bila kuthibitisha kama mkutano ulifanyika.

Kwa upande wake, Trump amesema angetamani kukutana na Putin ili kuhakikisha Russia inakubaliana na mpango wa kusitisha mapigano. “Tunataka kuona Russia ikisitisha mapigano,” alisema Trump alipokuwa katika Ikulu ya White House akizungumza na Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte.

Mgawanyiko kati ya Russia, Ukraine

Baada ya kauli za Putin na majibu ya Zelensky, inaonekana kuwa mgawanyiko baina ya pande mbili unazidi kuongezeka. 

Ukraine inataka mchakato wa hatua mbili: kwanza, usitishaji wa haraka wa mapigano na kisha mazungumzo ya amani ya muda mrefu. 

Kwa upande mwingine, Russia inashikilia msimamo kuwa haiwezi kutenganisha hatua hizo mbili na masuala yote yanapaswa kujadiliwa kwa pamoja na makubaliano ya jumla yafikiwe.

Mzozo huu unaipa Marekani changamoto kubwa, kwani Trump amesisitiza kuwa anataka kuona matokeo ya haraka ili kumaliza vita hivi ndani ya siku chache. Hata hivyo, kwa mtazamo wa sasa, Putin haonekani kuwa tayari kutoa mwanya wa haraka wa amani.

Matokeo ya msimamo wa Russia

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanauona msimamo wa Putin ni mkakati wa kuchelewesha na kupata muda wa kuimarisha vikosi vyake. 

Profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Harvard, John Mearsheimer, anasema: “Russia mara nyingi hutumia mbinu za mazungumzo marefu ili kujipatia muda wa kujipanga kijeshi na kimkakati.”

Hali hii inathibitishwa na mashambulizi mapya yanayoendelea, ambapo pande zote mbili zimeripoti mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones). 

Ukraine ilisema kuwa watu saba, wakiwamo watoto, walijeruhiwa katika shambulio lililotokea Kharkiv. Wakati huo huo, Russia iliripoti moto mkubwa katika kituo cha mafuta cha Tuapse.

Mustakabali wa mazungumzo ya amani

Kwa sasa, swali kuu linabaki: Je, Putin yuko tayari kwa amani, au anajaribu kuchelewesha muda? Kwa mtazamo wa Ukraine, Russia inatumia hila za kidiplomasia ili kupata wakati wa kujihami. Kwa upande wa Russia, viongozi wake wanasisitiza wanataka Amani, lakini kwa masharti.

Ikiwa Russia itaendelea kuweka masharti magumu, kuna uwezekano mkubwa kuwa mpango wa kusitisha mapigano wa siku 30 hautafua dafu. 

Ukraine inatarajia kuwa shinikizo la kimataifa, hususan kutoka Marekani na NATO, litailazimisha Russia kufikia makubaliano ya kweli.

Wakati huo huo, dunia inasubiri kuona ikiwa mazungumzo ya Trump na Putin yatakuwa na matokeo chanya, au yataishia kuwa sehemu ya mchezo wa kisiasa wa Russia unaolenga kuchelewesha mchakato wa amani kwa faida yake ya muda mrefu.

Related Posts