Simba V Dodoma Jiji… Ni mechi ya kisasi

UMUHIMU wa pointi tatu za mchezo wa leo baina ya Simba na Dodoma Jiji katika Ligi Kuu Bara, zinatoa majibu ya namna upinzani unaotarajiwa kuwepo muda wote wa dakika 90 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam saa 10:00 jioni.

Simba inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 54, inahitaji ushindi ili kupunguza gepu na vinara Yanga yenye 58. Ushindi kwa Simba leo utawafanya kufikisha pointi 57, moja nyuma ya Yanga.

Kwa upande wa Dodoma Jiji, inashika nafasi ya nane ikikusanya pointi 27,n inasaka ushindi ili kupanda nafasi moja juu hadi ya saba ikiishusha Fountain Gate na kuwa sawa na JKT Tanzania, zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, pia kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani.

Katika mchezo kwa kwanza, Dodoma ililala kwa bao 1-0 lililotokana na penalti lililofungwa na Jean Charles Ahoua katika dk63 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Rekodi za jumla zinainyima nafasi Dodoma Jiji kufurukuta mbele ya Simba kwani katika mara zote tisa walizokutana katika Ligi Kuu Bara, hawajapata ushindi wala sare, zaidi ikipoteza nyumbani na ugenini.

Si kupata pointi tu, bali Dodoma Jiji mbele ya Simba imekuwa haina makali ya kutikisa nyavu ikifanikiwa kufunga mabao mawili pekee huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16.

Katika mechi saba za mwisho kati ya tisa, Dodoma Jiji haijafunga bao lolote dhidi ya Simba, huku mabao yake mawili iliambulia msimu wa kwanza walipopanda daraja kushiriki Ligi Kuu Bara 2021-2022 ambapo mechi ya kwanza ilifungwa 1-2 nyumbani, kisha ugenini ikachapwa 3-1.

Pia Dodoma Jiji imekuwa na rekodi mbaya msimu huu kwenye ligi kwani kati ya mechi 10 za ugenini, haijashinda zaidi ya kuambulia sare tano na kupoteza tano ikiruhusu mabao 14 na kufunga manane.

Simba inapokuwa nyumbani, imefanya vizuri ikishinda mechi saba kati ya 10, ikipoteza moja na sare mbili ikifunga mabao 24 na kuruhusu matano.

Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amezungumzia utayari wa kikosi chake kuelekea mchezo huo akisema: “Tumejiandaa kucheza na Dodoma, haiwezi kuwa mechi rahisi hasa ukizingatia huu ni mzunguko wa pili. Dodoma ina mwalimu mzuri, Mecky ni kocha anayependa ushindani kwani hata mechi ya kwanza dhidi yao haikuwa rahisi.”

Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime, alisema: “Ligi ni ngumu, Simba wanapambania ubingwa na sisi tunataka kukaa sehemu nzuri, hiyo ndiyo sababu itafanya mechi kuwa ngumu.

“Mashabiki wa Dodoma Jiji waje kwa wingi na wa Simba waje kwa wingi, naamini burudani itakuwa nzuri.”

Matola amebainisha, Che Fondoh Malone na kipa Moussa Camara wote ni majeruhi.

“Kwa mchezo wa kesho (leo) tutaendelea kumkosa Che Malone na Camara ambao ni majeruhi ingawa Camara ameanza mazoezi na tunatarajia mechi zijazo atakuwepo,” alisema Matola.

“Tunafahamu namna mchezo utakavyokuwa mgumu, hivyo tumejiandaa kuona namna ya kupata matokeo mazuri.”

Dodoma msimu huu katika mechi 22 za ligi ilizocheza hadi sasa imeshinda saba, sare sita na kupoteza tisa, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 27.

Kwa upande wa Simba inayofundishwa na Fadlu Davids, mechi zake 21 ilizocheza imeshinda 17, sare tatu na kupoteza moja ikifunga mabao 46 na kuruhusu manane.

Beki wa Dodoma, Abdi Banda alisema: “Kwa niaba ya wachezaji tupo vizuri, hakuna kingine tunachowaahidi Wana Dodoma zaidi ya kwenda kupambana.

“Utakuwa mchezo mzuri kwa sababu kila timu inataka pointi tatu, sisi zaidi tunazitaka pointi tatu kutokana na namna tulivyoachana pointi na wale tunaokimbizana kwenye msimamo.

“Mchezo wa Dodoma na Simba unakuwa mgumu, sisi wachezaji tunalitambua hilo, hivyo tunafahamu tunakwenda kucheza mchezo wa aina gani kulinganisha na nafasi tuliyopo.”

Related Posts