Imeandikwa na Mzee wa Atikali: Buriani mama yangu mkubwa Tabitha Siwale, waziri wa kwanza mwanamke
“Mama Tabitha Siwale became Tanzania’s first female Minister in 1975”. Prof. M. Mwandosya, Jan. 20, 2014.
“Pole sana Ganga. Hiki ni kilio chetu sote tuliomfahamu Mama Siwale na Taifa pia. Mama Siwale alifungua njia za uhuru wa wanawake kujieleza na kutambuliwa sawa na wanaume. Alionyesha njia sahihi za mwanamke kuheshimika kama kiongozi kwa kufanya kazi kwa bidii na kujiamini. Tutamkumbuka sana.” Mama Loyce Francis Nyalali, Mwalimu wa “Mzee wa Atikali” Oysterbay Primary School, Machi 14, 2025.
Wanawake maarufu watatu hapa nchini; Bibi Titi Mohammed, Lucy Lameck na Mwami Theresa Ntare walikuwa wanawake wa kwanza kuwa naibu mawaziri baada ya kuteuliwa na Rais Julius Kambarage Nyerere mwaka 1962.
Je, iwapo hawa wanawake watatu walikuwa wa kwanza kuwa naibu mawaziri, nani alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa waziri?
Kama alivyoeleza kwa ufasaha hapo juu Profesa Mark Mwandosya, mwanamke wa kwanza kuwa waziri hapa nchini si mwingine bali ni Mama Tabitha Siwale ambaye aliteuliwa na Rais Nyerere kuwa Waziri Jumapili, Novemba 9, 1975.

Mama Siwale alivyopenda kuvaa akiwa Waziri
Mama Tabitha Siwale, ambaye aliumaliza mwendo Jumatano, Machi 12, 2025 saa 5:00 usiku kwenye Hospitali ya Hindu Mandal akiwa na miaka 86, alikuwa ni mama mkubwa wa “Mzee wa Atikali”.
Tarehe na mahali pa kuzaliwa
Mama Tabitha Siwale, ambaye kabla ya kuolewa aliitwa Tabitha Ijumba Wilfred Mwambenja, alizaliwa Alhamisi, Julai 28, 1938 huko Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Babu yake Tabitha Siwale aliitwa Mzee Mwambenja Mwasalukwa. Mzee huyu alikuwa msomi na “Deputy Chief”. Wanyakyusa walishindwa kutamka “Deputy” wakamwita “Liputi”.
Mzee huyu alikuwa na wake na watoto wengi. Miongoni mwa watoto wake ni Alexander (Hakimu), William (Mwenyekiti wa TANU Rungwe 1955-1969), Wilfred (Baba yake Tabitha) na Halliday (Baba yake mama Sophia ambaye ndiye mama mzazi wa “Mzee wa Atikali”). Iponjola, Katumba “Mwambenja Avenue”, Rungwe ndiko kwenye ukoo wa Mwambenja.
Wakati wa harakati za kupigania uhuru, siasa ilirindima vilivyo kwenye ukoo wa Mwambenja kama Profesa Mark Mwandosya alivyosimulia katika kitabu chake “38 Reflections on Mwalimu Nyerere” uk. 250 :
“Our house was nothing but political. For, my father and his colleagues, who included Mzee Wilfred Mwambenja, the father of Tabitha Siwale, would engage in endless political debates.”
Wakati wa harakati hizo, Mwalimu Nyerere, Oscar Kambona na Rashidi Kawawa mara kwa mara walilala nyumbani kwa Mzee William Mwambenja. Keneth Kaunda wa Zambia pia alifika na kulala hapo na hadi leo anakumbukwa na Wana-Mwambenja kwa usemi wake “I only eat vegetables like an elephant” kwa vile kila alipochinjiwa jogoo, aligoma kula kwa kuwa alikuwa “Vegetarian”
Tabitha alipenda siasa tangu utotoni na alikuwa akihudhuria mikutano ya TANU kwa kificho kwani baba yake alimkataza akimhimiza ajikite kwenye masomo.
Safari ya elimu ya Tabitha
Tabitha alianza shule mwaka 1947 katika Native Authority Primary School”. Alikuwa mwanafunzi mwenye akili sana. Alifanya mtihani wa darasa la nne mwaka 1951 na akafaulu na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Kati ya Tosamaganga Girls. Huko ndiko alikoonana kwa mara ya kwanza na Edmond Siwale aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Kati ya Tosamaganga Boys, ambaye baadaye alikuja kuwa mume wake.
Tabitha Siwale alifanya mtihani na kuchaguliwa kujiunga na Tabora Girls “Warsaw” mwaka 1955. Enzi hizo, ni wasichana wachache sana na wenye akili ndio waliofanikiwa kupata fursa ya kusoma shule hii. Tabitha alikuwa miongoni mwao na alihitimu shuleni hapo mwaka 1958.
Tabitha alipenda kujiendeleza kielimu hivyo alisomea uchumi wa kijamii katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Geita, akapokea mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Mpwapwa na kisha akaanza kazi ya ualimu mwaka 1961.

Mama Siwale (kushoto) akiwa na mdogo wake, Sophia, Mama yake Mzee wa Atikali.
Mwaka 1965, Mama Siwale alisafiri hadi Nairobi, Kenya ambako alikwenda kusomea kozi ya “Home Economics” na kutunukiwa shahada mwaka 1968.
Mama Siwale: Mwalimu Mkuu
Mama Siwale, aliyekuwa mmoja wa wanawake wazalendo wa kwanza nchini kuwa walimu wakuu, alihudumu kama Mwalimu Mkuu kwenye shule zifuatazo :
Mama Siwale alihudumu kama Mwalimu Mkuu wa Shule ya Bwiru Girls na alihakikisha wasichana wanapata elimu bora ya maisha. Wanawake wengi maarufu waliosoma shule hii walipitia mikononi mwake akiwemo Rachel Nyirabu, mke wa Gavana wa pili wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Charles Nyirabu.
Akiwa Bwiru, Mama Siwale alikutana tena na Edmond Siwale, aliyekuwa mwalimu katika shule ya Bwiru Boys. Baadaye walifunga ndoa na kupata watoto wanne – Fred, Mary, Abel na Maka.
Baada ya mafanikio makubwa Bwiru Girls, Mama Siwale alihamishiwa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe, Tanga ambako pia alileta mafanikio makubwa. Mama Siwale alijulikana kama mwalimu mkuu mkali mwenye kusisisitiza sana nidhamu.
Novemba 2, 2019, Salome Peter, mmoja wa wanafuzi wa zamani wa Korogwe Girls alisimulia mambo yalivyokuwa enzi zao miaka ya 1970 chini ya Mwalimu Mkuu, Mama Siwale:
“Mimi ni mmoja wa wasichana waliobahatika kuchaguliwa kujiunga Korogwe Girls. Headmistress alikuwa Mama Tabitha Siwale. Shule ilikuwa ya mchepuo wa kilimo. Mama Siwale alitulimisha mashamba makubwa. Kila mwanafunzi wa kidato cha 1 hadi 6 alipewa eneo bila kujali alikuwa mtoto wa kiongozi au nani. Pale tulisoma na watoto wa Vigogo. Kulikuwa Anna Watiku, mtoto wa JK Nyerere, Asha Rose Migiro na ndugu zake (mmoja ni Balozi Afrika Kusini) nk. Kilimo kilikubali mno- mahindi, matango, matikiti nk. Kila mwanafunzi alipewa jembe lenye namba, ukipoteza unalipa. Kila tulicholima kilikuwa kwa matumizi yetu. Rais Nyerere alipokuja alishangaa eka na eka zimezaa vizuri. Alivutiwa sana. Mama Siwale alikuwa msimamizi hodari aliyefuatilia sana suala la masomo, nidhamu na shule ilikuwa safi mno ndiyo maana Rais Nyerere akamteua kuwa Waziri mwaka 1975.”
Mama Siwale, kwa upande wake, aliwahi kuhabarisha:
“Niliongoza shule hizo za Bwiru na Korogwe kwa ufanisi mkubwa. Kwa mfano, Korogwe ilikuwa shule iliyotuma idadi kubwa zaidi ya wasichana kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nilikuwa mkali sana na sikuvumilia uzembe. Sasa ninafurahia matunda ya kazi yangu. Miongoni mwa wanafunzi ni Dk Asha Rose Migiro na Kejo Bisimba (Hellen)”
Walimu wakuu wapelekwa Kivukoni
Mwaka 1975, walimu wakuu wote wa shule za sekondari nchini walipelekwa katika Chuo cha Siasa cha Kivukoni kwa mafunzo ya siasa ya ujamaa kwa mwaka mmoja. Mama Siwale alimchukua mtoto wake wa mwisho, Maka, aliyekuwa mtoto mchanga, katika safari hiyo. Akaenda kusoma akiwa na mwanaye huyo.
Jioni ya Jumatatu, Novemba 3, 1975, Ofisi ya Rais Ikulu ilimpigia simu Mkuu wa Chuo cha Kivukoni. Bahati mbaya hakupatikana. Ikabidi Peruzi Butiku, mke wa Joseph Nyerere, mdogo wa Mwalimu Nyerere, atumwe kwenda chuoni Kivukoni. Mama Siwale, akiwa darasani, alishtukia anatakiwa atoke nje alikokutana na Peruzi aliyempa maagizo kuwa Rais Nyerere anamhitaji Ikulu mara moja.

Baraza la Mawaziri likiwa na wanawake wawili (Mama Siwale na Julie Manning).
Mama Siwale alipatwa na hofu kubwa kwani kuitwa Ikulu na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, halikuwa jambo dogo:
“Nilikuwa na wasiwasi mkubwa. Sikuamini Rais angeniita. Nikajiuliza maswali mengi lakini nikakosa majibu.”
Safari fupi ya kutoka Kivukoni hadi Ikulu ilionekana ndefu kama safari ya kutoka Musoma hadi Mtwara!
Mama Siwale ateuliwa mbunge
Mama Siwale alifika Ikulu akiwa na hofu kubwa akijaribu kuwaza ni kosa gani ambalo huenda alilifanya. Rais Nyerere alipomweleza kuwa amemteua kuwa mbunge kupitia nafasi 10 za uteuzi wa Rais, alipigwa butwaa. Hakuamini alichokisikia na akaomba Rais Nyerere arudie taarifa hiyo. Rais Nyerere alicheka sana na akarudia ndipo Mama Siwale alipotambua kuwa ameteuliwa.
Usiku huo saa 2:00, Taarifa ya Habari, kupitia RTD, ilitangaza uteuzi wa Mama Siwale pamoja na Hadija Swedi, Anna Kabati na wengine sita kuwa wabunge.
Mama Siwale ateuliwa waziri
Jumapili, Novemba 9, 1975, Rais Nyerere alimwita tena Ikulu Mama Siwale na kumweleza kuwa amemteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji.
Mama Siwale alishangaa kwa kusema: “Lakini mimi si mtaalamu wa ardhi.” Rais Nyerere alicheka na kumjibu:
“Kama nimekuteua, tayari nimefanya utafiti wa kutosha. Nina imani na wewe; utajifunza kazi ukiwa kazini.”
Baraza la Mawaziri lilipotangazwa, Julie Manning ni mwanamke mwingine aliyekuwa ameteuliwa. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria.
Mama Siwale anatambuliwa kuwa ndiye hasa waziri wa kwanza mwanamke kwa vile yeye ndiye alitangulia kuapa.
Mama Siwale ajichana ugali kwa Mama Sophia kusherehekea
Mama Siwale alipotoka Ikulu, aliwachukua ndugu na marafiki wachache na breki ya kwanza ikawa Masaki nyumbani kwa mdogo wake, Mama Sophia, (Mama wa “Mzee wa Atikali”). Walisali kumshukuru Mungu na walipomaliza, Mama Sophia alimweka kando kitinda mimba wake, Carol “Manecha” aliyekuwa mtoto mchanga akapika ugali wa nguvu kwa ajili ya dada yake, Mama Siwale, mwanamke wa kwanza kuwa waziri pamoja na wageni wote!
Mama Siwale aleta mabadiliko wizarani
Licha ya kutokuwa na ubobevu kwenye masuala ya ardhi, Mama Siwale alileta mabadiliko mengi kwenye Wizara ya Ardhi ambayo yameainishwa kwenye makabrasha mbalimbali ya wizara hiyo.
Mama Siwale amkwamua Bibi Titi Mohammed
Serikali ilipopitisha sheria ya kutaifisha majumba, ilitaifisha nyumba mbili za Bibi Titi Mohammed.
Bibi Titi alihukumiwa kifungo cha maisha mwaka 1970 baada ya kupatikana na hatia ya kutaka kuipindua Serikali na kufungwa jela ya Isanga, Dodoma. Hata hivyo, Rais Nyerere alimpa msamaha mwaka 1972. Aliporejea, akakuta nyumba zake zimetaifishwa. Alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake huku akienda kwa mawaziri lakini akagonga ukuta.

Mama Siwale akiongoza ujumbe wa Tanzania huku Profesa Mark Mwandosya akiwa nyuma yake, kwenye Mkutano wa 21 wa UNESCO, Belgrade, Yugoslavia 1980/81.
Mama Siwale hakuwa na simile kwenye suala la kutetea haki. Hivyo, mwaka 1976, akiwa amekaa kwenye uwaziri kwa mwaka mmoja tu, aliamua “kumvaa” Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliyekuwa akiogopwa sana na kumpiga shule kuhusu haki ya Bibi Titi Mohammed kurudishiwa nyumba. Hatimaye, Baba wa Taifa akaingia kwenye mfumo” na walau Bibi Titi akarudishiwa nyumba moja baada ya dokezo la Mama Siwale lililosheheni hoja zenye mashiko kukubaliwa na Rais Nyerere. Bibi Titi alimshukuru sana na akasema kuwa maishani hatakuja kumsahau Mama Siwale kwa wema huo mkubwa aliomfanyia.
Mama Siwale ateuliwa Waziri wa Elimu
Mwaka 1980 baada ya uchaguzi mkuu, Mama Siwale alihamishiwa Wizara ya Elimu ambako alileta mabadiliko kadhaa. Miongoni mwa mabadiliko aliyoleta kupitia waraka ni kuelekeza kuwa shule za seminari haziko kwenye mfumo wa kiserikali hivyo wanaofaulu kidato cha nne hawawezi kujiunga na kidato cha tano shule za serikali.
Mwaka 1982, Mama Siwale alirudishwa tena Wizara ya Ardhi hadi mwaka 1984 uwaziri ulipogota, akaendelea kuwa mbunge hadi mwaka 2000.
Tabitha: Mwanamke msomi, mchapakazi na madilifu
Mama Siwale alikuwa mchapakazi hodari na mwadilifu wa hali ya juu.
Mama Siwale aliwahi kunena:
“Katika maisha yangu, maneno “Sijui” au “Siwezi” hayamo kwenye kamusi yangu. Kazi yoyote unayopewa ifanye kwa bidii yako yote ili matokeo yake yaonekane na watu waithamini.”
Mama Siwale ampigania mwanamke haki ya ardhi
Mama Siwale, akiwa mbunge, alitoa mchango mkubwa kwenye masuala ya haki na usawa wa kijinsia pamoja na umiliki wa ardhi kwa mwanamke. Zamani mwanamke kumiliki ardhi ilikuwa kizungumkuti, siyo kama hali ilivyo sasa. Miongoni mwa waliotoa mchango mkubwa ni Mama Siwale.
Mwaka 1993, Mama Siwale alikuwa mmoja wa wabunge 55 waliotaka Serikali ya Tanganyika.
Mama Siwale apewa tuzo ya “Mwanamke wa Karne”
Mwaka 2000, taasisi maarufu ya Marekani ilimtunuku Mama Siwale tuzo ya “Mwanamke wa Karne” kwa mchango wake mkubwa kwa Taifa lake.
Mama Siwale atumikia bodi mbalimbali
Uchapakazi na uadilifu wa Mama Siwale ulipelekea ateuliwe kuwa Mwenyekiti au M/Mwenyekiti wa Bodi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na PPF, NBC, DAFCO, NMC, Baraza la Taasisi ya Ardhi na Women’s Advancement Trust.
Mama Siwale: Kioo cha mabinti wa Kikyakyusa
Wazazi wengi Wanyakyusa walipenda kutoa mfano wa Mama Siwale kila walipowahimiza mabinti zao kupenda masomo. Hivyo, mabinti wengi wakapenda kusoma ili nao wawe kama Mama Siwale. Wazazi wengine waliamua kuwaita mabinti zao “Tabitha”
Mama Siwale: “Mke na jiko ni uji na mgonjwa”
Mama Siwale alikuwa mpigania haki za wanawake mahiri sana. Hata hivyo, daima alisisitiza kuwa mke ni lazima alitambue jukumu lake na aelewe jiko ni sehemu muhimu ya maisha yake. Alipokuwa Waziri, alikuwa akiuvua uwaziri getini na kuvaa cheo chake cha mke na mama.
Mama Siwale na kuzaliwa kwa “Mzee wa Atikali
Baba yake “Mzee wa Atikali” aliwahi kuwa “Area Commissioner” Geita. Siku moja, Mama Siwale alifika Geita kumuona mdogo wake, Mama Sophia, aliyekuwa na ujauzito wa “Mzee wa Atikali” na akamfanyisha mazoezi ya kutembea kwenye kokoto na changarawe. Kesho yake, Ijumaa usiku, Desemba 29, akazaliwa Mzee wa Atikali”. Wakati huo, wadogo wa “Mzee wa Atikali” (Prof. Lucy, Gona, Sr. Angela, Sam na Caro) na mwanaye, Attu, walikuwa hawajazaliwa.
Mama Siwale ampa zawadi Mzee wa Atikali
Mzee wa Atikali alisoma Shule ya Msingi Oysterbay. Matokeo ya darasa la saba yalipotoka, Mama Siwale ndiye aliyempa taarifa Mzee wa Atikali. Matokeo hayo yalionyesha kuwa kati ya wanafunzi 170, wanafunzi 40 (28 wasichana na 12 wavulana) walikuwa wamefaulu. Mama Siwale akampa zawadi ya mpunga. Mzee wa Atikali akapanga na Fred, mtoto mkubwa wa Mama Siwale kwenda “Shamba la Bibi” Desemba 20, ambako kulikuwa na mechi kati ya Taifa Stars na Super Eagles ya Nigeria. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kwenda uwanja huo. Siku moja kabla, Mzee wa Atikali akapelekwa kwenda kulala kwa Mama Siwale mkabala na ilipo Ikulu. Keshoye, Fred na Mzee wa Atikali wakaenda Posta, wakagombea UDA hadi kufika uwanjani ambako walikaa mzunguko na watu walikuwa wengi mno. Mzee wa Atikali alikuwa mdogo sana hivyo hata kuona mpira ilikuwa ni shughuli pevu!. Mechi ikaisha 1-1. Mzee wa Atikali akapoteana na Fred na mabasi ya UDA yalikuwa machache mno, yasingeuweza umati wote ule.

Ikabidi Mzee wa Atikali aunge Azimio la Arusha! Akiwa na watu wengine, alistukia amefika mjini saa mbili usiku. Hata hivyo, akawa hajui atafikaje Ikulu. Akaulizia na kisha akaweza kwenda “Central Police Station” na kuelezea masaibu yaliyomkuta na kuwa anataka kwenda kwa Waziri Mama Siwale lakini hajui jinsi ya kufika Ikulu. Akaingizwa ndani ya Defender” na kufikishwa! Akamkuta kaka yake, Fred, amebanisha nje akiogopa kuingia ndani kwani alijua angeulizwa “Mdogo wako yuko wapi?”
Mama Siwale ainusuru familia ya Mzee wa Atikali
Wazazi wa Mzee wa Atikali na watoto wao waliwahi kuishi Mbezi kwa Musuguri. Usiku mmoja, “Wazee wa Kazi” waliligeuza eneo hilo kuwa “Ukanda wa Gaza”! Walivamia nyumba zisizopungua 10 na kujeruhi wakaaji vibaya sana. Baba wa Mzee wa Atikali aliumizwa hadi akalazwa Muhimbili, Mzee wa Atikali akiwa boarding shule ya sekondari ya Malangali. Mama Siwale alienda akamchukua mdogo wake, Mama Sophia na watoto wengine, na kukaa nao kwa mwaka mzima kwake mkabala na Ikulu. Baada ya kutoka hospitali, baba yake Mzee wa Atikali aliamua kumuuzia nyumba hiyo Paul Rupia kwani hiyo ilikuwa ni mara ya pili eneo hilo kuvamiwa.
Mama Tabitha Siwale alikuwa mwanamke mchapakazi na mwaminifu aliyelifanyia mengi Taifa lake. Alipoteuliwa kuwa Waziri hakuwaangusha wanawake na kupelekea wanawake wengine kuja kupewa nafasi kubwa za uongozi na sasa tunaye mwanamke, Mama Samia Suluhu Hassan, kama Rais wa nchi.
Mama Siwale ameacha watoto wawili
Mzee Edmond Siwale alifariki 2016, Fred alifariki 1993 na Abel alifariki 2008. Mary na Dk Maka ndiyo walio hai.
Msiba wa Mama Siwale uko Mikocheni mkabala na nyumba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Mazishi yatafanyika Jumamosi, Machi 15, 2025, Kinondoni.
Wizara ya Wanawake mna mpango wa kumuenzi vipi Mama Siwale?
Pumzika kwa amani mama Tabitha Ijumba Siwale