Arusha. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva, amesema ni muhimu kuwa na mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na utekelezaji wa maazimio na ahadi zinazotolewa na nchi wanachama ili kuimarisha uwajibikaji na kufanikisha utekelezaji wa ajenda za ujumuishaji wa kanda.
Akihutubia mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Huduma za Umma na Mawaziri jijini Arusha leo Machi 14, 2025, Nduva amesema EAC inakabiliwa na changamoto za utekelezaji wa maazimio kutokana na masilahi yanayoshindana kati ya nchi wanachama, ucheleweshaji wa michango ya kifedha, na ukosefu wa mbinu ya pamoja ya kikanda.
“Ukosefu wa mfumo thabiti wa ufuatiliaji unasababisha ahadi nzuri kubaki kwenye makaratasi bila utekelezaji wa vitendo. Hii inaathiri kasi ya ujumuishaji wa kanda na manufaa yanayopaswa kuwafikia wananchi,” amesema Nduva.
Ameongeza kuwa ucheleweshaji wa utekelezaji wa maamuzi ya sera umesababisha kuendelea kwa vikwazo visivyo vya kiforodha (NTBs), huku mifumo ya kisheria isiyo na ulinganifu ikiathiri biashara ya kikanda.
Mkutano huo, ulioandaliwa na Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (Esami) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), ulihimiza umuhimu wa uwajibikaji wa nchi wanachama katika kutekeleza maazimio ya kanda.
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC, Beatrice Askul, ambaye pia ni Waziri wa EAC na Maendeleo ya Kanda wa Kenya, amesema mfumo wa ufuatiliaji utawezesha maendeleo yanayoweza kupimwa na kusaidia viongozi wa serikali kusimamia kwa ufanisi ajenda ya ujumuishaji wa EAC.
“Utafiti unaonyesha kuwa nchi zikikubaliana na kutekeleza ahadi zao kwa pamoja, wananchi wote watanufaika zaidi. Changamoto kubwa ni nchi zingine kushindwa kutekeleza majukumu waliyoahidi,” amesema Askul.
Kwa upande wake, Mkuu wa Watumishi wa Umma na Katibu Mkuu wa Serikali ya Kenya, Felix Koskei, amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuzingatia wajibu wao wa kifedha kwa EAC ili kuimarisha ujumuishaji wa kanda, ikiwemo kulipa michango yote kwa wakati.
“Pia kuna haja ya kutekeleza maagizo ya wakuu wa nchi wa EAC, kuridhia itifaki na nyaraka rasmi, na kuimarisha uaminifu kati ya nchi wanachama,” amesema Koskei.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Esami, Dk Peter Kiuluku ameeleza kuwa baadhi ya changamoto zinazokwamisha ujumuishaji wa EAC ni sera zisizoratibiwa, ukosefu wa rasilimali za kutosha, na udhaifu katika mifumo ya ushirikiano wa utawala wa kitaifa na vipaumbele vya kanda.
“Kuna haja ya kuimarisha mifumo ya ushirikiano kati ya wakuu wa huduma za umma ili kurahisisha mwingiliano wa kitaasisi na kuwezesha utekelezaji wa maazimio ya kikanda,” amesema Kiuluku.
Aidha, amesema kuwa ili kuimarisha utekelezaji wa maazimio, kuna umuhimu wa kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa maendeleo unaohakikisha ahadi za kitaifa zinazingatia malengo ya kanda.
Katika hitimisho la kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Dennis Londo, alipendekeza kuwa mijadala ya aina hii ifanyike mara kwa mara ili kuleta mawazo mapya yatakayosaidia utekelezaji wa maazimio ya jumuiya.
“Tunapaswa kuweka msisitizo kwa yale tunayojipangia, nani muhimu kufuatilia yale yaliyotekelezwa, changamoto zilizojitokeza, na nini kifanyike ili kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya ujumuishaji,” amesema Londo.
Amesema mkutano huo wa kimkakati umewaleta pamoja Wakuu wa Huduma za Umma na Mawaziri kutoka nchi wanachama wa EAC pamoja na wanazuoni kutoka vyuo vikuu ili kujadili hatua za kuhakikisha utekelezaji wa maazimio ya kanda kwa ufanisi zaidi.