Dar es Salaam. Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonesha wanaume wapo hatarini zaidi kufa kwa magonjwa yasiyo ambukiza (NCDs), ikilinganishwa na wanawake.
Takwimu hizo zinaonesha vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ambukiza vimeongezeka kutoka asilimia 34 mwaka 2019 mpaka kufikia 38.8 mwaka 2021.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Health Promotion Tanzania (HDT), Dk Peter Bujari wakati wa kutambulisha ubunifu mpya wa kifurushi cha virutubishi cha ‘SeamossPlus’ kilichoundwa kwa kutumia mwani ili kuimarisha utendaji kazi wa afya ya mwili.
Hata hivyo takwimu za mfumo wa taarifa za uendeshaji wa huduma za afya (Mtuha) zinaonesha ongezeko la wagonjwa wa NCDs 2,626,107 walitibiwa kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na wagonjwa 3,140,067 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la wagonjwa 513,960 au asilimia 20.
Akizinukuu takwimu za WHO, Dk Bujari amesema uwezekano wa mtu kufa katika umri wa miaka 15 mpaka 60 katika kila watu 1,000, wanaume ni 245 na wanawake ni 185.
“Lakini kwa kila wanaume 100,000 wa Tanzania uwezekano wa kufa kwa magonjwa yasiyo ambukiza ni kwa idadi ya 557 ikilinganishwa na 498 kwa wanawake,” amesema Dk Bujari.
Amesema hatari ya magonjwa yasiyo ambukiza inaongezeka kwa takwimu za mwaka 2021 magonjwa ya mfumo wa upumuaji yaliongoza kwa vifo, ikifuatiwa na malaria, kifua kikuu, Ukimwi, shinikizo la damu kwa asilimia 33.9, magonjwa ya moyo kukosa hewa asilimia 31.5.
“Jumla ya magonjwa yote kwa upana wake ya kuambukiza, vifo vya mama na mtoto pamoja na lishe vinachangia asilimia 51 ya vifo vyote. Magonjwa yasiyo ambukiza manne kwa ukubwa wake yalichangia kwa asilimia 38.8 na magonjwa ya ajali yanachangia asilimia 8.4,” amesema Dk Bujari.
Amesema ongezeko kwa wanaume linatokana na vyakula visivyofaa, kutofanya mazoezi, uzito kupita kiasi na vitambi, presha, kisukari, matumizi ya pombe na uvutaji wa sigara.
Kwa mujibu wa Dk Bujari, vyakula visivyofaa, kutofanya mazoezi na uzito kupita kiasi vinachangia kwa zaidi ya asilimia 65 mpaka 75 ya vifo, na kwamba hatua zisipochukuliwa kufikia mwaka 2030 kutakua na ongezeko zaidi la vifo vitokanavyo na magonjwa hayo.
Akizinukuu takwimu hizo, Dk Bujari amesema walio wengi wanajua kuhusu vihatarishi hivyo, lakini bado wanaishi maisha hatarishi hasa wanaume.
Tabia za wanaume kutoangalia afya zao ni moja ya vyanzo vya tatizo hilo, kama anavyosema mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Ali Mzige.
Amesema wanawake ni wepesi wa kwenda kuangalia afya zao vituo vya afya pindi wanapohisi tofauti, ukilinganisha na wanaume hivyo kupata huduma mapema kabla tatizo kuwa kubwa.
“Mwanamume anachelewa kidogo kutafuta matibabu kuliko mwanamke na ukitazama kwa sasa wanaume wanaanza kushindana na wanawake kwa unene na vitambi na ni vichocheo vya magonjwa hayo.”
Pia Dk Mzige amesema wanawake wana vikundi vingi ikiwemo marafiki, vikoba na makundi sogozi ambako wanazungumza yanayowasibu ikilinganishwa na wanaume.
Kwa mujibu wa Dk Mzige vipimo vya mara kwa mara ni muhimu kwa mwanaume yeyote anayetaka kubaki na afya njema wakati wote, akisisitiza unywaji maji wa kutosha.
“Wanaume wengi hawanywi maji ya kutosha, ndiyo tatizo. Usisubiri mpaka figo zako ziharibike. Lakini kupiga mswaki, kuoga ni vitu muhimu sana kwa mwanaume ili ubaki na afya njema.”
“Waende kliniki maalumu kufanyiwa hivyo vipimo, kuna programu muhimu pia watapewa pamoja na vidokezo mbalimbali. Huduma zipo, shida wanaume hawafuatilii na wengi hawajui hata kama kuna hizo huduma.”
Awali akizungumzia kuhusu SeamossPlus, Dk Bujari amesema una manufaa ya kiafya ikiwemo kuboresha kusagika kwa chakula hasa kwa wingi wa nyuzinyuzi iliyonazo.
“Inaboresha kinga ya mwili kwa sababu ina madini ya chuma na Fuxanthine ambayo ina antioxidant. Pia inalisha na kunawirisha ngozi na kuboresha afya ya uzazi ya wanaume kwa sababu ya kuwa na zinc ambayo husaidia homoni ya testosterone kubakia kwenye kiwango sahihi,” amesema Dk Bujari.