Morogoro. Watu wawili wa familia moja wamefariki dunia katika kijiji cha Kalenga kata ya Mofu Halmashauri ya Mlimba baada ya kupigwa na radi wakiwa shamba, huku mmoja akipata mshtuko kutokana na radi hiyo.
Akizungumzia tukio hilo diwani wa kata ya Mofu, Graison Mgonela amesema tukio hilo limetokea Machi 13 mwaka huu saa 11 jioni ambapo mvua iliyoambatana na upepo na radi ilianza kunyesha.
Diwani huyo amewataja waliofariki katika tukio hilo ni Ally Abdallah pamoja na mtoto wa kaka yake Kulwa Paulo wote ni wakazi wa kata ya Mofu.
“Huyu mwanamke aliyepata mshtuko ametambulika kwa jina moja la mama Ibu na kwa sasa yuko anaendelea vizuri,” amesema Mgonela.
Amesema kabla ya radi kupiga watu hao walipoona mvua na upepo mkali walienda kukaa chini ya mti kujikinga wasiloe na mvua, ambapo mwanamke huyo alikimbilia kwenye kibanda kilichopo jirani na shamba.
“Radi hii ilivyopiga huyu mama hakupata majeraha bali alipata mshtuko na anaendelea vizuri,” amesema diwani Mgonela.
Amesema tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kata hiyo na limewashtua na kuwasikitisha wananchi wengi wa eneo hilo.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mofu Agripinus Manyerere amethibitisha vifo hivyo ambapo amesema mwili mmoja kati ya hiyo miwili umepelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Fransis, ukisubiri kusafirishwa kwenda kwao Tanga.