Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemteua mwamuzi Ahmed Arajiga kuamua mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Pyramids ya Misri dhidi ya FAR Rabat ya Morocco ambao utageuka kama Dabi ya Kariakoo ndogo.
Pyramids itakutana na FAR Rabat kwenye mchezo wa kwanza utakaopigwa Uwanja wa June 30 mjini Cairo, Misri, mechi ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Ndani ya mchezo huo Arajiga atakuwa kwenye vita nyingine ya Simba na Yanga kutokana na kuwapo kwa Wakongomani wawili mshambuliaji Fiston Mayele anayeichezea Pyramids anayekutana na mshindani wake beki Henock Inonga.
Mayele alikuwa kwenye vita kubwa dhidi ya Inonga wakati wakiwa hapa Tanzania wakifanyiana bato ndani ya uwanja kuzipigania timu zao kipindi hicho Mayele akikipiga Yanga na Inonga akiwa Simba.
Arajiga atawakumbushia vita hiyo atakapokutana na wawili hao Aprili Mosi, 2025 kwenye mechi hiyo kabla ya timu hizo kwenda kumalizana wiki Moja baadaye nchini Morocco.
Mchezo huo sio tu utafuatiliwa zaidi na Waarabu, bali hata Watanzania mashabiki wa Simba na Yanga wakikumbushia juu ya wachezaji hao wawili ambao waliondoka hapa nchini kwa nyakati tofauti.