FA yampa mzuka Mcameroon | Mwanaspoti

BAADA ya Kagera Sugar kumrejesha aliyekuwa mshambuliaji wake raia wa Cameroon, Moubarack Amza kutoka Namungo, nyota huyo amesema anajisikia furaha katika timu hiyo kutokana na kuanza kufunga mabao.

Nyota huyo amerejea baada ya awali kujiunga na Kagera Sugar Januari, mwaka jana, kwa mkopo wa miezi sita akitokea Ihefu ambayo sasa ni Singida Black Stars, kisha kuondoka msimu huu na kutua kwa ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Amza alisema licha ya kutofunga bao lolote Ligi Kuu Bara, ila kitendo cha kufunga mabao mawili katika ushindi wa kikosi hicho wa 3-0, dhidi ya Namungo FC kwenye Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya 32, kimempa motisha.

“Kama mshambuliaji usipofunga huwa kwa kiasi kikubwa inakutoa mchezoni lakini nashukuru nimefunga mabao mawili ambayo yametupa nafasi ya kusonga hatua inayofuata, huu ni wakati wangu mzuri wa kufanya vizuri kila nikipewa nafasi uwanjani,” alisema.

Bao lingine katika mchezo huo lilifungwa na Mkenya Saphan Siwa na kuipeleka timu hiyo hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) na sasa itacheza na Tabora United iliyoitoa Transit Camp kwa penalti 4-2, baada ya sare ya bao 1-1.

Amza hadi sasa hajafunga bao lolote la Ligi Kuu Bara ingawa msimu bora kwake nchini ambao hata yeye anakiri ulikuwa wa 2022-2023, wakati akikichezea kikosi cha ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union na alimaliza kwa kufunga mabao saba.

Katika kipindi chote cha miezi sita aliyoichezea Kagera Sugar, alifunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara huku mara yake ya mwisho kufunga ilikuwa ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0, dhidi ya Tabora United, mechi ikipigwa Aprili 17, 2024.

Related Posts