Fadlu: Sasa tunawataka Al-Masry | Mwanaspoti

BAADA ya ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika Ligi Kuu Bara, Kocha wa Simba, Fadlu Davids ameonyesha kuridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na kikosi chake akisisitiza kuwa kazi bado haijaisha, kwani malengo yao makubwa msimu huu wa 2024/25 ni kushinda mataji, lakini akituma salamu kwa wapinzani wao wajao, Al Masry.

Simba inakutana na Al-Masry katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho, Aprili 2, mwaka huu mjini Cairo, Misri

“Nina furaha kwa wachezaji na mashabiki wetu, lakini sasa tunapaswa kuweka matokeo haya nyuma na kuangalia mbele. Tunakabiliwa na mchezo mgumu wa robo fainali dhidi ya Al-Masry, hivyo tunapaswa kujipanga kwa kina ili kuhakikisha tunasonga mbele kwenye michuano hii ya kimataifa,” amesema Fadlu.

Kocha huyo ameeleza kuwa baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, wachezaji wake watakuwa na mapumziko mafupi kwa ajili ya kurejesha nguvu, isipokuwa wale ambao wameitwa kwenye timu za taifa. 

“Sasa tunahitaji siku chache za kupumzika, kurejesha nguvu na kujiandaa kwa undani kwa mchezo wetu wa robo fainali. Wachezaji walioteuliwa kwenda kwenye timu zao za taifa hawatapata muda wa kupumzika, lakini kwa wale waliobaki tutatumia muda huu kufanya maandalizi ya kina kuhakikisha tunaingia uwanjani tukiwa kwenye kiwango bora zaidi,” ameeleza.

Fadlu amezungumzia pia kuhusu maandalizi yao kuelekea mchezo dhidi ya Al-Masry, akisisitiza kuwa licha ya ushindi mnono walioupata, bado wana mambo mengi ya kuboresha kabla ya kucheza dhidi ya timu hiyo kutoka Misri. 

“Baada ya ushindi wa aina hii, wachezaji wanapata hali ya kujiamini zaidi, lakini pia kuna mambo kadhaa ambayo lazima tuyaboreshe. Sitaki kuwa na mtazamo wa juu kupita kiasi. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya. Tunakwenda kucheza dhidi ya timu inayoshikilia nafasi ya nne kwenye ligi ya Misri, na ni wapinzani wenye uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya Afrika,” amesema.

Ameongeza kuwa ingawa wachezaji wake wako kwenye hali nzuri, lakini haitoshi kutegemea kujiamini pekee bali wanapaswa kuongeza umakini na kufanyia kazi upungufu ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini. 

“Ndiyo, tunaingia kwenye mchezo huu tukiwa na hali nzuri ya kujiamini, lakini hatuwezi kutegemea hilo pekee. Tunahitaji maandalizi ya kina na nidhamu ya hali ya juu ili kuhakikisha tunatinga nusu fainali ya mashindano haya,” alisisitiza kocha huyo.

Ushindi jana umeifanya Simba kufikisha pointi 57, ikikaribia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa nyuma kwa alama moja dhidi ya vinara Yanga SC wenye pointi 58. 

Fadlu ambaye ameiongoza Simba katika michezo 16 mfululizo bila ya kupoteza sawa na dakika 1,440 katika ligi tangu wafungwa na Yanga kwenye duru la kwanza kwa bao 1-0, amesema matokeo hayo yalikuwa na umuhimu mkubwa kwa Simba kwani yamewarejesha kwenye mbio za ubingwa na kuwarudishia morali kuelekea mechi zinazofuata. 

“Huu ulikuwa mchezo muhimu kwetu, tulikuwa na kiporo ambacho tulihitaji kukitumia kupunguza pengo la alama dhidi ya vinara wa ligi. Wachezaji wangu walionesha kiwango cha juu na tulistahili ushindi huu mkubwa,” amesema.

“Lakini cha muhimu zaidi ni kuwa tulihakikisha hatukuruhusu shambulizi lolote lenye madhara kwa lango letu. Tumemaliza mchezo bila kuruhusu hata shuti moja lililolenga lango letu, jambo ambalo ni muhimu kwa uimara wa kikosi chetu.”

Kocha huyo mzaliwa wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa ingawa Simba ilipata ushindi mkubwa, lakini kulikuwa na nafasi ya kuongeza mabao zaidi akisisitiza kuwa anajivunia kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake. 

“Ninafurahia sana kiwango cha wachezaji. Tulicheza kwa kushambulia kwa kasi na kujilinda vizuri, naamini tungeweza kufunga mabao zaidi. Hata hivyo, ushindi wa 6-0 ni jambo la kujivunia na ni moja ya michezo muhimu sana tuliyoicheza msimu huu,” ameongeza. 

Related Posts