Hamdi ajichorea ramani ya ubingwa

LIGI Kuu imesimama hadi Aprili Mosi wakati ngarambe ya lala salama itapigwa hadi bingwa wa msimu huu atakapopatikana Mei 25, lakini kocha wa watetezi wa taji hilo Yanga, Miloud Hamdi amejipata kwa kukiangalia kikosi alichonacho na mechi zilizosalia anaona nafasi ya kutetea ni kubwa.

Yanga imesaliwa na mechi nane ikiwamo wa Dabi ya Kariakoo iliyokwama kupigwa Machi 8, ikiwa kileleni kwa sasa ikikusanya pointi 58 kupitia mechi 22, ilihali Simba ikiwa nyuma ya watetezi hao na pointi 54 (kabla ya mechi ya leo), ambayo nayo imesaliwa na idadi kama hiyo.

Kocha Hamdi ametamba kinachompa jeuri na kuona kama ana nafasi kubwa ya kumaliza vyema msimu ni aina ya wachezaji alionao na mechi zilizosalia ambazo anaamini wakizikomalia mwanzo mwisho kila kitu kitakuwa poa, licha ya kukiri kasi ya Wekundu wa Msimbazi inawatisha kileleni.

Bila kuweka pambano lao ambalo bado halijafahamika litachezwa lini baada ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi, timu hizo zina nafasi ya kumaliza msimu zikitofautiana pointi moja au nne kutegemea na matokeo ya jumla iwapo tu kama zitashinda zote. Yanga ikishinda zote ikiwamo ya dabi itamaliza msimu na pointi 82, lakini kama itapoteza kwa Simba itafikisha 79 na kuipa nafasi Simba kubeba taji kwani wapinzani hao kama watashinda zote ikiwamo ya Yanga itafuikisha 81. Iwapo itapoteza mbele ya Yanga itamaliza msimu na pointi 78.

Yanga imebakiza mechi dhidi ya Simba, Tabora United, Coastal Union, Azam FC, Singida Black Stars, Namungo, Tanzania Prisons na Dodoma Jiji, huku kati ya hizo ni vikosi viwili tu vilivyoitibulia ktika duru la kwanza Azam iliyowafunga bao 1-0 na Tabora United iliyowafumua 3-1, huku wengine wakitembeza vipigo nje ndani, kitu kianchoonyesha Hamdi na jeshi alilonalo wana kazi nyepesi.

Kwa upande wa Simba, imebakiza mechi dhidi ya Yanga, Mashujaa, JKT Tanzania, Pamba Jiji, KMC, Singida Black Stars, KenGold na Kagera Sugar, huku ikiwa na mzigo mwepesi zaidi kwani katika duru la kwanza ilipoteza mbele ya Yanga kwa bao 1-0, huku wapinzani wengine wote ikiwatembezea vipigo.

Kwa hesabu za haraka inaonyesha kwamba Simba ina kazi nyepesi kulinganisha na Yanga, licha ya kocha Hamdi kusisitiza, anataka kuweka heshima kwa mechi zilizosalia ikiwamo wapinzani waliowanyima raha katika duru la kwanza ambalo hakuwepo wakati Yanga ikipoteza.

Kama mechi ya dabi itapigwa na Simba kupata ushindi mbele ya Yanga, kazi itakuwa rahisi na itajiweka pazuri kubeba taji inalolisotea kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, lakini kama itatelekeza kwa mtani, basi ijue kabisa ndoto ya Hamdi itatimia kwa kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo.

Simba na Yanga katika mechi nane ilizonazo kila mmoja, zitacheza nne nyumbani na nyingine kma hizo ugenini, lakini rekodi zinaonyesha Wekundu hao kama walivyo Yanga, wao kambi ni popote kwa maana hupata matokeo bila kujali inacheza wapi.

Hata hivyo Simba imefungwa mabao manne nyumbani na manne mengine ugenini, tofauti na Yanga ambayo nyumbani imefungwa mabao nane na ugenini imeruhusu moja, kitu kinachoonyesha lolote linaweza kutokea kabla ya msimu kufungwa Mei 25.

Akizungumza na Mwanaspoti kocha Hamdi alisema, namna ambavyo kikosi chake kimeenea hasa wakati huu ambao kila mchezaji yuko sawa, kuna mpa utulivu na uhakika zaidi wa kupambania ubingwa.

Alisema, kila idara kwenye kikosi chake kuna nyota wenye uwezo mkubwa, ambapo hataki kumuacha mchezaji nyuma katika kutoa nafasi katika mechi zilizosalia.

“Imekuwa rahisi kufanya mzunguko,hasa wakati ambao tutakuwa tunaamua mechi zetu mapema, kwa kutengeneza ushindi mkubwa kipindi cha kwanza inatoa nafasi kuwapa mapumziko wengine na wengine kucheza.

“Mfano; Ndani ya siku chache nitakuwa na mabeki watatu wa kulia Kibwana, Israel Mwenda na hata Yao, ambaye amerejea na anakiwango kizuri, hivyo kitu pekee kitawapa nafasi sawa ni mzunguko katika kila mechi.

Kocha Hamdi aliongeza kwa kufichua kuwapa likizo fupi ya siku sita mastaa wa timu hiyo, huku akisema anahitaji kucheza mechi za kirafiki kabla ya kurejea katika Ligi na michuano ya Kombe la Shirikisho.

“Nimewapa wachezaji wangu mapumziko ya siku sita, lakini watakaporudi nitaangalia uwezekano wa kuwa na mechi ndogo za kirafiki, ili kurudisha ubora wao uwanjani kwa kuwa watakwenda kucheza mechi ngumu ugenini,” alisema Hamdi

Kabla ya Yanga kucheza mchezo wa 23 wa ligi dhidi ya Tabora United utakaopigwa Aprili 1 ikiwa ugenini, itamaliza kwanza mechi ya hatua ya 16 Bora dhidi ya Songea United ambayo hata hivyo bado haijafahamika itapigwa lini, japo Yanga itakuwa wenyeji wa mchezo huo.

v Tabora United (ugenini)

v Coastal UnionĀ  (nyumbani)

v Fountain Gate (ugenini)

v Kagera Sugar (nyumbani)

Related Posts