Ilivyohitimishwa safari ya Naomi Kilimanjaro, gumzo miaka mitano

Mwanga. Familia imehitimisha safari ya maisha ya duniani ya Naomi Marijani, ikizika mabaki ya mwili wake yaliyopatikana baada ya tukio la mauaji lililofanyika miaka mitano iliyopita. 

Mei 15, 2019 nyumbani kwake Gezaulole, wilayani Kigamboni, Naomi aliuawa na mumewe, Hamis Luwongo, kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku. Masalia ya mwili na majivu alikwenda kuyazika shambani na kupanda migomba juu yake, ambayo yalifukuliwa wakati wa upelelezi wa tukio hilo la mauaji.

Leo Machi 15, 2025, mabaki ya mwili wa Naomi aliyeuawa akiwa na miaka 36 yamezikwa katika Kijiji cha Mbambua, Kata ya Lembeni wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Luwongo ambaye ni mfanyabiashara alishtakiwa kwa mauaji ya Naomi katika kesi ya jinai kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Hamidu Mwanga katika hukumu aliyoitoa Februari 26, 2025 alimuhukumu Luwongo kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa, Naomi baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi 14 na vielelezo 10 uliotolewa mahakamani hapo.

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mabaki ya mwili wa Naomi Marijani wakati wa kwenda kuzika nyumbani kwao katika Kijiji cha Mbambua, Kata ya Lembeni wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Alfajiri ya leo Machi 15, waombolezaji wakiwa na mabaki ya mwili wa Naomi yakiwa ndani ya jeneza jeupe walifika kijijini Mbambua ambako mazishi yalifanyika mchana kwenye makaburi ya ukoo.

Robert Marijani, baba ndogo wa Naomi akizungumza wakati wa kuaga mwili wa mwanaye, amewashukuru wote walioshiriki kupigania haki ya mtoto wao Naomi.

“Tunamshukuru Mungu kwa kutufikisha hapa leo, lakini niwashukuru wote kwa ushirikiano mlioonyesha kwetu mpaka tunampumzisha mtoto wetu Naomi, haya mengine tunamwachia Mungu,” amesema.

Salma Marijani, mdogo wake na Naomi amesema wataendelea kumkumbuka, akieleza alikuwa jasiri, mchapakazi na alikuwa akivaa viatu vya wengine (kutoa msaada).

“Mimi na dada yangu tulikuwa tukishirikiana mambo mengi, naweza kusema Naomi alikuwa mchapakazi kwelikweli, alikuwa ni mwanamke jasiri katika kupambana, alikuwa anajituma na ni mtafutaji.

“Naomi alikuwa mhitimu wa shahada ya kwanza, alipomaliza chuo alipata kazi ya kuajiriwa, baadaye aliacha kazi akawa mjasiriamali,” amesema.

Amesema alikuwa akipapamba katika biashara na alifanikiwa.

“Alikuwa na maduka aliuza kila kitu, alikuwa kiongozi wa makundi mbalimbali ya ujasiriamali ambayo hata mimi alinishirikisha. Alikuwa na maduka ya dawa, alikuwa akisambaza gesi maeneo mbalimbali, kwa ujumla alikuwa mpambanaji,” amesema.

Ismail Marijani, kaka wa Naomi akisoma wasifu wa marehemu amesema dada yao alikuwa mtu mwema kwao na kwa wengine, alikuwa mpenda haki, hivyo watamkumbuka kwa mengi.

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mabaki ya mwili wa Naomi Marijani wakati wa kwenda kuzika nyumbani kwao katika Kijiji cha Mbambua, Kata ya Lembeni wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

“Tunatambua sisi sote siku moja tutalala milele, lakini Naomi nyota yake imezimwa wakati bado tukiwa tunamhitaji,” amesema.

Amesema dada yao alichukia dhuluma, alikuwa msikivu kwa kila mtu na hakuwa mgomvi.

“Dada Naomi alichukia dhuluma, alikuwa mpenda haki, alikuwa dada mwema sana. Naomi alikuwa na sifa ya usikivu ni mtu ambaye hata ukitaka kumwelezea jambo lako alikuwa anakusikiliza na aliweza kuvaa viatu vya watu wengine.

“Tunamkumbuka kama mama aliyekuwa mpambanaji, familia kwake ilikuwa namba moja, ilikuwa ni ngumu kusikia amegombana na mtu, alikuwa tayari kutumia muda na gharama zake kukusikiliza,” amesema.

Mchungaji wa Kanisa la TAG- Gezaulole, Jacob Chinegu amesema Naomi alikuwa akishiriki matukio ya kanisa.

“Nitoe pole kwa wanakijiji cha Mbambua, niwatie moyo familia ya Marijani kwa msiba huu mzito. Naomi alikuwa anapenda kanisa, nakumbuka wakati kanisa linaanza yeye ndiye aliyekuwa mwanamke wa kwanza kutununulia viti vya kanisa,” amesema.

Amesema alikuwa na uchaji, aliweza kuwaunganisha wanawake katika makundi ya ujasiriamali.

Florah Chilangazi, aliyekuwa rafiki wa Naomi amesema walipoteza dada aliyewasaidia.

“Tumeishi na familia ya dada Naomi tukiwa wote Mbeya tangu tukiwa shule ya msingi, katika ukuaji wetu sikuwahi kuona dada akigombana na mtu, tutaongozana kwenda shule tutarudi vizuri na hata akiona mtu anagombana na mwingine atamuonya.

“Alikuwa mpole, ukishindwa kukaa na Naomi hata jiwe utashindwa kukaa nalo, alikuwa dada anayeweza kubeba jambo la mtu akalifanya kama lake,” amesema.

Related Posts