OR-TAMISEMI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeuagiza uongozi wa Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera, kuhakikisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Biija na Shule ya Sekondari ya Amali (Ufundi) Mubunda unakamilika ifikapo Aprili 2025 ili wanafunzi waanze masomo.
Miradi hiyo inafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia mradi wa SEQUIP, ambapo kila shule imepokea Sh.Milioni 584.2 na ujenzi wake unafanyika kwa njia ya ‘Force Account’.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Justin Nyamoga, akizungumza katika ziara ya kamati ya kukagua ujenzi huo, amesema Shule ya Biija imejengwa ili kupunguza umbali wa wanafunzi wanaosafiri kutoka maeneo ya mbali na kuagiza pindi ujenzi utakapokamilika, walimu waletwe haraka na wanafunzi waanze masomo bila kuchelewa.
Pia, amesisitiza kuwa wanafunzi wanaotembea mwendo mrefu wahamishiwe katika shule hiyo ili kurahisisha upatikanaji wa elimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amehimiza viongozi wa Halmashauri kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na miundombinu ya shule inatunzwa ili iweze kuwanufaisha vizazi vingi na kwamba ucheleweshaji wa miradi haukubaliki.
Aidha, Mhe. Katimba amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kuimarisha matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa manunuzi ya umma (NEST) ili kuepusha ucheleweshaji wa miradi.