KAMPUNI YA USAFIRISHAJI YA MWEMBE LOGISTICS YAREJESHA TABASAMU KWA WANAFUNZI WALIOPATA JANGA LA MOTO MAKANYA SEKONDARI.

NA WILLIUM PAUL, SAME.

KAMPUNI ya usafirishaji ya Mwembe logistics imetoa msaada wa magodoro, vyandarua, matraka pamoja na taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Makanya wilayani Same mkoani Kilimanjaro waliopata hadha ya bweni kuteketea kwa moto Februari 14 mwaka huu majira ya saa kumi na mbili asubuhi

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa Mkuu wa wilaya ya Same, Afisa Masoko na Uhusiano wa kampuni hiyo, Janeth Mtui alisema kuwa, msaada huo ni sehemu ya kuwatia moyo na kuwafariji Wanafunzi hao kutokana na madhara waliyoyapata.

Janeth alisema kuwa, kampuni yao imekuwa ikijitolea kirejesha katika jamii kile ambacho wamekuwa wakikipata lengo ni kuhakikisha jamii inafurahi kupitia kampuni hiyo.

“Bweni lililotokea kwa moto lilikuwa likikaliwa na Wanafunzi wa kike wapatao 22 na vitu vyote vilivyokuwamo viliteketea kwa moto hivyo sisi kama Mwembe logistics tumeleta magodoro 22, matraka, neti na taulo za kike lengo ni kuhakikisha tunawarejeshea tabasamu pamoja na kuwafariji ili waweze kufikia malengo yao” alisema Janeth.

Aidha aliongeza kuwa, kampuni hiyo imekuwa na tabia ya kuwashika mkono jamii na kudai kuwa wataendelea kushikamana na jamii katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni aliwashukuru wadau mbalimbali ambao waliojitolea kwa hali na mali katika kuwakimbilia Wanafunzi hao na kuwarejeshea tabasamu.

Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kuwaomba wadau mbalimbali wenye nia njema kuendelea kuisaidia shule hiyo ili kuwezesha kurejesha mazingira kama yalivyokuwa awali ikiwamo kujenga jengo hilo jipya la bweni lililoteketea kwa moto.

“Wanafunzi ambao mlikuwa mnatumia lile bweni lililoungua niwatoe hofu mtaendelea kusalia kwenye bweni la Wanafunzi wa kidato cha tano na sita mpaka pale ambapo tutakapojenga bweni jipya maana hili lililoungua limeharibika sana na halifai kukarabatiwa” alisema Kasilda.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Same, Abdallah Mnyambo aliwashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitoa tangu kutokea kwa tatizo hilo.

Alitumia pia nafasi hiyo, kuwataka walimu na Wanafunzi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya shule kwani serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha sekta ya elimu.


 

Related Posts