Kiama kwa waingiza simu feki Tanzania

Dar es Salaam. Serikali imetangaza kiama kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa feki za mawasiliano kufuatia kuanzishwa kwa maabara ya uidhinishaji vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki.

Maabara hiyo iliyo chini ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapima na kuhakiki sampuli za vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki kuthibitisha usalama wa matumizi kabla havijaingizwa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari amewaambia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa maabara hiyo ambayo uwekezaji wake ni takribani Sh7.4 bilioni imeiwezesha uhakiki wa vipimo vya vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki.

Dk Bakari amesema upimaji huo pia pia unalenga kuwajengea imani watumiaji wa vifaa hivyo simu za mkononi, vishikwambi na kompyuta mpakato.

“Mawasiliano hayawezi kutokea kama hakutakuwa na vifaa vinavyotumika kuwasiliana, miongoni mwa majukumu yetu ni kukagua na kuthibitisha vifaa vya mawasiliano vinavyoingia nchini.

“Hapa namaanisha toleo lolote la kifaa cha mawasiliano kabla hakijaingia nchini lazima mtengenezaji alete sampuli aliyobuni tuikague kwenye maabara. Kupitia maabaara tunaweza kujua kama kifaa kimekidhi ubora unaohitajika,” amesema na kuongeza:

“Mfano kubaini kiwango cha nishati ya umeme katika simu husika, kwa sababu kinapozidi ni hatari kwa matumizi ya binadamu, ili kuhakikisha vifaa viko salama lazima hiyo sampuli tuipime kuthibitisha ubora wake na kila kifaa kinafanya kazi kulingana na dhumuni la kutengenezwa kwake, kusiwe na mwingiliano na vifaa vingine.”

Amesema tangu kuanza kufanya kazi kwa maabara mwaka huu imeshapima sampuli 148 za vifaa tofauti tofauti vya mawasiliano na kuthibitisha usalama wa matumizi.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi amesema kuwepo maabara hiyo nchini kumeleta ufanisi kwenye uidhinishaji wa vifaa va mawasiliano.

Amesema kuanzishwa maabara hiyo kunaashiria nia ya dhati ya Serikali ya katika kujenga miundombinu na mifumo thabiti ya kidijitali.

 “Uwepo wa maabara hii ni hatua muhimu katika safari ya taifa letu kuhakikisha vifaa vya mawasiliano vinavyotumika nchini ni salama kwa watumiaji pamoja na mitandao.  Tunapoingia zama hizi za uchumi wa kidijiti, hitaji la vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki vyenye ubora wa juu, sanifu na salama ni la umuhimu mkubwa.

“Niwatangazie kiama wale wote waliokuwa wanaingiza vifaa vya kielektroniki kijanja janja, sasa hivi Serikali iko macho na makini, nasi kama wizara tutaongeza umakini kupitia TCRA kuhakikisha vifaa vyote vinavyoingia nchini vimethibitishwa,” amesema Maryprisca.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso ameitaka TCRA kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha vifaa vyote vya mawasiliano vinapimwa ubora wake na ikionekana viko chini ya viwango visiingie kwenye soko.

“TCRA ina maabara itapima sampuli, sasa kama hakutakuwa na ushirikiano kati yake na TBS tija ya hii maabara haitaonekana. Nasema hili la ushirikiano kwa sababu tumeona vita ya kupambana na uhalifu wa mtandao inapaswa kushirikisha wenzetu wa polisi lakini ushirikiano wao umekuwa mdogo. Tusingependa hilo litokee kwenye udhibiti wa vifaa vya mawasiliano, taasisi zote zinapaswa kushirikiana,” amesema.

Kakoso pia amesisitiza mamlaka hiyo kutengeneza mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili Watanzania wawe na uwezo wa kubaini vifaa vya mawasiliano vilivyoidhinishwa.

Nchi zingine zenye maabara kama hiyo barani Afrika ni Afrika Kusini, Tunisia, Ghana, Nigeria, Cameroon, Benin, Guinea, Togo, Senegal, Mali na Mauritania.

Related Posts