Kocha Azam aanza kupiga hesabu za msimu ujao

KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema katika mipango yake msimu ujao, kuhusu usajili anataka wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuipambania timu hiyo.

Zikiwa zimesalia mechi saba tu kwa timu hiyo kuhitimisha msimu huu, kocha huyo tayari ameshapiga hesabu za msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema Azam tayari ina wachezaji wazuri vijana lakini wanahitajika kuchanganyika na waliokomaa na wenye ubora zaidi.

Alisema kikosi walichonacho sasa wapo wachezaji ambao wameshindwa kuwa na mwendelezo mazuri ndiyo sababu inayowanyima kuwa na matokeo bora kila wakati, hivyo jambo hilo hataki litokee msimu ujao.

“Kuna wachezaji ambao wasipobadilika kwenye mechi zilizobaki sitakuwa na sababu za kuendelea nao, wapo ambao Azam inatakiwa kuhakikisha inawabakiza ili kutunza msingi wa timu.

“Msimu ujao nahitaji kuwa na mastaa wenye uzoefu mkubwa ambao utaiweka timu sehemu nzuri zaidi ya sasa, lakini wapo ambao watapungua pia,” alisema kocha huyo ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kuinoa timu hiyo.

Taoussi ambaye kwa sasa anapambana kuona hatoki nafasi tatu za juu kwenye msimamo, anaamini kikosi hicho bado kina uwezo mkubwa wa kupambana na wakongwe Simba na Yanga katika suala zima la kuwania ubingwa kwa msimu ujao.

Ikumbukwe, Azam iliyoanza kushiriki Ligi Kuu Bara mwaka 2008, imebeba ubingwa wa ligi mara moja msimu wa 2013-2014 huku misimu mingine ikiziachia Simba na Yanga zikipokezana na timu hizo zimekuwa zikifanya hivyo tangu mwaka 2001 kabla ya Azam kutibua 2013-2014.

Related Posts