Kocha Hamdi aanza upya na Ikanga

BAADA ya kuonyesha uwezo wake ndani ya dakika 66 alizopewa winga mpya wa Yanga, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’, kocha wake Miloud Hamdi ametaja mambo makuu mawili ambayo Mkongo huyo anatakiwa kuyazingatia kwa sasa.

Winga huyo aliyetua Yanga dirisha dogo lililofungwa Januari 15, 2025, amecheza mechi mbili tu, moja ya ligi dhidi ya Pamba Jiji na alipewa dakika 21 kisha dakika 45 dhidi ya Coastal Union katika Kombe la FA.

Ni wazi, kiwango cha winga huyo taratibu kimeanza kumvutia kocha Hamdi, japokuwa bado hajafunga wala kutengeneza nafasi ya bao ‘asisti’.

Akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema, Ikanga ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na kwa sasa ndio anaingia kwenye kikosi hivyo hana haraka ya kumwona akifanya makubwa.

Alisema Ikanga ana mambo makubwa mawili ya kuzingatia ambayo yatazidi kumfanya awe bora zaidi, huku akimtaka kuondoa presha ili afanikiwe.

“Jambo la kwanza anatakiwa kuzoeana na wenzake, lazima wenzake wajue anahitaji pasi za aina gani ili kuisadia timu kupata matokeo mazuri.

“Kitu cha pili anatakiwa kuingia kwenye mifumo ya timu na azijue falsafa zake, kuhusu kufunga nimemwambia sitaki aweke akilini sana jambo hilo kwani ishu hiyo siyo kazi yake kubwa, mabao yatakuja tu.

“Sitaki afanye vitu kwa presha ya mashabiki, naamini baada ya miezi michache Ikanga atakuja kuwa mchezaji tegemeo kwenye timu na hatari kwenye ligi endapo akizingatia haya,” alisema kocha Hamdi.

Ikanga mbali na kucheza winga zote mbili, kulia na kushoto, pia ana uwezo wa kutumika kama mshambuliaji wa kati anapocheza Prince Dube, Kennedy Musonda na Clement Mzize.

Related Posts