Makundi haya hatarini kupata maambukizi ya Mpox

Dodoma. Wakati ugonjwa wa Mpox ukiendelea kustua nchini na tahadhali mbalimbali zikiendelea kutolewa ni ukayajua makundi yaliyoko hatarini kupata ugonjwa huo.

Machi 10 mwaka huu Waziri wa Afya Jenista Mhagama alitangaza kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Mpox nchini ambapo alisema kuwa jumla ya wagonjwa wawili wameripotiwa kuwa na ugonjwa huo jijini Dar es salaam.

Baada ya kubainika kuwapo wagonjwa hao Serikali ilichukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuiweka Tanzania katika sehemu salama dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo ikiwemo kutoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya inaelezwa kuwa  ugonjwa huo huanzia kwa Wanyama wa porini kabla ya kufikia kwa wanyama wa nyumbani ambao wapo karibu na binadamu na kuwafikishia kwa urahisi.

Hata hivyo wataalamu hao pia wamebainisha juu ya uwepo wa baadhi ya makundi ya watu katika jamii ambayo yapo hatarini zaidi kukumbana na ugonjwa wakiwamo wenye kinga dhaifu kama vile wazee, watoto na watu wenye magonjwa sugu.

Mratibu wa Elimu ya Afya kwa umma Mkoa wa Dodoma, Dk Nassoro Matuzya, amesema ugonjwa huo huambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kula nyama pori za wanyama walioathirika.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Machi 15, 2025 Dk Matuzya amesema  makundi hayo yanaweza kuathirika zaidi na maambukizi hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kinga za miili yao, magonjwa ya kudumu lakini pia hali za kiafya walizonazo kwa wakati ambao watakumbana na ugonjwa huo.

‘’Sayansi inasema watu wenye kinga dhaifu ikiwemo wazee au watu wenye umri mkubwa ,watoto na watu wenye magonjwa sugu wapo katika hatari zaidi ya kupatwa na ugonjwa huu hatari,”amesema Dk Matuzya.

Hata hivyo ameongeza kuwa kundi lingine ni la watu walio karibu na wagonjwa wa walioathirika ikiwemo wahudumu wa afya au watu wengine walio katika mazingira yanayomzunguka mgonjwa kama hawatachukua tahadhari zinazoshauriwa.

Aidha Matuzya amesema ili watu waepukane  na ugonjwa huo hawana budi kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuvaa barakoa, kuepuka kugusana na wagonjwa lakini pia kutochangia vitu mbalimbali na waathirika.

‘’Ugonjwa huu ni hatari na unachukua siku kuanzia 21 ili kuanza kuonyesha dalili za awali hivyo kama mtu atakuwa amekaa karibu na mtu anayehisiwa  kuwa na ugonjwa huu, hana budi kufika katika vituo vya afya ili kupatiwa matibabu kulingana  na dalili alizonazo.’’

Amewataka watu kuepuka  kugusa majimaji ya mwathirika wa ugonjwa huo, kuchangia vitu vyenye ncha kali, kujamiiana na mwathirika pamoja na kuchangia mavazi ama kugusa mavazi ya mwathirika wa ugonjwa, ikiwemo matandiko.

Amewataka Watanzania kwenye makundi yote kuchukua tahadhari na hatua stahiki  ili kupambana na ugonjwa huo na kukumbuka kuwa kwa sasa hauna tiba, lakini mtu anaweza kujiweka salama kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Miongoni mwa namna bora ya kujikinga ni kunawa mikono kwa maji tiririka.

Lakini pia kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya pindi mtu atakapohisi ama atakapoona kuwa ana dalili za ugonjwa  huo au kupiga simu bure kwa kupitia namba 199.

Dalili za awali za Mpox ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa, misuli, uvimbe na maumivu ya mgongo.

Baada ya homa,  upele unaweza kutokea, mara nyingi huanza kwenye uso kisha kuenea kwenye sehemu nyingine za mwili, mara nyingi viganja vya mikono na nyayo za miguu.

Upele, ambao unaweza kuwasha au kuumiza sana, hubadilika na kupitia hatua tofauti kabla ya kutengeneza kipele, ambacho hutumbuka baadaye. Vidonda vinaweza kusababisha makovu.

Maambukizi kawaida huisha yenyewe na hudumu kati ya siku 14 na 21.

Ugonjwa ukikomaa zaidi vidonda licha ya kuenea mwili mzima, huenea mpaka mdomoni, machoni na sehemu za siri.

Related Posts